DARAJA LA KIGAMBONI KUFUNGULIWA RASMI APRILI.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amesema
daraja la Kigamboni litafunguliwa rasmi Aprili, 16 mwaka huu.
Amesema
kazi inayoendelea sasa hivi ni kupitisha magari maalum kwa ajili ya
kupima ubora wa daraja hilo ili kujiridhisha kabla ya kukabidhiwa rasmi
Serikalini.
Amewataka
watumiaji wa daraja hilo kuwa waangalifu, kulinda miundombinu na
kuepuka vitendo vya hujuma ili lidumu kwa muda mrefu.“Daraja hili lina
urefu wa mita 640, barabara sita, tatu zinapanda na tatu zinashuka,
hivyo tunawaomba wananchi watakaovuka kuzingatia usafi na ustaarabu”,
amesema Profesa Mbarawa.
Amebainisha
kuwa Serikali itaweka sheria kali kwa wote watakaokiuka matumizi sahihi
ya daraja hilo na kusisitiza umuhimu wa madereva kuzingatia sheria za
usalama barabarani wanapovuka katika daraja hilo.
Meneja
Msimamizi wa ujenzi wa daraja hilo Eng. Karim Mattaka amesema wataalam
wanaendelea na taratibu za kulipima daraja hilo ili kujiridhisha kama
linamudu kupitisha uzito uliokusudiwa kabla ya kulikabidhi kwa Serikali
mapema mwezi ujao.
Amesema
awamu ya kwanza ya kulipima daraja hilo imekamilika na sasa wanaendelea
na awamu ya pili hadi watakapomaliza awamu nne ili kujiridhisha kabla
ya kuanza kutumika.
Takribani
shilingi bilioni 216 zimetumika katika ujenzi wa daraja hilo
linalotazamiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa abiria na
magari katika kivuko cha Magogoni na Kigamboni.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akipata
maelezo kutoka kwa Meneja Msimamizi wa ujenzi wa daraja la Kigamboni
Eng. Karim Mattaka alipokagua daraja hilo leo jijini Dar es salaam.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa
maelekezo kwa Meneja miradi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Eng.
John Msemo wakati alipotembelea daraja la Kigamboni kuangalia ujenzi wa
daraja la Kigamboni leo jijini Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment