WAZIRI MKUU AENDESHA HARAMBEE UJENZI WA SEKONDARI MPYA RUANGWA
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amelazimika kuendesha harambee ya papo kwa papo ma kuchangisha
sh.milioni 138.26 ili kufanikisha ujenzi wa shule mpya ya sekondari wilayani
Ruangwa.
Hatua hiyo hiyo
inafuatia wingi wa wanafunzi waliofaulu mtihani wa darasa la saba na
kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza lakini hawakufanikiwa kupata nafasi
katika mkupuo wa kwanza.
“Katika kikao cha
Halmashauri ya Wilaya cha hivi karibuni ilionekana kuna haja ya kujenga shule
mpya ya sekondari ili kukabiliana na wingi wa watoto waliofaulu mtihani wa
darasa la saba na kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza. Tunawashukuru sana
wenzetu ambao wametoa maeneo yao bure ili shule ijengwe haraka,” amesema.
Katika harambee iliyofanyika
kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Ruangwa leo mchana (Ijumaa, Desemba
30, 2016), Waziri Mkuu amefanikisha kupatikana kwa fedha kiasi cha sh. milioni 120.65
na mifuko 550 ya saruji na mabati 360 (vyenye
thamani ya sh. milioni 17.61) ambavyo vitatumika kujenga madarasa manne ya
kidato cha kwanza yanayotakiwa kuwa yamekamilika ifikapo Januari 15, 2017.
Kwa mujibu wa
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Bw. Andrea Chezue, jumla ya
watoto 319 walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza lakini walikosa nafasi
sababu ya ukosefu wa madarasa na walitakiwa kusubiri hadi chaguo la pili ambalo
kwa kawaida hufanyika Februari, kila mwaka.
“Wanafunzi
waliofaulu na kukosa nafasi jumla yao ni 319 lakini kwa hapa Ruangwa mjini ni
179 na waliobakia 140 wanatoka kwenye kata za jirani za Nachingwea na Mandarawe.
Shule hii ya sekondari itahudumia kata tatu. Kwa hiyo Halmashauri imepanga
kujenga madarasa manne hapa mjini ili watoto wote waweze kuanza mara moja,”
amesema.
Mkurugenzi huyo amesema
ili kupunguza tatizo hilo mwakani, wataendeleza ujenzi wa madarasa manne manne
waweze kuwa na mikondo minne kwa kila kidato. “Halmashauri ya Ruangwa imetenga
sh. milioni 75, wananchi wa Kata ya Ruangwa wametoa sh. milioni 1.2 na wananchi
wa kata ya Nachingwea wametoa sh. milioni 2.25,” amesema.
Waziri Mkuu ambaye
ni mbunge wa jimbo hilo, amechangia sh. milioni 33 kutoka kwenye mfuko wa jimbo
ili kuharakisha ujenzi wa madarasa mawili ya kuanzia. Wengine waliochangia
harambee hiyo ni kampuni ya Paco Gems Ltd, (sh. milioni 6), Baraka Solar (sh. milioni
moja), Ofisi ya Mkuu wa Mkoa (sh. milioni 1), Kampuni ya Asamalema (sh. milioni
1) na mfanyabiashara wa Ruangwa, Bw. Abdallah Namkudai (sh. 200,000).
Wengine ni kampuni
ya wanyumbani construction mifuko 100 ya saruji, kampuni ya Lindi Jumbo (mabati
100 na mifuko 100 ya saruji), kampuni ya madini ya Nazareth (mifuko 150 ya
saruji), kampuni ya URANEX inayochimba madini ya Graphite (mabati 260), mgodi
wa dhahabu wa Namungo (mifuko 100 ya saruji) na Kampuni ya ujenzi ya Nahungo Construction
Ltd. (mifuko 100 ya saruji).
Waziri Mkuu
amewashukuru wote waliojitolea kuchangia ujenzi wa shule hiyo. Amerejea jijini
Dar es Salaam jioni hii.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
IJUMAA, DESEMBA 30, 2016.
No comments:
Post a Comment