HUDUMA YA MSAADA WA KISHERIA CHINI YA RC MAKONDA WANUFAISHA WAKAZI 80, 000 DAR
NA LUGENZI KABALE
AKIITIKIA
agizo la Rais John Pombe Magufuli alilowataka wateule wake kuwa
wabunifu na kujituma ili kuwaondolea wananchi shida mbalimbali , Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ametatua migogoro takribani 8, 000
iliyowahusisha zaidi ya watu 80, 000 ndani ya takribani miezi minane
kati ya Disemba mwaka jana na Mwezi Juni mwaka huu.
Makonda
ametekeleza jukumu hilo kupitia timu ya wanasheria 35 wanaojitolea
kutoa huduma ya msaada wa kisheria bure kwa wananchi wa mkoa wa Dar es
Salaam.
Kiongozi
wa timu ya Wanasheria hao, Georgia Kamina, aliitaja baadhi ya migogoro
ambayo timu yake imekuwa ikisuluhisha kupitia Ofisi za Wakuu wa Wilaya
zote za mkoa wa Dar es Salaam kuwa ni ile ya umiliki wa ardhi na
michakato ya mirathi mahakamani na katika ngazi ya familia,
Migogoro
mingine ambayo timu hiyo ya wanasheria imekuwa ikimsaidia Makonda
kuitatua kwa kushirikiana na Wakuu wa wilaya ya Ilala (Sofia Mjema),
Kinondoni (Ally Hapi), Temeke ( Felix Lyaniva ), Ubungo (Kisare Makori )
na Kigamboni (_Hashimu Mgandilwa ) ni pamoja na ndoa na matunzo ya
watoto kwa ndoa zilizo sambaratika, ajira na mikataba ya ajira, ubakaji,
faili kupotea mahakamani, ucheleweshwaji wa kesi mahakamani, umiliki wa
nyumba, umiliki au mauziano ya ardhi, mikopo kutoka mabenki ya
biashara, uuzwaji mali mbalimbali kwa kukiuka sheria au makubaliano na
hata ukosefu wa uaminifu.
Akiiongea
kwa niaba ya Makonda, Kamina aliliambia Habari LEO katika mahojiano
maalum yaliyofanyika hivi karibuni katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa, Ilala
Boma Jijini Dar es Salaam hivi karibuni, alitaja migogoro wanayopokea na
inayotia fora katika mkoa wa Dar es Salaam kuwa ni ile inayohusisha
masuala ya mirathi, umiliki wa ardhi, ajira na mikataba kati ya waajiri
na waajiriwa, ndoa na matunzo ya watoto kwa ndoa zilizo sambaratika na
baadhi ya wananchi kuingia mikataba mibovu na mabenki katika harakati za
kupata mitaji ya biashara.
"Mheshimiwa
Paul Makonda alichukua jukumu la kuanzisha huduma ya msaada wa kisheria
bure kwa wananchi kutokana na uzoefu alioupata katika ziara ya kukutana
na wananchi aliyofanya mkoa mzima mwezi Novemba mwaka jana,"
alibainisha Kamina na kuongeza kuwa ili kuwaepusha wananchi na mchakato
mrefu na unaoumiza wa kumaliza migogoro yao mahakamani aliamua kuunda
timu ya wanasheria wa kujitolea ili kutekeleza dhamira hiyo ya
kuwasaidia wananchi wenye migogoro mbalimbali ya kisheria.
Kiongozi
wa timu ya wanasheria hao aliongeza kwa kusema kuwa Mkuu wa Mkoa
aliguswa na namna baadhi ya wananchi walivyokuwa wakipoteza mashamba,
nyumba, mali na hata kufukuzwa kazi kwa uonevu kwa kukosa uelewa wa
sheria.
“Ili
kupata suluhisho la matatizo hayo hapo juu na kwakuwa yeye binafsi akiwa
msaidizi wa Rais kwa mkoa wa Dar es Salaam basi ndio akaja na wazo la
kuanzisha kitengo cha kutatua migogoro ya kisheria kwa njia ya kutoa
huduma ya msaada kisheria bila malipo kwa wananchi katika kila wilaya ya
mkoa wa Dar es Salaam.
"Tupo
jumla ya wanasheria 35 ambao tumegawanyika katika Wilaya zote za mkoa wa
Dar es Salaam yaani Ilala, Kinondoni, Temeke, Ubungo na Kigamboni.
Tukiwa katika Ofisi za Wakuu wa Wilaya nilizotaja tunafanya kazi nao kwa
karibu sana na pengine wakati mwingine tunajumuika na Makatibu Tawala
wa Wilaya husika (DAS) na hata wakati mwingine Wakurugenzi Watendaji wa
manispaa za mkoa wa Dar es Salaam katika kutatua migogoro hiyo
kisheria,” alifichua Mkuu huyo wa Timu ya Wanasheria.
Akizungumzia
uzoefu waliopata katika kipindi cha miezi saba walichofanya kazi ya
kutoa huduma ya msaada wa kisheria bure kwa wananchi kwa kusuluhisha
migogoro mbalimbali wamegundua wananchi wengi ama hawana au wana uelewa
mdogo wa sheria na kila wakati wanafanya makosa makubwa ya kisheria
yanayoishia kuwaumiza kimaisha.
"Kuna
kina baba na kina mama wengi tu wamekuja mara baada ya kunyang'anywa
nyumba zao na mabenki kutokana na kukubali kutoa hati za nyumba hizo
kudhamini mikopo ya jamaa zao wakiamini kuwa kama kutakuwa na
kutokuelewana kati ya mabenki na ndugu zao nyumba hizo hazitauzwa jambo
ambalo sio kweli," alisimulia Kamina.
Akitaja
baadhi ya migogoro iliyowagharimu muda na juhudi za ziada kuisuluhisha,
Kamina alitaja mgogoro wa umiliki wa ardhi ya hekari 28 unaomhusisha
Ogwari Nashon na wakazi wa kijiji cha Viwege, Mbondela eneo la Chanika
katika Wilaya ya Ilala.
“Mgogoro
huu ulifika mahala ukahatarisha maisha ya ndugu Nashon kwani baadhi ya
wanakijiji wasioheshimu sheria walivamia eneo lake, kuchoma moto majengo
na kuharibu mazao kama mihogo, mananasi na michungwa.
Mara
baada ya Nashon kuja ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Ilala alikutanishwa na
wanasheria wa Mkuu wa Mkoa wanaotoa huduma ya msaada wa kisheria
bure kwa wananchi walioko wilayani hapo na kueleza tatizo lake ambapo
timu yetu iliingilia kati kwa kushirikiana na Mkuu wa wilaya ya Ilala
Sofia Mjema, ili kupata ufumbuzi wa mgogoro huo.
Ni
jambo la kutia faraja kwa sasa tumepiga hatua kubwa kuelekea kutatua
mivutano iliyokuwepo kwani Nashon ana vielelezo halali vya nyaraka za
kiserikali zinazothibitisha umiliki wa eneo hilo," alibainisha Kamina.
Licha
ya kujitokeza picha nzuri iliyojaa mafanikio ya huduma hii ya msaada wa
kisheria kwa wananchi katika Mkoa wa Dar es Salaam, Habari Leo
imearifiwa juu ya changamoto lukuki zinazowakabili watoa huduma hiyo
katika kutekeleza majukumu yao.
Baadhi
ya changamoto hizo ni wananchi kutokuwa na uelewa wa sheria, kanuni na
taratibu za kukopa fedha kwa watu binafsi na katika taasisi za fedha,
wananchi hawana uelewa wa sheria na taratibu za mirathi na hata
wasimamizi wa mirathi hawajui wajibu wao kwa warithi na kwa mahakama
jambo ambalo linapelekea warithi kuchelewa au kutopatiwa haki zao hata
baada ya mchakato wa mirathi kukamilika katika Mahakama.
“Katika
eneo la ajira huko ndio kunatisha kwa uvunjaji wa sheria za ajira na
nchi uliokithiri kwani makampuni mengi hasa ya ujenzi na ulinzi hayatoi
mikataba ya ajira kwa wafanyakazi, wakati mwingine mikataba inakuja
kutolewa baada ya mwajiriwa kuwa amekwisha fanya kazi muda mrefu na
inapotolewa inakuwa inakiuka makubaliano ya awali,” alisema na
kuwanyooshea kidole viongozi wa serikali za mitaa na kata, katika baadhi
ya maeneo kwa kuwa chanzo cha migogoro kwa kufanya majukumu ambayo si
yao kisheria na uendeshwaji wa kesi mahakamani kuchukua muda mrefu
pasipo na sababu za msingi huku Mabaraza ya kata nayo kuwa dhaifu katika
kutekeleza majukumu yake ya kimsingi katika kuwahudumia wananchi na
hasa wale wa kipato cha chini.
Akizungumzia
huduma hiyo, Makonda alisema aliamua kuanzisha huduma ya msaada wa
kisheria kupitia wanasheria hawa (35) katika kila wilaya ya mkoa wa Dar
es Salaam ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya chama tawala Chama
Cha Mapinduzi (CCM) inayoagiza kusikiliza na kutatua kero au malalamiko
ya wananchi.
Mkuu
huyo wa Mkoa alifafanua kuwa katika ziara ya mkoa wa Dar es Salaam
mwishoni mwa mwaka 2016 aligundua wananchi wengi hawakuwa na uelewa wa
sheria jambo lililowafanya kupoteza haki zao aidha kwa kutapeliwa,
kuonewa au kutojua mahala sahihi pa kupeleka matatizo hayo.
"Pamoja
na changamoto nyingi zinazoambatana na huduma hii ya kutafuta suluhu ya
matatizo ya wananchi kwa kuzileta pande husika mezani kuongea bado nina
dhamira ya kuendelea kuwasaidia Watanzania wenzangu kwa juhudi na
maarifa yangu yote.
Na hii
ndio gharama ya kuteuliwa na Rais, unapoteuliwa na Mkuu wa nchi anakuwa
na matarajio mengi kutoka kwako. Mimi nimeamua kufanya ninayoweza kwa
nguvu na juhudi zote ili kumuondolea Rais John Pombe Magufuli na
mashinikizo juu ya shida mbalimbali za Wana Dar es Salaam," alimaliza
Makonda.
No comments:
Post a Comment