WAZIRI MKUU AWASIMAMISHA KAZI MAAFISA WAWILI CHATO
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi watumishi
wawili wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato kwa tuhuma za ubadhirifu,
rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.
Watumishi hao ni Mkuu wa Idara ya Kilimo na Ushirika, Bw.
Mwita Mirumbe Waryuba pamoja na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya, Bw.
Dioniz Mutayoba. Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana usiku (Jumatano, Machi
16, 2016) alipokuwa akizungumza na watumishi wa idara zote na taasisi
zilizomo kwenye wilaya ya Chato katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi
wa Mshikamano SACCOS wilayani humo.
Afisa Kilimo na Ushirika anadaiwa kuchangisha kiasi cha sh.
milioni 20 kutoka kwa watumishi wa Halmashauri hiyo kwa ajili ya
kuanzisha SACCOS tangu mwaka 2013 lakini hadi sasa SACCOS haijaanzishwa
na wala fedha hizo hazijarejeshwa. Fedha hizo zinadaiwa kuliwa na
watumishi watatu (majina yamehifadhiwa). Aidha, Bw. Waryuba anadaiwa kutumia lugha chafu na za
vitisho kwa watumishi walio chini yake ikiwa ni pamoja na kuomba na
kupokea rushwa, na kunyanyasa na kudhalilisha kijinsia baadhi ya
watumishi wa kike.
Inadaiwa pia Bw. Waryuba alikopa bila kufuata taratibu za
mikopo wilayani Chato ambapo alikopa sh. milioni 15 kutoka Mwambao
SACCOS na sh. milioni 15 nyingine kutoka Chato Teachers’ SACCOS tangu
mwaka 2015 na tangu wakati huo hajazirejesha hali ambayo imeleta
manung’uniko kutoka kwa viongozi na wananchama wa SACCOS husika.
“Malalamiko ya watumishi na wananchi dhidi ya huyu bwana
yamefikishwa kwa Kaimu Mkurugenzi lakini hajachukua hatua kwa sababu ni
rafiki yake,” alisema Waziri Mkuu. Kaimu Mkurugenzi huyo ni Mhandisi
Joel Baha ambaye hakuwepo ukumbini hapo kwa sababu yuko kwenye ziara ya
mafunzo huko Japan. Kwa upande wake, Bw. Mutayoba ambaye ni Afisa
Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo anadaiwa kuzembea kusimamia mradi wa
kufyatua matofali ya gharama nafuu (interlocking bricks) zilizogawiwa
kwa vikundi vinne vya vijana wa wilaya hiyo.
“Mwaka 2013 Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lilitoa
mashine nne za kufyatulia matofali ya bei nafuu kwa ajili ya vikundi
vinne vya vijana wilayani Chato. Mashine hizo ziligawiwa kupitia kwa
Afisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya, Bw. Dioniz Mutayoba na kila kikundi
kilipewa sh. 500,000 ili waanze kazi ya kufyatua matofali na kuyauza kwa
bei nafuu katika maeneo waliyopo lakini hadi leo hakuna kitu
kilichofanyika,” inasema sehemu ya taarifa.
Afisa huyo anadaiwa kugawa mashine mbili kwa kila kata
katika kata za Muganza na Buseresere lakini hadi sasa hakuna
kilichofanyika kwani vikundi hivyo havikuzalisha kitu chochote tangu
wakati huo. Aidha, Bw. Mutayoba anatuhumiwa kudai na kupokea rushwa kwa
wanachama wa vikundi vya ujasiriamali ili aweze kuvisaidia kupata
mikopo. “Yaani watu wanakuja kukopa sh. milioni mbili halafu unawadai
kitu kidogo cha sh. 300,000. Sasa mradi waliotaka kufanya wataweza
kuukamilisha kweli?,” alihoji Waziri Mkuu.
“Huyu bwana amelalamikiwa lakini Mkurugenzi aliyepita
lakini naye anadaiwa kumlinda kwa sababu ni rafiki yake,” alisema Waziri
Mkuu na kuibua minong’ono ndani ya ukumbi huo. Aliyekuwa Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Chato, Bw. Clement Berege hivi sasa amehamishiwa
Halmashauri ya Wilaya ya Iramba.
“Katika Serikali hii tunataka tuwe na Halmashauri zilizo
safi. Lakini pia Serikali hii ina mkakati wa kuimarisha ushirika na
tunataka kuinua kilimo. Kwa hiyo basi, TAKUKURU na polisi wachunguzeni
hawa watu wawili kwa maana ya Afisa Ushirika na Afisa Maendeleo ya Jamii
na nipewe taarifa uchunguzi utakapokamilika,” alisema Waziri Mkuu.
Mapema, akizungumza na watumishi hao,
Waziri Mkuu ambaye amewasili mkoani Geita kwa ziara ya siku mbili
akitokea mkoani Kagera, alitumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi hao
aliwakumbusha wajibu wao wa kuwahudumia Watanzania bila kujali hali zao
na akasisitiza kuwa Serikali haitamuonea mtumishi yeyote ambaye
anatimiza wajibu wake.
“Napenda kusisitiza kuwa malengo ya Serikali ni kuimarisha
utendaji wa watumishi lakini pia Serikali hii haitamvumilia mtu
mdanganyifu, mzembe, asiye mwadilifu na mla rushwa. Ukiharibu kazi hapa
Chato mwwisho wako ni hapa hapa tu. Usitarajie kupelekwa Bunda au
kwingine ili ukaharibu na huko,” aliongeza.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
ALHAMISI, MACHI 17, 2016.
No comments:
Post a Comment