WATANZANIA WAISHIO NJE KUTOPIGA KURA OKTOBA - PINDA
*Waziri Mkuu aomba Watanzania waiombee nchi yao
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema Watanzania waishio ughaibuni hawataweza
kupiga kura wakiwa nje ya nchi kwenye uchaguzi wa Oktoba mwaka huu, kwa
sababu kuna mambo kadhaa ambayo Serikali inabidi iyatekeleze kabla ya
zoezi hilo kufanyika.
Ametoa
kauli hiyo jana jioni (Jumamosi, Aprili 11, 2015) wakati akizungumza na
baadhi ya Watanzania waishio Uingereza kwenye makazi ya Balozi wa
Tanzania nchini humo, Balozi Peter Kallaghe, yaliyoko Highgate,
Kaskazini mwa Jiji la London.
Akizungumza
na Watanzania hao ambao baadhi yao walitoka miji ya Leicester na
Manchester, Waziri Mkuu alisema mambo makuu ambayo yanahitaji
kuzingatiwa kabla hawajaweza kupiga kura ni pamoja na marekebisho ya
Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya mwaka 1985 pamoja na uandikishwaji wa
Watanzania wana-Diaspora kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
"Najua
suala kubwa ambalo mnatamani kulisikia ni hili la Watanzania kuweza
kupiga kura kutokea huku mliko. Hili inawezekana lisifanikiwe wakati huu
kwa sababu kuna mambo muhimu ya kuzingatia kubwa likiwa ni marekebisho
ya sheria na hili zoezi la uandikishaji wapigakura kwenye Daftari la
Kudumu la Wapigakura. Ili mwananchi aweze kupiga kura ni lazima awe
ameandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura," alisema.
"Itabidi
tuangalie kama mashine za BVR nazo zitapaswa kupelekwa kwenye kila
ubalozi ili watu wetu waweze kujiandikisha au itafutwe njia nyingine ya
kufanikisha hilo jambo.... lakini watu wa Tume wanaamini kwamba jambo
hilo linaweza kufanikiwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2020," aliongeza.
Waziri
Mkuu ambaye aliwapatia nakala zisizopungua 40 za Katiba
Inayopendekezwa, alitumia fursa hiyo kuwasisitizia wasome kwa makini
Katiba hiyo ili wawe na uelewa mpana na kisha wailinganishe na Katiba ya
mwaka 1977 ambayo inatumika hivi sasa ili waweze kubaini kama kweli
haina kitu kama ambavyo watu wengine wanadai.
"Moja
ya changamoto zinazotukabili huko nyumbani ni mjadala kuhusu Katiba
Inayopendekezwa... wako watu wanaosema kwamba hakuna kitu kipya kabisa
kwenye Katiba Inayopendekezwa, lakini mimi nasema hayo ni mawazo yao
binafsi," alisema.
Akifafanua
kuhusu Katiba hiyo, Waziri Mkuu alisema: "Mimi nilikuwa sehemu ya Bunge
Maalum la Katiba, ni kweli tulibadili baadhi ya vipengele lakini kwa
nia ya kuiboresha. Ninawasihi kila mmoja wenu aisome na kuangalia kama
kweli hamna kitu au kuna kitu kipya ikilinganishwa na Katiba inayotumika
hivi sasa. Angalieni na pimeni, je kuna kitu kimeboreshwa au la?"
Aliwasihi
waendelee kuiombea nchi ya Tanzania ili iendelee kuwa na amani na
utulivu na hasa katika kipindi hiki ambacho inakabiliwa na uchaguzi wa
madiwani, wabunge na Rais. "Ninawasihi muendelee kuiombea nchi yetu ili
ipate viongozi wazuri ambao watajali maslahi ya wengi," aliongeza.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, APRILI 12, 2015.
No comments:
Post a Comment