SERIKALI YASISITIZA UWAZI SHUGHULI ZA MADINI
Kampuni za Madini nchini zimetakiwa kufanya shughuli zake kwa uwazi sambamba na kufuata Sheria za nchi ili kuepuka migongano.
Wito
 huo umetolewa jijini Dar es Salaam Januari 29, 2018 na Katibu Mkuu wa 
Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila kwenye mkutano na Balozi wa 
Canada nchini, Ian Myles aliyeambatana na Mshauri masuala ya Uwajibikaji
 kwa Jamii kwenye Tasnia ya Uziduaji kutoka Serikali ya Canada, Jeffrey 
Davidson.
Ujumbe
 huo ulimtembelea Katibu Mkuu Msanjila kwa lengo la kujadiliana masuala 
mbalimbali kwenye Sekta ya Madini ikiwemo suala la Sheria ya Madini, 
masuala ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) yanayofanywa na kampuni 
mbalimbali zikiwemo za kutoka nchini Canada na matarajio ya Serikali kwa
 kampuni (wawekezaji).
Profesa
 Msanjila alisisitiza kuwa kampuni zinazofanya shughuli zake nchini 
zinalazimika kufuata taratibu na sheria za nchi ili kujijengea mazingira
 rafiki ya utekelezaji wa shughuli husika.
Alisema
 lengo la Serikali ni kuhakikisha Sekta ya Madini inanufaisha Taifa kwa 
ujumla sambamba na wawekezaji na alibainisha kwamba lengo hilo 
litafikiwa ikiwa kampuni husika zitatekeleza wajibu wake kwa uwazi 
kulingana na matakwa ya sheria.
“Kampuni
 zinazojihusisha na shuguli za madini zinapaswa kufanya shughuli zake 
kwa usahihi na uwazi,” alisisitiza Profesa Msanjila.
Aidha,
 Profesa Msanjila alisisitiza kuwa kampuni zinazojihusisha na shughuli 
za madini nchini, zinapaswa kupata taarifa sahihi kutoka kwa Wataalam 
waliopo Serikalini ili kupata mwelekeo sahihi wa dhamira ya Serikali.
“Kampuni
 zinatakiwa kupata taarifa sahihi kutoka kwa vyanzo sahihi ili kufanya 
shughuli zake kwa usahihi,” alisisitiza Profesa Msanjila.
Profesa
 Msanjila vilevile alizungumzia dhamira ya Serikali ya kuhakikisha 
madini yanayochimbwa nchini yanaongezwa thamani kabla hayajasafirishwa 
nje ili kukuza uchumi wa Taifa.
“Madini
 yakiongezwa thamani hapa nchini, faida ni nyingi ikiwemo ajira na pia 
mapato yataongezeka kwani tutakuwa tumeelewa thamani halisi ya madini 
husika, kabla hayajasafirishwa,” alisema.
Ili
 kufikia dhamira hiyo, Profesa Msanjila alisema Serikali ipo kwenye 
mazungumzo na kampuni zilizoonyesha nia ya kujenga viwanda vya kuyeyusha
 na kusafisha madini (smelting and refining).
Mbali
 na hilo, Profesa Msanjila alizungumzia suala la uwezeshaji wachimbaji 
wadogo wa madini ambapo alisema Serikali imedhamiria kuhakikisha kwamba 
wananufaika ipasavyo na shughuli zao sambamba na mchango wao kwenye pato
 la Taifa kuonekana.
Alielezea
 jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kuwawezesha 
wachimbaji wadogo ikiwemo uanzishaji wa vituo vya mafunzo vya mfano 
(centre of excellence) ambavyo alivitaja baadhi yake kuwa ni Kituo cha 
Tanga, Geita na Mtwara.
Kwa
 upande wake Balozi Myles alisema ni muhimu Serikali, Wawekezaji na 
Jamii kwa ujumla kushirikiana na pia kuwa na lengo la wazi la namna ya 
kunufaika kutokana na Sekta ya Madini.
Naye
 Davidson aliahidi kuzungumza na kampuni za Canada kuelezea matarajio ya
 Serikali kwao kwa namna mbalimbali ikiwemo suala la sheria, uwajibikaji
 kwa jamii, mazingira na michango mbalimbali ya kampuni kwa maendeleo ya
 jamii.
“Nitawakumbusha
 kwamba wanawajibika si kwa wanahisa wao peke yake bali pia kwa jamii 
wanapofanyia shughuli zao,” alisema Davidson.
Mkutano
 wa Katibu Mkuu wa Madini na Balozi wa Canada nchini ulihudhuriwa na 
watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Madini akiwemo Kamishna wa Madini 
ambaye pia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kamisheni ya Madini, Profesa 
Shukrani Manya. 
 Katibu
 Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila (katikati) akizungumza
 jambo wakati wa mkutano na Balozi wa Canada nchini, Ian Myles (kulia) 
na Mshauri masuala ya Uwajibikaji kwa Jamii kwenye Tasnia ya Uziduaji 
kutoka Serikali ya Canada, Jeffrey Davidson (kushoto).
 Watendaji
 mbalimbali kutoka Wizara ya Madini na Ubalozi wa Canada nchini Tanzania
 wakifuatilia majadiliano kwenye mkutano wa Katibu Mkuu Madini na Balozi
 wa Canada (hawapo pichani). Kushoto ni Kamishna wa Madini ambaye pia ni
 Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kamisheni ya Madini, Profesa Shukrani Manya na 
kulia ni Kamishna wa Biashara Ubalozi wa Canada nchini, Anita Kundy. 
Wengine ni Maafisa kutoa Wizara ya Madini.
 Katibu
 Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila (kulia) akimsikiliza 
Mshauri masuala ya Uwajibikaji kwa Jamii kwenye Tasnia ya Uziduaji 
kutoka Serikali ya Canada, Jeffrey Davidson (katikati). Kushoto ni 
Balozi wa Canada nchini, Ian Myles (kulia). 
Katibu
 Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila (wa pili kulia) mara 
baada ya kumalizika kwa mkutano na Balozi wa Canada nchini Tanzania, Ian
 Myles (katikati). Kulia ni Kamishna wa Madini ambaye pia ni Kaimu 
Mtendaji Mkuu wa Kamisheni ya Madini, Profesa Shukrani Manya. Kutoka 
kushoto ni Mshauri masuala ya Uwajibikaji kwa Jamii kwenye Tasnia ya 
Uziduaji kutoka Serikali ya Canada, Jeffrey Davidson na Kamishna wa 
Biashara Ubalozi wa Canada nchini, Anita Kundy.
 



 
 
 
 
 
No comments:
Post a Comment