AFISA MIFUGO ANUSURIKA KUTUMBULIWA JIPU NA WAZIRI MKUU
AFISA MIFUGO wa kata ya Kakunyu, wilayani Misenyi mkoani Kagera, Bw.
Eric Kagoro amenusurika kutumbuliwa jipu kwenye mkutano wa hadhara
kuhusiana na sakata la kuruhusu ng'ombe 291 waje kulishwa kwenye
ranchi ya mifugo ya Misenyi.
Tukio hilo limetokea leo mchana (Jumatatu, Machi 14, 2016) wakati
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na mamia ya wananchi waishio
jirani na ranchi hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye
makao makuu ya ranchi hiyo.
Waziri Mkuu alimuibua Bw. Kagoro katikati ya mkutano kwa kumtaja jina
na tuhuma zinazomhusu kuhusu mifugo iliyokamatwa. "Afisa Mifugo wa
kata yupo hapa? Aliuliza Waziri Mkuu. Wewe ndiyo Eric?" Alipojibu
ndiyo akaulizwa tena:"Nimekujuaje?"
"Nimeambiwa wale ng'ombe waliokamatwa ni wa rafiki yako na wewe ndiye
ulitoa libali waje kulishwa kwenye ranchi hii. Siyo kazi yako kuruhusu
mifugo ya nje ije kulishwa hapa kwenye ranchi. Kuanzia sasa ni
marufuku kwa mtu yeyote kuingiza mifugo kwenye ranchi ili ipate
malisho "
"Leo Nimekusamehe .Kazi yako ni kuhakikisha mifugo ya kwenye kata hii
iko salama. Kazi yako ni kuwasaidia wafugaji wa kata hii wafuge vizuri
na uhakikishe mifugo yao inakuwa na tija." alisema Waziri Mkuu huku
akishangiliwa.
Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaasa
watendaji wa kata na vijiji kutotumia nafasi zao kuleta migogoro baina
ya watu wa nje na wananchi wanaowaongoza. "Mwenyekiti wa kijiji huna
ruhusa ya kugawa kitalu cha ranchi au kuruhusu mtu yeyote akalime
ndani ya ranchi", alisema.
Aliwataka pia maafisa uhamiaji wawe makini na vyeti vya kuandikisha
uraia wanavyovitoa kwa wananchi wanaoishi mipakani kwani imekuwa ni
mianya ya kuleta migogoro ya ardhi. "Watu wa uhamiaji kuweni makini na
CN mnazotoa (CN=Certificate of Naturalisation). Wote wanaoomba CN
wanataka blocks tu"
Alitoa agizo kuwa watafutwe watu wote walioingia nchini kwa mgongo wa
CN, wakamatwe na kurejeshwa makwao. "Kuna watu wamekuja hapa nchini
wakaomba CN lakini wakikaa wanaleta wenzao waje kununua ardhi kwa
kutumia mgongo wa CN zao."
Alisema kuna watu wametoja wilaya ya Karagwe ambako pia kuna tatizo
kama la Misenyi na kuwataka wahusika wajiandae kuchujwa na kuchukuliwa ardhi zao kama watakuwa hawajaziendeleza ili wapewe Watanzania wenye uhitaji wa kulima na kufuga.
No comments:
Post a Comment