JPM Kuzindua Pasipoti ya Kielektroniki
Jonas Kamaleki- MAELEZO
Rais
 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. John Pombe Magufuli kesho 
atazindua Pasipoti Mpya ya Tanzania ya kielektroniki jijini Dar es 
Salaam.
Uzinduzi huo utafanyika Jumatano, Januari 31, 2018 kuanzia saa moja na nusu asubuhi, Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji, Kurasini Dar es salaam.
Hayo 
yamesemwa na Mrakibu wa Uhamiaji ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Idara ya 
Uhamiaji, Ali Mtanda katika mahojiano maalum na Idara ya Habari 
(MAELEZO).Mtanda amesema kuwa Pasipoti Mpya ya Tanzania ya kielektroniki
 ni sehemu ya Mfumo wa Uhamiaji Mtandao ambao utakuwa na visa, vibali 
mbali mbali na manejimenti mipakani.
Kwa
 kuwa teknolojia inazidi kukua, Tanzania haiwezi kubaki nyuma ndiyo 
maana imeamua kuingia katika masuala ya digiti. Uzinduzi huu 
utahudhuriwa pia na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la 
Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein.Marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano
 wa Tanzania, waheshimiwa, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin William Mkapa na 
Jakaya Mrisho Kikwete na viongozi wengine wa Serikali wanatarajiwa 
kuhudhuria uzinduzi huo kwa mujibu wa Mtanda.
Tanzania
 imekuwa mstari wa mbele katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati 
katika kutoa huduma zake kwa wananchi kwa njia ya mtandao. Ikumbukwe 
kuwa usajili wa makampuni chini ya Wakala wa Usajili wa Biashara na 
Leseni (BRELA) wamezindua usajili wa makampuni kwa njia ya mtandao, 
miamala ya pesa inafanyika kwa kiwango kikubwa kwa njia ya mtandao na 
kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi ikiwepo kulipa kodi mbali 
mbali.
 

 
 
 
 
 
No comments:
Post a Comment