Barabara ya Nanganga-Ruangwa kuwekwa lami
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na mwendesha pikipiki maarufu na
hodari, Zaina Amour wa kijiji cha Nandagara wilayani Ruangwa Aprili 10,
2016.
WAZIRI
Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa
amesema serikali inatarajia kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya
kutoka Nanganga, Ruangwa hadi Nachingwea.
Hatua
hiyo itawezesha kutatuliwa kwa kero ya changamoto ya miundombinu ya
barabara inayowakabili wananchi wa wilaya za Ruangwa na Nachingwea kwa
muda mrefu.Waziri Mkuu, Majaliwa amesema barabara hiyo ambayo kwa sasa
haipo katika hali nzuri itajengwa kwa kiwango cha lami, ambapo serikali
inatarajia kuanza kuifanyia upembuzi yakinifu katika mwaka wa fedha wa
2016/2017.
Hayo
yamesemwa jana jioni (10 Aprili, 2016) na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
alipozungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Likunja,
Nkowe na Namahema katika mikutano ya hadhara aliyoifanya wilayani
Ruangwa wakati akiwa kwenye ziara yake ya kikazi.
Amesema
serikali imejipanga katika kuboresha miundombinu ya barabara kwenye
maeneo mbalimbali nchini na kwamba mara baada ya kumalizika kwa upembuzi
yakinifu ujenzi wa barabara hiyo utaanza, hivyo amewataka wananchi kuwa
na subira.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu, Majaliwa amewataka wananchi wa vijiji hivyo
kushirikiana katika shughuli za maendeleo na kuweka kando itikadi zao
za kisiasa kwa sababu uchaguzi ulishamalizika tangu Oktoba 25 mwaka
jana.
“Mimi
nitaendelea kuwaheshimu, kuwasikiliza na kuwahudumia, nawaomba
tushirikiane na tuweke kando masuala ya itikadi za vyama, sasa ni wakati
wa kazi, hivyo ni bora tukashirikiana kufanya kazi kwa maendeleo ya
Ruangwa jambo ambalo linawezekana.
Hata kama
wewe ambaye najua ulinichukia mimi nimekusamehe kutoka moyoni, wewe ni
wangu hata kama hukunichagua nitakuhudumia na kukutumikia kwa sababu
mimi ndiye mbunge wako hivyo naomba tushirikiane,” amesema.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Rashid
Nakumbya aliomba wakazi wa wilaya hiyo kushirikiana kwa pamoja kwa ajili
ya kuboresha maendeleo ya wilaya yao na hatimaye iweze kupiga hatua.
No comments:
Post a Comment