Header Ads

SHIRIKA LA TAIFA LA BIASHARA ZANZIBAR LATILIANA SAINI MAKUBALIANO YA KILIMO HAI CHA KARAFUU NA KAMPUNI YA GANEFRYD YA DENMARK

Na Ramadhani Ali/Maelezo.

Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) litapatiwa hati ya kuuza karafuu hai kwenye soko la Ulaya baada ya kutiliana saini na Kampuni ya Ganefryd ya Denmark makubaliano ya kuimarisha kilimo hai cha mazao tofauti (organic) kwa kuanzia na kilimo cha karafuu.

Sherehe za kutiliana saini makubaliano hayo zilifanyika katika ofisi za eneo tengefu Saateni na ZSTC iliwakilishwa na Mkurugenzi Mwendeshaji Dkt. Said Seif na Kampuni ya Genefryd iliwakilishwa na Afisa wake Bw. Pale Christeusen.

Akizungumza baada ya kutia saini makubaliano hayo, Dkt. Said amesema Zanzibar imekuwa ikifanya biashara ya karafuu kwa miaka mingi lakini hivi sasa itapanua wigo wa kuuza karafuu hai Ulaya na kupata faida kubwa.

Alisema ili Zanzibar iweze kutoa karafuu hai tahadhari kubwa inapaswa kuchukuliwa wakati wa kuotesha miche, ukuaji wake na kufikia wakati wa kuzaa bila ya kuingizwa aina yoyote ya mbolea zenye kemikali. 

Ameongeza kuwa uangalizi mkubwa pia unahitaji katika mchakato mzima wa kushughulika kilimo hicho kuanzia hatua ya kuchuma, kuanika, kuzihifadhi mpaka kuzisafirisha hivyo amewaomba wananchi kuunga mkono kuingia katika kilimo hai kwa vile karafuu ndio tegemeo lao na Taifa kwa jumla. 

Amesema sambamba na kuanzisha kilimo hai cha zao la karafuu Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSTC amewataka wananchi kuendeleza zao hilo katika mfumo wa kawaida kwa kuongeza upandaji miche na kuacha tabia ya kukata mikarafuu kwa ajili ya kuni, kufanyia mkaa na kujengea.

Afisa wa Kampuni ya Genefryd Bw. Pale Christeusen amesema hatua ya kutiliana saini makubaliano hayo ni kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili na kuongeza kipato cha mkulima wa karafuu na kuiongezea Serikali mapato.

Bw. Christeusen amewashauri wakulima wa karafuu Zanzibar kuongeza kilimo hai cha karafuu kwa vile kinafaida kubwa katika soko la Ulaya.
 Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar (ZSTC) Dkt. Said Seif akitiliana saini na mwakilishi wa Kampuni  Denmark Bw. katika ofisi za Shirika hilo ziliopo Saateni Mjini Zanzibar.

 Wafanyakazi wa  ZSTC wakisafisha karafuu hai kabla ya kuhifadhiwa kwenye mifuko maalum kwa ajili ya kuuzwa kwa wateja. 
 Afisa Masoko wa ZSTC Nassor Salum Nassor akitoa maelezo kwa waandishi wa habari kuhusu utaratibu unaotumika wa kupokea na kuzihifadhi karafuu hai kabla ya kuingizwa sokoni.
Picha na Makame Mshenga.

No comments:

Powered by Blogger.