Na Grace Michael, Lindi
MWENYEKITI
wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Bw. Deogratius Ntunkamazina
amewataka watoa huduma za afya nchini kuutumia Mfuko huo kwa uzalendo
ili uweze kunufaisha Watanzania wote.
Amesema
kuwa endapo Mfuko huo watautumia kwa ulafi na kwa kughubikwa na
udanganyifu utafilisika na kushindwa kufikia malengo yanayokusudiwa na
Serikali ya kuhakikisha asilimia kubwa ya wananchi wanakuwa kwenye
utaratibu wa Bima ya Afya.
Bw.
Ntunkamazina aliyasema hayo jana wakati akitoa salaam za Bodi ya Mfuko
huo kwenye Mkutano wa Wadau uliofanyika mkoani Lindi uliokutanisha
wadau mbalimbali wakiwemo wakitoa huduma, wanachama, viongozi wa
kiserikali, kidini na wadau wengine.
"Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya ni fursa nzuri ya kuboresha huduma za afya
nchini hivyo tumieni fursa hii kwa uzalendo mkubwa sana ili baadae
wananchi wote waweze kunufaika na Mfuko huu. Mkiwa walafi na kuweka
udanganyifu mwingi katika kuandaa madai yenu mtaufilisi Mfuko huu,"
alisema Ntunkamazina.
Mwenyekiti
huyo wa Bodi alitumia maneno ya Kiongozi shupavu na mwana Falsafa
Mahtma Gandhi kiongozi wa India, ambaye alinukuu maneno yake aliyowahi
kusema kuwa “Dunia hii ina raslimali za kutosha mahitaji muhimu ya kila
mtu lakini haina raslimali za kutosha ulafi wa kila mtu” mwisho wa
kunukuu. Hivyo kwa kauli hiyo alisisitiza uzalendo katika kuutumia
Mfuko huo.
Alisema kuwa endapo Mfuko huo utatumika ipasavyo Watanzania wote watanufaika lakini ukitumika isivyo utafilisika.
"Jamani
hata Rais wetu ana ndoto kubwa na angependa kabisa aondokapo
madarakani mwaka 2015 aache Watanzania asilimia 50 wakiwa chini ya
utaratibu wa Bima ya Afya hivyo tumuungeni mkono kwa kila mdau kutimiza
wajibu wake," alisema.
Naye
Kaimu Mkoa wa Lindi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Magalula Said
naye aliwasisitiza viongozi wote wa Halmashauri kuhakikisha wanaongeza
juhudi katika uhamasishaji wa wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya wa
Jamii.
"Nimejaribu
kupitia takwimu za hapa Lindi na nimegundua kuwa tunazidi kuporomoka
katika suala hili la CHF hivyo kila mmoja kwa nafasi yake ajipange
kuhakikisha hali hii inaondoka na wananchi wetu wanajiunga na Bima
kwani ndio mkombozi wa afya kwa wote hivyo ni lazima tuiweke kama
agenda ya kudumu katika vikao vyetu,' alisema.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emanuel Humba aliwaomba viongozi wa kisiasa
wakiwemo madiwani kuhakikisha wanasimamia vyema fedha zitokanazo na
mifuko hiyo ili ziweze kutumika katika matumizi sahihi hasa ya dawa.
No comments:
Post a Comment