TASISI YA KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA TANZANIA (THPS) YAANDAA MKUTANO WA SIKU MOJA WA WADAU WA MAPAMBANO YA VVU NA UKIMWI ZANZIBAR
Waziri
wa Afya Mahmoud Thabit Kombo akifungua mkutano wa wadau wa mapambano ya
ukimwi Zanzibar katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mbweni.
Waziri
wa Afya Mahmoud Thabit Kombo akizindua Mpango Mkakati wa miaka mitano
wa THPS katika mkutano wa wadau wa mapambano ya ukimwi uliofanyika
Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mbweni, anaeshirikiana nae katika
uzinduzi huo ni Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Redempta Mbatia.
Mkurugenzi
Mtendaji wa THPS Dkt. Redempta Mbatia akizungumza na wadau wa mapambano
ya ukimwi Zanzibar katika mkutano wa siku moja uliofanyika Hoteli ya
Zanzibar Beach Resort Mbweni.
Muhudumu
Mkuu wa huduma za mama na mtoto na huduma za upimaji vvu kwa jamii
kutoka Hospitali ya Mwembeladu Mwanakhamis Alawi Nguzo akipokea zawadi
maalum kutoka Waziri wa afya Mh. Thabit Kombo baada ya kuwa kituo bora
katika mapambano ya ukimwi kipindi cha miezi mitatu Octoba – Disemba.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya kuimarisha huduma za afya Tanzania (THPS) Dkt.
Redempta Mbatia akimkaribisha Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo
alipowasili kufungua mkutano wa wadau wa mapambano ya ukimwi Hoteli ya
Zanzibar Beach Resort Mbweni.
Na Ramadhani Ali-Maelezo
Taasisi
zinazojishughulisha na mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya
ukimwi (VVU) na ukimwi Zanzibar zimetakiwa kuelekeza nguvu katika
makundi maalum ambayo maambukizi bado ni makubwa.
Waziri
wa Afya Mahmoud Thabit Kombo alitoa ushauri hao alipokuwa akifungua
mkutano wa siku moja wa wadau wa mapambano ya ukimwi uliotayarishwa na
Taasisi ya kuimarisha huduma za afya Tanzania (THPS) na kuzindua mpango
mkakati wa miaka mitano wa taasisi hiyo katika Hoteli ya Zanzibar Beach
Resort Mbweni.
Alisema
wakati Zanzibar inajivunia kuwa na asilimia chini ya moja ya maambukizi
ya VVU, katika makundi maalumu maamukizi yapo kwa asilimia 10 hadi 19
ambapo ni hatari.
Aliyataja
makundi hayo kuwa ni vijana wanaojidunga sindano za madawa ya kulevya,
wanawake wanaofanya biashara ya ngono na wanaume wanaofanya ngono na
wanaume wenzao.
Alisema kunapokuwa na kikundi kidogo cha watu wenye hali kubwa ya maambukizi ya VVU hatari ya maambukizi inaelekea kwenye jamii.
“Makundi
maalum yanaonekana kuwa ni daraja la maambukizi ya Virusi vya Ukimwi
kutoka kwao kuja kwenye jamii, ”alisisitiza Waziri wa Afya.
Aliongeza
kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeridhia kuyafanyia kazi malengo
ya dunia ya kutokomeza kabisa maambukizi ya VVU ifikapo mwaka 2030 hivyo
mashirikiano zaidi yanahitajika katika kufikia malengo hayo.
Hata
hivyo alieleza kuwa ushiriki wa wananchi katika kupima VVU bado
hauridhishi na wale wanaopima na kubainika na maambukizi wengi wao
hawajiungi kwenye huduma za tiba na wachache wanaotumia dawa hawazitumii
ipasavyo.
Waziri
wa Afya alikumbusha kuwa wakati huu ambapo Zanzaibar inatekeleza Mpango
wa kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa
ujauzito lakini wanaume hawajitokezi kupima afya zao.
“Akinababa
tuwasindikize wake zetu kliniki ili na sisi tupimwe Virusi vya ukimwi,
hivi sasa tupo chini ya asilimia tano wakati wenzetu Tanzania Bara
wamefikia asilia 80, “Waziri Mahmoud alihimiza.
Mkurugenzi
Mtendaji wa THPS Dkt. Redempta Mbatia alisema katika kupambana na
ukimwi Zanzibar, taasisi hiyo imekuwa ikiwajengea uwezo wafanyakazi wa
afya na taasisi nyengine zinazoshiriki katika mapambano hayo.
Aidha
alisema wamekuwa wakisaidia masuala ya uongozi pamoja kuimarisha utawala
bora na kusaidia vifaa tiba katika Hospitali na vituo vya afya ili
kuhakikisha huduma za afya zinakuwa endelevu na kufikia malengo
yaliyowekwa.
No comments:
Post a Comment