Sabodo: Ukaribu wangu na Mwl. Nyerere uliokoa Taifa
Mfanyabiashara maarufu, Mustafa Jaffar Sabodo
Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere
Aliyekuwa Kiongozi wa Taifa la Iran, Ayatolah Khomein
HAKIKA ukitaja jina la Mustafa Jaffer
Sabodo, siyo geni masikioni mwa Watazania wengi.
Hii ni kutokana na mchango wake kwa
jamii katika kuliondoa taifa kutoka sehemu moja ya chini kwenda juu, yaani
maendeleo.
Sabodo mfanyabiashara maarufu ambaye ni
Mtanzania mwenye asili ya Asia amekuwa akitoa mchango kwa maendeleo ya Taifa
katika nyanja mbalimbali kuanzia za uchumi, siasa, elimu, afya na maji.
Mfanyabiashara huyo ambaye ni mzaliwa wa
mkoani Lindi takriban miaka 73 iliyopita amejitolea kujenga shule mbalimbali
nchini, hospitali, visima vya maji hata kufadhili shughuli za kisiasa na
kiuchumi.
Michango yake hiyo kwa jamii ya
Watanzania, imefanya jina lake kuandikwa katika mioyo ya wananchi wengi kwani
alidhirisha tabia yake isiyojificha ya uzalendo kwa Taifa lake Tanzania.
Sabodo anatajwa kuwahi kuvifadhili vyama
vya siasa vya CCM na Chadema kwa nyakati tofauti.
Pia anatajwa kwamba alikuwa rafiki wa
karibu wa Mwalimu Julius Nyerere na wanasiasa mbalimbali nchini hata kuwahi
kutumwa kwenda nchini Iran kukutana na kuomba mafuta kwa aliyekuwa kiongozi wa
taifa hilo la Kiislamu, Ayatolah Khomein katika miaka ya 1970 baada ya taifa
kukumbwa na uhaba wa mafuta uliochagizwa na sababu mbalimbali ikiwamo ukosefu
wa fedha za kigeni.
Hali hiyo ilitokea kipindi hicho wakati dunia
ilikuwa bado ikishuhudia mgawanyiko kwa baadhi ya nchi kuegemea Marekani
kisiasa na kimfumo, nyingine zikifuata mfumo wa iliyokuwa Muungano wa nchi za
Kisovieti za Urusi (USSR).
Si hivyo tu kwa kusoma alama za nyakati,
baadhi ya nchi zilikaa kando na utengano huo na kuanzisha Jumuia ya Nchi
Zisizofungamana na Upande Wowote.
Miungoni mwa mataifa yaliyofuata siasa
za kutofungamana na upande wowote, Tanzania wakati huo chini ya uongozi wa Baba
wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ilikuwa mojawapo.
Tofauti hizo za kisiasa hata kidini kati
ya mataifa zilisababisha athari zilizozaa tofauti ya hali hasa kiuchumi na
kisiasa hata baadhi ya nchi kuingia kwenye mahangaiko ikiwamo Tanzania
iliyokumbwa na uhaba wa mafuta ya Petroli na fedha za kigeni.
Sabodo anasimulia kwamba kufuatia hali
hiyo iliyoilazimu Serikali kuzuia magari yake kutembea Jumapili huku Jumamosi
yakitembea hadi saa nane mchana, alipata nafasi ya kukutana na Rais Nyerere.
Anasimulia kwamba katika mazungumzo hayo
alimwabia Rais Nyerere haja yake ya kutaka kwenda Iran kuomba mafuta.
“Nikamwambia wacha niende Iran.
Nilifanya hivyo nikiamini Khomein atanisikiliza. Nakumbuka nilikwenda na Chifu
Adam Sapi Mkwawa,” anasema.
Anasimulia: “Mimi ni Khoja, Mwislamu wa
dhehebu la Shia na Khomein pia, nilipokutana naye, nikamwambia wanaoteseka
Tanzania kwa shida ya mafuta wamo piaWaislamu wa Shia wengi tu.”
“Nilimwambia Tanzania ni nchi nzuri
haina ubaguzi na Rais Nyerere ni mtu mwema, hata Waziri Mkuu wake ni Rashid
Kawawa na Waziri wa Madini na Mafuta ni Anoor Kassam, nikamwangukia miguuni
nikiliaa kuomba aipe nchi yetu mafuta, akakubali” anakumbuka Sabodo.
Hata hivyo, anasema licha ya kukubali,
Khomein akasema hawezi kumpa mafuta yeye
Sabodo hadi watu wa Serikali ya Tanzania watakapofika Iran kuthibitisha ombi
hilo.
“Nikarudi Tanzania na kumpa taarifa baba
wa Taifa naye alimwambia Kawawa na John Malicela ikakubalika tukaenda tena Iran
safari hii nikiwa na mawaziri wa Fedha, Cleopa Msuya, Anoor Kassam wa Mafuta na
Usafirishaji pia alikuwepo Peter Noni kwa niaba ya Benki Kuu na Adam Sapi
Mkwawa,” anasema.
Sabodo anakumbuka kuwa safari hiyo
ilizaa matunda kwani Khomein aliipa Tanzania mafuta yenye thamani ya Dola za
Kimarekani 80,000.
“Nakumbuka hapo urafiki wangu na Nyerere
uliniwezesha kuliokoa Taifa kwa kupata mafuta baada ya kunituma kwenda Iran
nilipomshauri,” anasema Sabodo ambaye wazazi wake alizaliwa Lindi.
Anakumbuka kuwa pia katika safari hiyo
alimshauri Khomein kufungua ofisi ya Ubalozi wa Iran nchini naye alikubali na
alifanya hiyo pia kwa Zambia, Tanzania nayo ikafungua ubalozi Iran.
Don’t
forget to read my book; CORRUPTION IS CRUCIFICATION OF
TANZANIA, which is in process
No comments:
Post a Comment