TANZANIA NA UAE ZAKUTANA KWA KIKAO CHA KWANZA CHA TUME YA USHIRIKIANO
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Balozi
Augustine Mahiga (kushoto) kwa pamoja na Mhe. Reem Ebrahim Al Hashimy,
Waziri wa Nchi anayeshughulikia Ushirikiano wa Kimataifa wa Umoja wa
Falme za Kiarabu (UAE) wakisaini Mkataba wa Ushirikiano katika Sekta ya
Anga. Mkataba huo ulisainiwa wakati wa kikao cha kwanza cha Tume ya
Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kilichofanyika Abu Dhabi, Falme za
Kiarabu tarehe 19 na 20, Desemba, 2016.
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Masharika, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi (kushoto) pamoja na Mkurugenzi
wa Uchumi na Biashara wa Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE wakiwekeana
saini baadhi ya makubaliano yaliyoafikiwa.
Mhe.
Dkt. Mahiga na ujumbe alioongozana nao wakiwa katika kikao cha kwanza
cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano na ujumbe wa UAE
kilichofanyika Abu Dhabi tarehe 19 na 20, Desemba, 2016.
Mratibu
wa Mkutano kwa upande wa Serikali ya Tanzania kutoka Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Hangi Mgaka akifuatilia
mkutano.
Picha
ya pamoja ya ujumbe wa Tanzania na UAE mara baada ya kukamilisha kikao
cha kwanza cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kilichofanyika
Abu Dhabi tarehe 19 na 20, Desemba, 2016.
TANZANIA NA UMOJA WA FALME ZA KIARABU ZAFANYA MKUTANO WA KWANZA TUME YA PAMOJA YA KUDUMU YA USHIRIKIANO HUKO ABU DHABI.
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Umoja wa Falme za
Kiarabu (UAE) zimefanya kikao cha kwanza cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya
Ushirikiano huko Abu Dhabi makao makuu ya Umoja wa Falme za Kiarabu.
Kikao hicho kilifanyika tarehe 19 na 20, Desemba, 2016.
Mkutano
huo ulioshirikisha sekta mbalimbali za Serikali zote mbili uliongozwa
na Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (MP), Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania na Mhe. Reem Ebrahim Al
Hashimy, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Ushirikiano wa Kimataifa wa
Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Pamoja
na mambo mengine, katika mkutano huo Tanzania na UAE zimekubaliana
kushirikiana kwenye masuala ya Kidiplomasia; Uchumi; Utalii; Nishati;
Kilimo; Sayansi na Teknolojia; Usafirishaji; Miundombinu; Ulinzi na
Usalama; Elimu pamoja na Kazi na Ajira.
Sambamba
na mkutano huo, Tanzania na UAE zimesaini Mkataba wa Ushirikiano katika
Sekta ya Anga (Bilateral Air Service Agreement-BASA) na Mkataba wa
Ushirikiano katika Sekta ya Utalii. Vilevile Serikali zote mbili
zimekubaliana kukamilisha na kusaini Mkataba wa Kutotoza Kodi Mara Mbili
na Kuzuia Ukwepaji wa Kodi za Mapato; Mkataba wa Kuhamasisha na Kulinda
Uwekezaji; pamoja na ushirikiano katika sekta ya Elimu, Afya, Ulinzi na
Usalama, Ushirikiano katika Usafiri wa Majini, Kazi na Ajira pamoja
ushirikiano katika masuala ya Zimamoto na Uokoaji.
Mkutano
huo umekuwa ni chachu katika mahusiano ya kihistoria ya nchi hizi mbili
ambapo umeweka mazingira rasmi ya ushirikiano sio tu kwa Serikali bali
pia kwa sekta binafsi. Mheshimiwa Waziri Mahiga katika hotuba yake ya
ufungaji alitoa wito kwa Jumuiya za Wafanyabiashara na sekta binafsi kwa
ujumla za Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu kuchangamkia fursa
zinazopatikana katika nchi hizi mbili kuafuatia mkutano huo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 21 Desemba, 2016.
No comments:
Post a Comment