Header Ads

Naibu Waziri Annastazia atoa maagizo Kiwanja cha TBC kilichopo Kimani Wilaya ya Kisarawe kupatiwa Hati

Na Shamimu Nyaki, WHUSM.

Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Annastazia Wambura amemuagiza Meneja wa Miradi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC ) Bw. Mackselin Chota kuhakikisha kiwanja Na.1 Kitalu “B” kilichopo eneo la Kimani wilaya ya Kisarawe kinapatiwa Hati Miliki ili kuepusha kuvamiwa pamoja na migogoro inayoweza kutokea.

Agizo hilo amelitoa jumamosi wakati alipotembelea kiwanja hicho na kueleza kuwa kiwanja hicho ni lazima kiendelezwe kwa ajili ya kuwasaidia wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ambapo kiwanja hicho kilitafutwa kwa dhumuni hilo.“Naishukuru Halmashauri kwa kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizo,hivyo natoa siku saba kwa idara ya Miradi ya TBC kushirikiana na Halmashauri kuhakikisha kiwanja hicho kinapatiwa Hati”.Alisema Mhe.Annastazia.

Aidha amewataka kuwasilisha gharama zilizotumika katika ujenzi wa nyumba zilizopo katika eneo hilo na wapi zimetoka na sababu zilizosababisha ujenzi huo kukwama kwa zaidi ya miaka mitatu.

Akitoa maelezo kuhusu Kiwanja hicho Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Bi Mwanamvua Mrindoko amesema kuwa kiwanja hicho kilipimwa na ramani yake ya upimaji ilipata kibali cha Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kusajiliwa kwa namba 68480,ramani namba E 292/83 ya tarehe 22 februari, 2012.

“Taratibu za umilikishwaji zilifanyika kwa kuandaliwa gharama za kulipia kabla hati haijaandaliwa,malipo hayo yalifanywa na TBC kupitia NMB na kuwasilisha fomu ya malipo hayo(Bank pay in slip)”.Alisema Bi Mwanamvua.

Naye Meneja wa Miradi wa Shirika la Utangazaji Tanzania Bw.Mackselin Chota amesema kuwa Shirika hilo lina jumla ya viwanja 55 nchi nzima,ambavyo 19 kati ya hivyo vina Hati miliki ambapo katika mkoa wa Pwani kuna kiwanja kimoja, Dar es Salaam viwanja vitano ambavyo viko Pugu Road,Kunduchi, na TAZARA, Mikocheni na Sinza.a

No comments:

Powered by Blogger.