ENG. NGONYANI ARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI UYOVU- BWANGA.
Mhandisi Mkazi Eng. Juma Msonge,
akitoa taarifa ya maendeleo yaliyofikiwa ya ujenzi wa barabara ya
Uyovu-Bwanga KM 45 inayojengwa kwa kiwango cha lami jana, mkoani Geita
kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, akitoa maelekezo kwa Mhadisi Mkazi
Eng. Juma Msonge, baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Uyovu-Bwanga KM
45 inayojengwa kwa kiwango cha lami jana, mkoani Geita.
Sehemu ya barabara ya Uyovu-Bwanga
KM 45 inayojengwa kwa kiwango cha lami na Mkandarasi Synohdro, mkoani
Geita. Hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 60.
Meneja wa Wakala wa Barabara
nchini (TANROADS), mkoa wa Geita, Eng. Harun Senkuku, akifafanua jambo
kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani,
ambae alikuwa mkoani humo kwa ajili ya kukagua miradi inayotekelezwa na
Wizara yake.
…………….
Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani ameridhishwa na kasi ya
ujenzi wa barabara ya Uyovu-Bwanga yenye urefu wa Km 45 inayojengwa na
Mkandarasi M/S Sinohydro Corporation.
Akizungumza mkoani Geita jana,
mara baada ya kukagua barabara hiyo ikiwa ni sehemu ya mradi wa ujenzi
wa barabara ya Uyovu-Bwanga-Biharamulo KM 112, Naibu Waziri Eng.
Ngonyani amemtaka mkandarasi huyo kahakikisha wanamaliza sehemu
iliyobakia kwa muda uliopangwa.
“Nimeridhishwa na kasi yenu,
hakika mmepiga hatua sana kwani awali nilipopita kukagua barabara hii
haikuwa hivi”, amesema Naibu Waziri Ngonyani.
Aidha, Eng. Ngonyani,
amewapongeza wasimamizi wa barabara ya Biharamulo – Bwanga kutoka wakala
wa barabara nchini (TANROADS) kupitia kitengo chake maalum cha
wahandisi washauri wazawa (TECU), kwa kuhakikisha wanamsimamia
mkandarasi M/S Sinohydro Corporation kujenga barabara hiyo kwa viwango
vilivyomo kwenye mkataba.
Kwa upande wake, Mhandisi mkazi wa barabara hiyo Eng. Juma Msonge, amemhakikishia Waziri huyo kumaliza barabara hiyo kwa wakati.
Eng. Msonge ameongeza kuwa kwa
sasa mradi huo umefika asilimia 60 ambapo mkandarasi anaendelea na kazi
ya kuweka matabaka ya lami ambapo ameshaweka km 30 kati ya 45 zilizopo
kwenye barabara hiyo.
Naibu waziri Ngonyani, amemaliza
ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Geita ambapo pamoja na mambo mengine
ametembelea na kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara yake.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment