TUMIENI NYUMBA ZA IBADA KUHAMASHISHA AMANI-WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitoa hutuba katika swala ya Idd El Haji iliyofanyika Viwanja vya Mwembe Yanga Dar es Salaam leo asubuhi.
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewaomba viongozi wa dini zote kutumia
nyumba za ibada kuwahamasisha waumini wao
umuhimu wa kulinda na kudumisha amani na utulivu uliopo nchini.Amesema
Serikali itahakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumishwa
nchini ili Watanzania
wawe na uhakika wa kuendelea kufanya kazi zao za kuwaingizia kipato na
kuwaletea tija.
Waziri
Mkuu ametoa wito huo leo (Jumatatu, Septemba 12, 2016) wakati akizungumza na waumini
wa dini ya kiislam mara baada ya kumaliza kuswali sala ya Eid El Haji kwenye viwanja
vya Mwembe Yanga, Temeke Dar es Salaam.
“Serikali
itaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo yote nchini. Wito wangu kwa viongozi
wa dini msisitize waumini juu ya utunzaji wa amani pamoja na kukemea vitendo viovu
ili Taifa lizidi kusonga mbele,” amesema.
Wakati huo huo Waziri Mkuu
amewasisitiza wananchi kuendelea kuwaombea mahujaji waliopo mjini Makka na
Madina nchini Saudi Arabia wakiendelea na ibada ya hijja warudi salama.Pia
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kuwasaidia kwa hali na mali
watu waliokumbwa na tetemeko la ardhi mkoani Kagera ambako jumla ya watu 16
walifariki na wengine 253 kujeruhiwa.
Pia
maelfu ya wananchi kukosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1264
zikipata nyufa yakiwemo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma.Awali
akisoma hutuba ya Eid viwanjani hapo Sheikh Nurdin Kishki alisema dini ya
Uislamu ni dini ya amani hivyo amewaomba waislamu kujiepusha na vitendo vya
uvunjifu wa amani yakiwemo mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.
Sheikh
Kishki amesema ni muhimu watu kulinda amani kwani ikitoweka ni vigumu kuirudisha,
alitolea mfano wanachi wa nchi za Libya
na Misri ambazo hadi sasa zimeshindwa kuirudisha.Amesema
mtu yeyote anayejihusisha na vitendo vya uwamwagaji wa damu, kudhulumu mali za
watu pamoja na kuwavunjia heshima wenzake atakuwa ameangamia, hivyo amewataka
Watanzania hususan wakazi wa Temeke kujiepusha navyo.
“Temeke
sasa inaongoza kwa matukio ya mauaji, wanaua hadi walinzi. Askari wameuawa bila
hatia, jambo hili linasikitisha sana. Watu waliokuwa wanafanya kazi ya kulinda
raia na mali zao wanauawa bila ya hatia! Ameongea kwa masikitiko na kuwaomba
Watanzania wajiepuszhe na vitendo hivyo.
Katika
hatua nyingine Sheikh Kishki ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuonyesha
dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo hivyo amewaomba
wananchi wawe mstari wa mbele kutoa ushirikiano ili taifa liweze kusomba mbele.
“Ndugu zangu tumepewa
heshima kubwa leo kuswali Eid na Mheshimiwa Waziri Mkuu tena amekuja hapa
kwenye viwanja hivi vya Mwembe Yanga, hii inaonyesha ukaribu wa viongozi wetu
wakuu kwa wananchi wao hususan wa hali ya chini,” amesema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
JUMATATU SEPTEMBA 12, 2016
No comments:
Post a Comment