NAIBU WAZIRI WA AFYA DR HAMIS KIGWANGALLA : 'SIKUSOMA HIGH SCHOOL NA NDG. JUMA MWAKA.
Naibu Waziri wa Afya na Mbunge wa Nzega Vijijini Dr Hamis Kigwangalla
-----
Kuna baadhi ya magazeti na mitandao imekuwa ikiandika kuwa Dkt.
Kigwangalla amesoma high school na aliyekuwa 'Tabibu', Ndg. Juma Mwaka,
shule ya Kigoma Sekondari na kwamba walikuwa marafiki; hizi ni habari za
uongo, za kupika zenye kupotosha ukweli ili kuwaaminisha watu kuwa
'wanajuana' na pengine wana ugomvi 'binafsi'.
Nimekuwa nikimpuuza kwa sababu sikuwa na haitotokea nikawa na nia mbaya
dhidi ya mtanzania mwenzangu yeyote kwa sababu tu mimi nina dhamana ya
uongozi. Sinaga tabia hiyo.
Uongo ukirudiwa rudiwa hubadilika na kuwa ukweli. Leo nimeamua, hapa
chini, kukanusha ili watanzania pia mumpuuze, tuendelee kuimarisha
huduma za tiba asili na tiba mbadala kutoka kwa matabibu wa kweli
wanaofuata taratibu na siyo wasanii kama huyu. Uongo ama uzushi dhidi
yangu mimi binafsi kamwe hautonirudisha nyuma mimi kama mtumishi wa
umma. Lazima ifike mahali tujenge nchi ya watu 'serious' wanaofuata
Sheria, Kanuni na Taratibu. Wanaoheshimu Serikali. Kwenye Afya za
watanzania hatuwezi kuvumilia usanii, lazima tuwalinde walaji. Hili ni
jukumu tulilopewa na Mhe. Rais. Tutasimamia Sheria ipasavyo.
Hatutolegeza hata kidogo.
1. Sikusoma 'high school' Kigoma Sekondari. Nimesoma O'level (form I -
IV) Kigoma Sekondari. High School nilisoma Shinyanga Sekondari.
Sikumbuki kusoma katika shule zote hizi mbili na mtu mwenye Jina Hilo.
Kama alisoma Kigoma Sekondari labda mbele yangu ama nyuma yangu. Pia
kipindi nasoma Kigoma Sekondari, hakukuwa na 'high school'.
2. Ndg. Juma Mwaka hajawahi kuwa rafiki wala adui yangu. Sina ugomvi
binafsi. Nafanya kazi ya kusimamia Sheria ya tiba asili na tiba mbadala
ipasavyo.
3. Naithamini tiba asili na tiba mbadala na Ndiyo maana nimeongoza
Wizara ya Afya kufanya Mapinduzi makubwa kwenye eneo hili, ikiwemo
kuweka utaratibu mzuri na rahisi zaidi wa kusajili watoa huduma, dawa
zao, mazingira wanapotunzia dawa, wasaidizi wao, viwanda vyao, na pia
kuweka mikakati ya uanzishwaji wa viwanda vya dawa za tiba asili na tiba
mbadala sambamba na kufanyia utafiti dawa zao na kudhibiti ubora wa
dawa zenyewe na dozi wanazowapa wateja.
4. Muulizeni Ndg. Juma Mwaka anaposema ana ugomvi 'binafsi' na mimi,
anamaanisha nini, ugomvi upi? Juu ya nini? Awape taarifa kamili. Mimi
Sina ugomvi naye. Kwanza sikuwahi kumjua kabla ya ziara yangu ya kikazi
pale Foreplan, ntakuwaje na ugomvi na mtu nisiyemjua? Si utakuwa ujuha
huo?
5. Mnaofuatilia suala hili mtakeni Ndg. Juma Mwaka awape majibu ya
Msingi ya hoja za wakaguzi kutoka Wizara ya Afya. Mimi nilikuwa
msimamizi nikiwapa nguvu wataalam wafanye kazi yao. Wataalamu
walikuwepo, nao ana ugomvi nao 'binafsi'? Mwambieni awajibu kama dawa za
tiba ya kisasa kukutwa kwenye eneo lake la kazi ilikuwa halali? Alikuwa
na vibali vya kutunza zaidi ya maboksi 200 ya dawa? Alikuwa na vibali
vya kutunza zaidi ya magunia 10 ya dawa za tiba asili na tiba mbadala
baada ya kufutiwa usajili? Alikuwa na uhalali wa kuendelea kutangaza
kwenye vyombo vya habari kuwa wateja wake wafuate dawa pale ili
wasikatishe dozi? Tena kinyume na katazo la Baraza la tiba asili na tiba
mbadala! Yeye yuko juu ya Serikali? Yuko juu ya Sheria? Ama anadhani
anaweza kuidhihaki na kuiogofya Serikali?
6. Baada ya ziara yangu ya December 2015, ambapo sikutoa maelekezo ya
kumfungia wala kumfutia kibali, niliwaelekeza Baraza la Tiba Asili na
Tiba mbadala kuwa wawaite wawaelekeze matabibu wote wafuate Sheria,
kanuni na taratibu. Waliitwa. Wakaelekezwa. Waungwana wakatii. Yeye
hakutii, wakamfuta. Baada ya kufutiwa usajili, akaendelea kujitangaza na
kutoa huduma, yeye ni nani?
7. Kufanya haya ni kuvunja sheria za nchi. Na makosa haya yana adhabu
zake. Sisi kama Serikali tumeagiza hatua za kisheria zichukuliwe dhidi
yake. Serikali ina mkono mrefu, itamkamata. Itamtia nguvuni na
atafikishwa mahakamani. Ataenda kujitetea huko kuwa ana 'ugomvi binafsi'
na Naibu Waziri Kigwangalla!
Mwisho, aende akafuatilie kisa cha mfanyabiashara wa kigiriki aliyesema
ameiweka Serikali mfukoni - Mwalimu Nyerere alimfanya nini!
Dkt. Hamisi Kigwangalla, MB.
No comments:
Post a Comment