Umeme wa Gridi kuokoa bilioni 30 kwa mwaka Njombe, Ruvuma
Na Greyson Mwase, Ruvuma
Waziri
wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema kuwa mara baada ya kukamilika
kwa mradi mkubwa wa umeme utakaopelekea mikoa ya Njombe na Ruvuma
kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa Septemba, 20 mwaka huu, Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco) litaweza kuokoa shilingi bilioni 30 zilizokuwa
zikitumika kama gharama ya kuendesha mitambo ya kuzalishia umeme
inayotumia mafuta mazito katika mikoa hiyo.
Waziri
Kalemani aliyasema hayo mapema jana tarehe 04 Juni, 2018 kwa nyakati
tofauti kupitia mikutano na vijiji vya Suluti kilichopo wilayani
Namtumbo na Lukumbule na Mkowela vilivyopo wilayani Tunduru mkoani
Ruvuma kwenye ziara yake ya kukagua njia ya Makambako – Songea, vijiji
vinavyotakiwa kuunganishwa na umeme wa Gridi ya Taifa pamoja na miradi
ya usambazaji wa umeme vijijini inayosimamiwa na Wakala wa Nishati
Vijijini (REA)
Katika
ziara hiyo Waziri Kalemani aliambatana na wataalam kutoka Wizara ya
Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Wakala wa Nishati Vijijini
(REA), wakandarasi pamoja na wakuu wa wilaya husika.
Dkt.
Kalemani alisema kuwa, shirika la Tanesco limekuwa likitumia gharama
kubwa ya shilingi bilioni 30 kwa mwaka kama gharama ya uendeshaji wa
mitambo inayotumia mafuta mazito katika mikoa ya Njombe na Ruvuma na
kusababisha hasara badala ya faida.
Alisema
kuwa, mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vya
Makambako, Madaba na Songea mapema mwezi Septemba mikoa ya Njombe na
Ruvuma itaunganishwa rasmi na Gridi ya Taifa na kuokoa kiasi cha
shilingi bilioni 30 kinachotumika kuendesha mitambo ya mafuta mazito
gharama ambazo ni kubwa tofauti na mapato ya shirika hilo ya shilingi
bilioni tisa kwa mwaka kwa mikoa husika.
Aidha,
aliongeza kuwa kuingizwa katika Gridi ya Taifa kwa mikoa ya Njombe na
Ruvuma kutapelekea uwepo wa nishati ya uhakika na kuchochea ukuaji wa
uchumi.
Kazi ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Songea kilichopo mkoani Ruvuma ikiendelea.
Waziri
wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kulia) akizungumza na waandishi wa
habari mara baada ya ziara yake katika kituo cha kupoza umeme cha Songea
kilichopo mkoani Ruvuma. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet
Mgema na kushoto ni Msimamizi wa Mradi wa Umeme wa Makambako – Songea,
Mhandisi Didas Lyamuya.
Sehemu
ya wananchi wa kijiji cha Suluti kilichopo wilayani Namtumbo mkoani
Ruvuma wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo
pichani) alipokuwa akiwaelezea mikakati ya serikali katika upelekaji wa
huduma ya umeme vijijini.
Waziri
wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akielezea matumizi ya kifaa cha Umeme
Tayari (UMETA) kwa wananchi wa kijiji cha Suluti kilichopo wilayani
Namtumbo mkoani Ruvuma (hawapo pichani)
Waziri
wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akielezea mikakati ya Wizara ya
Nishati kwenye usambazaji wa miundombinu ya umeme katika mikoa ya Njombe
na Ruvuma katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Omela.
No comments:
Post a Comment