SHIRIKA LA NDEGE LA ETIHAD LATOA MSAADA KWA KITUO CHA WATOTO JINJA, UGANDA.
Wanachama
wa mpango wa kujitolea wa "i-Volunteer" wa shirika la ndege la Etihad
wakiwa kwenye picha ya pamoja na watoto wa kituo cha kulea watoto cha
“Whisper Children’s Home” kilichopo Jinja-Uganda walipotembelea kituo
hicho kutoa msaada mwishoni mwa juma.
SHIRIKA
la ndege la Etihad limezindua rasmi mpango wake wa kuzifikia jamii
nchini Uganda ambapo wametoa misaada ya tiketi za ndege, mablanketi na
vifaa vya shule kwa kituo cha kulea watoto “Whisper Children’s Home”
kilichopo Mutai, wilaya ya Jinja, Uganda.
Kituo
hicho cha watoto kilianzishwa Mei 2011 lengo kuu likiwa ni kuboresha
maisha ya watoto walioathirika kwa utapiamlo na wanaoishi katika
mazingira hatarishi kijijini hapo.
Akitoa
maoni yake juu ya msaada walioupata kutoka Shirika la ndege la Etihad,
Bi. Veronika Cejpkova, Mwanzilishi na Mkurugenzi wa kituo hicho alisema:
“Tunashukuru kwa moyo wa ukarimu uliooneshwa na shirika la ndege la
Etihad. Tiketi hizi zitasaidia sana katika kuwasafirisha wanaojitolea na
wafanyakazi kutoka Ulaya wanaoamua kushiriki na sisi katika shughuli
zetu za kila siku hapa kituoni.
“Mpaka
sasa tunawatunza watoto takribani 30. Mahitaji yao ni pamoja na
matunzo, vifaa vya shule kama vile kalamu za wino, kalamu za rangi na
vitabu ambavyo vitawasaidia watoto katika masomo na kuwaburudisha.”
Shirika
hili la ndege limetoa msaada huu chini ya mpango wake wa uwajibikaji
kwa jamii uitwayo “Giving Together” unaohusisha programu mbalimbali
zinazotoa misaada kwa wahitaji waliopo katika mtandao wao duniani.
Toyin
Alaran, Meneja Mkuu wa shirika la ndege la Etihad, Uganda, alisema:
“Shirika letu limejikita kuleta maendeleo na kusaidia jamii zilizopo
katika mtandao wetu. Tumeona kituo cha watoto cha Whisper kama mwangaza
wa matumaini kwa watoto na familia zenye kuishi katika mazingira magumu
na tumefurahi kupata nafasi ya kushirikiana nao katika hili.
“Msaada
huu kutoka Etihad unadhihirisha msimamo wetu wa kuunga mkono mipango
inayolenga kuleta maendeleo katika jamii na kuboresha maisha ya
wanajamii katika sekta mbalimbali kama elimu kwa watoto na kuboresha
hali ya maisha ya wasiojiweza,” alisema Bw. Alaran.
Etihad
ilikabidhi zaidi ya mablanketi 200 kwa kituo hicho cha watoto.
Waliosindikiza katika ugeni huo ni pamoja na; Toyin Alaran, Meneja Mkuu
wa Etihad, Uganda, Maclynn Kemigisha, Mratibu Masoko wa Etihad, Uganda,
Luzelle Boado-Berger, Afisa wa Mipango Endelevu wa Etihad na wanachama
watano wa mpango wa “i Volunteer” wa Etihad, waliowasili Uganda kutoka
makao makuu ya Shirika hilo huko Abu Dhabi ili kuungana na wenzao katika
kutimiza azma hii.
Tangu
kuanzishwa kwake, timu ya Whisper imetoa huduma ya kwanza na msaada kwa
watoto zaidi ya 2000 waliathiriwa na funza na imeboresha sehemu za
kulala za watoto wa kijiji cha Mutai na vijiji vingine kanda ya Busoga
kwa kuwapa vitanda, magodoro, vyandarua, mablanketi na mashuka.
Whisper
pia imezipatia familia mafunzo ya jinsi ya kuandaa chakula, usafi wa
mwili na uzazi wa mipango, imewafundisha wazee jinsi ya kukarabati
nyumba zao, au kutunza bustani ya mbogamboga, imewapa watoto usafiri wa
kwendea shule, na chakula na kuni kwa familia zinazopitia kipindi kigumu
wakati wa mvua kali.
No comments:
Post a Comment