Header Ads

St Anne Maria yazawadia walioipaisha kitaifa


SHULE ya St Anne Maria ya Mbezi jijini Dar es Salaam imewazawadia wanafunzi wake waliofanya vizuri kwenye matokeo ya darasa la nne na kidato cha pili yaliyotangazwa hivi karibuni na kuipaisha kitaifa.

Akizungumza na wakati wa hafla hiyo shuleni hapo, Mkuu wa Shule hiyo, Gladius Ndyetabura, alisema shule yake imeweka utaratibu wa kuwazawadia wanafunzi hao vitu mbalimbali kama vitabu na madaftari kama motisha wa kuendelea kufanya vizuri kwenye masomo.

Alisema wanafunzi wa darasa la nne wamefanikiwa kuitoa kimasomaso shule hiyo kwa kuiwezesha kuwa ya pili kiwilaya kati ya shule 90 na ya pili Mkoa wa Dar es Salaam kati ya shule 497.Alisema mbali na kuiwezesha shule hiyo kupata mafanikio hayo kiwilaya na kimkoa pia wanafunzi wote wa darasa la nne wamefanikiwa kupata wastani wa wa ufaulu wa alama A mtihani wa kitaifa.

“Mafanikio yameanzia msingi hadi sekondari maana kwenye matokeo ya kidato cha sita mwaka 2017 shule ilikuwa ya kwanza kwa Wilaya ya Ubungo na ya  tano Mkoa wa Dar es Salaam tulitoa daraja la kwanza wanafunzi 15, daraja la pili 48, daraja la tatu 23 na daraja la nne mmoja tu na hatuna aliyepata 0,” alisema

Alisema hivi karibuni Mkoa wa Dar es Salaam uliipatia Ngao Maalum shule hiyo kama sehemu ya kutambua mchango wake katika kuinua elimu hapa nchini na kuwa miongoni mwa shule zinazofanya vizuri kitaaluma.

Alisema shule yake ilipewa ngao inayoonyesha kuwa ni miongoni mwa shule zilizofanya vizuri zaidi kwenye matokeo ya darasa la saba mwaka 2016, Best Performing Primary School in Tanzania.Alisema ngao hiyo imewapa changamoto ya kuendelea kufundisha kwa bidii ili hatimaye wapate matokeo mazuri zaidi ya mwaka huu.

Alisema ingawa shule yake imefanikiwa kuingia kumi bora kwenye matokeo ya darasa la saba mwaka huu, lakini hawajabweteka na badala yake wanafanya jitihada za kuwa namba moja.“Kwenye matokeo ya darasa la saba mwaka huu tumefanikiwa kuwa wa kwanza Wilaya ya Ubungo, tumekuwa wa pili Mkoa wa Dar es Salaam na tumekuwa wanane kitaifa sasa hii haitufanyi tubweteke tutapambana kupata nafasi za juu zaidi,” alisema 
 Mwalimu Mkuu wa shule ya St Anne Maria Academy ya Mbezi, Gladius Ndyetabura, akimkabidhi zawadi mwanafunzi aliyefanya vizuri zaidi kwenye mtihani wa darasa la nne mwaka 2017 Charles Lusato, ambaye alipata alama A kwenye masomo yote na kuwezesha shule hiyo kuwa ya pili Wilaya ya Ubungo kati ya shule 90 na ya pili pia kwa Mkoa wa Dar es Salaam kati ya shule 497.
Mwalimu Mkuu wa shule ya St Anne Maria ya Mbezi, Gladius Ndyetabura akiwasomea matokeo ya kidato cha pili wanafunzi wa shule hiyo ambayo yanaonyesha wanafunzi 48 kupata daraja la kwanza, 31 daraja la pili, 27 daraja la tatu na 13 daraja la nne na hakuna aliyepata 0.

No comments:

Powered by Blogger.