Header Ads

Uchambuzi Wa Habari: Gazeti Uhuru Linapofichua Njama Za Kufunika Madudu Ya Ekelege Wa TBS

Ndugu zangu,

Mhariri wa gazeti la Uhuru anaitwa Jaqueline Liana.  Hakika anastahili pongezi kwa kazi yake njema kwa  taifa. Niweke wazi, katika magazeti yote niliyoyapitia siku ya jana Jumamosi, gazeti la Uhuru ndilo kwangu

lilitia fora.


Kati ya habari kadhaa  zenye kumfumbua macho msomaji, gazeti Uhuru lilibeba habari tatu zenye umuhimu mkubwa kwa nchi yetu; habari kuuilikuwa na kichwa cha habari; “ Ripoti uozo TBS yavaiva- Njama za

kuizima zaandaliwa”. Nyingine ni; “ Majengo ya UDA kuhifadhi makontena”. Na mwisho ni wito; “Tumieni mitandao ya kijamiikuhabarisha”. Habari hizo mbili za mwisho nitazichambua katika siku za usoni kutokana na ufinyu wa muda kwa sasa.


Nianze basi  na habari kuu iliyotokana na uchunguzi wa gazeti Uhuru; Mwandishi anabainisha, kuwa taarifa ya uozo wa ndani ya Shirika laViwango Tanzania  ( TBS) imekamilika na imewasilishwa  kwa Spika wa

Bunge kwa hatua zaidi.

Kwamba wakati  ripoti hiyo ikiwa tayari na huku Watanzania wakisubiri hatua gani zitachukuliwa, gazeti Uhuru limebaini uwepo wa mipangokabambe inayosukwa ili  kuzima na kuwalinda  vigogo wa shirika hilo la

umma wanaotuhumiwa  kufanya mambo kinyume na taratibu.


Uhuru linabainisha, kuwa Kamati  ya Bunge ya Mahesabu ya Mashirika ya Umma  ( POAC) imebaini matatizo mengi ndani ya TBS  yakiwemo ukaguzi wa bidhaa usiokidhi viwango na mazingira  ya rushwa miongoni mwa maofisa waandamizi.  Na kutokana na kubainika kwa madudu hayo, Kamati

hiyo  imependekeza  baadhi ya maofisa waandamizi wa TBS, akiwemo Mkurugenzi Mkuu, Charles Ekelege, wasimamishwe kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili.


Na licha ya Kamati ya Bunge kukamilisha ripoti yake hiyo, uchunguzi uliofanywa na  gazeti la Uhuru  unaonyesha kuwa kuna mipango inasukwa kwa kuwahusisha baadhi ya wabunge, ofisi ya bunge na wizara ya Viwanda na Biashara  kuhakikisha suala hilo halifikishwi katika mkutano ujao wa bunge na kuchukuliwa hatua.



Uchunguzi wa  gazeti Uhuru  unazidi  kuonyesha , kuwa  wahusika wa mpango  huo ni baadhi ya wabunge ambao ni wajumbe  wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali ( PAC) na maofisa wa bunge  kwa kushirikiana na maofisa  waandamizi wa wizara.



Kwa mujibu wa gazeti Uhuru, mmoja wa  wajumbe wa POAC alithibitisha kuwepo  mipango hiyo  na kuongeza kuwa, baadhi ya wabunge wanatumiwa katika suala hilo.


Mjumbe mwingine wa kamati hiyo alisema, kwa uozo ndani ya TBS uko wazi kwa sababu hata wafanyakazi  wa chini wamekuwa wakilalamika  kuwa wanakwamishwa kufanya kazi ipasavyo na viongozi wao.



” Wafanyakazi  walitueleza kuwa wanapogundua  kuna bidhaa mbovu na kuzizuia, wafanyabiashara wanazungumza moja kwa moja  na viongozi wa juu  wa shirika na matokeo yake bidhaa zile ambazo ni mbovu zinaruhusiwa kutumika.


” Kama watu walioaminiwa na kupewa nafasi kuongoza shirika kubwa kama hili wanakiuka utaratibu, kuna imani gani tena? Hii inaonyesha watu hawa  hawana  nia njema  na maisha yetu na wako tayari kuwaangamiza

Watanzania kwa sababu  ya maslahi yao”. Alisema mjumbe huyo.


Kwa mujibu wa gazeti Uhuru,  Makamu wa Mwenyekiti wa kamati hiyo ya bunge ,  Mbunge wa Ludewa , Deo Filikunjombe, ameweka  bayana msimamo wa kamati yake, kuwa hawatakubali  suala hilo kuzimwa au kumalizwa kinyemela kwa sababu  kufanya hivyo  ni kukubali  Watanzania waendelee kuangamia kwa kutumia bidhaa mbovu.



Filikunjombe anasema;

” Upo ushahidi  kwamba zipo bidhaa zisizo na  viwango kama kondomu, mafuta ya kupikia, matairi, vyakula na blue band ambazo zina nembo ya TBS na zinatumika. Huu ni uoza mkubwa, ni lazima tufike  mahali tuseme
basi. Ni lazima TBS isafishwe na wahusika wa mchezo huu mchafu lazima waondolewe haraka”. ( Deo Filikunjombe, Uhuru Februari 25, 2012)

Naam, kila Mtanzania mwenye mapenzi mema na nchi yake  hana budi kuwaunga  mkono wahariri wa mfano wa Jacqueiline Liana na wabunge wa mfano wa Deo Filikunjombe. Ni Watanzania wenzetu  walioonyesha

utayari wa kujitoa muhanga  kuipigania nchi yao dhidi ya vitendo vya kifisadi kama hiki cha TBS chenye hatari ya kuliangamiza taifa.

Maggid Mjengwa,


Iringa

Jumapili, Februari 26, 2012

No comments:

Powered by Blogger.