ACT WAZALENDO WAMTAKA SPIKA WA BUNGE KUSHUGHULIKIA SUALA LA RUSHWA KWA WABUNGE WALIOTUHUMIWA.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge na Serikali za Mitaa, wa ACT Wazalendo, Yeremia
Maganja akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya Chama
cha ACT Wazalendo wakimtaka Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kuunda mara moja kamati ya uchunguzi kwa kamati zote
zilizotuhumiwa ili ukweli ubainike na hatua za kisheria zichukuliwe mara
moja ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu
Mawasiliano wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu.
Katibu
Mawasiliano wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu akisisitiza jambo katika
mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge na Serikali za Mitaa wa ACT Wazalendo, Yeremia Maganja.
Waandishi
wa habari wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge na Serikali za
Mitaa wa ACT Wazalendo, Yeremia Maganja leo Jijini Dar es Salaam.
(Picha na Emmanuel Massaka, Globu ya Jamii)
Na Chalila Kibuda, Globu ya Jamii.
CHAMA cha ACT Wazalendo kimepokea kwa masikitiko uamuzi uliofanywa
na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, kwa
kuhamisha kamati, Wenyeviti, Makamu Wenyeviti na Wajumbe wa baadhi ya
Kamati za Kudumu za Bunge uliofanywa jana.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo,
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge na Serikali za Mitaa ACT Wazalendo,
Yeremia Maganja,
amesema uamuzi huu wa spika unafuatia kashfa nzito ya viongozi na
wajumbe wa kamati mbalimbali za Bunge kupokea rushwa kutoka mashirika
tofauti ya umma kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari
Amesema bunge ni mhimili wenye jukumu la kuisimamia serikali ,
hivyo baadhi ya wabunge akiwemo Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT
Wazalendo) walimwandikia barua za kujiuzulu Spika wa Bunge, Job Ndugai
ili kupisha uchunguzi ufanyike na wataobainika kupokea rushwa
kuchukuliwa hatua za kisheria.
Maganja amesema ACT Wazalendo imempongeza Mbunge wao na Wabunge
wengine waliochukua hatua ya kujiuzulu ujumbe kwenye kamati zao ili
kupisha uchunguzi.
Aidha amesema kuwa uamuzi huo wa mbunge wao unakwenda sambamba na misingi ya Chama cha ACT Wazalendo ya uadilifu na uwajibikaji.
Amesema mabunge yaliyopita, kamati za Bunge zimekuwa zikituhumiwa
mara kadhaa kujihusha na vitendo vya kupokea rushwa kutoka kwa Mashirika
ya Umma, Makampuni na watu binafsi.
Maganja amesema rai zimekuwa zikitolewa mara kwa mara huko nyuma
ya kuitishwa kwa uchunguzi ili kulinda hadhi na heshima ya Bunge
ilipuuzwa na matokeo yake, kashfa hizi zimeliondolea heshima Bunge na
Wabunge.
Amesema kwa mujibu wa Ibara ya 63(2) ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Bunge ndiyo chombo kikuu chenye madaraka kwa niaba
ya wananchi kuisimamia na kuishauri serikali na vyombo vyake vyote
katika utekelezaji wa majukumu yake. Kinapotuhumiwa kupokea rushwa,
kinawezaje chenyewe kuisimamia serikali na kuongoza mapambano dhidi ya
rushwa?
Maganja amesema uamuzi wa kuwahamisha Kamati viongozi na wajumbe
wa Kamati zilizotuhumiwa kupokea rushwa ni sawa na kuufunika uozo na
kuendeleza utamaduni mbovu wa siku nyingi hapa nchini wa kuwahamisha au
“kuwapangia kazi nyingine” viongozi na watumishi wa umma wanaotuhumiwa
kupokea rushwa au kukosa ufanisi. Kimsingi Utamaduni huu unafifisha
mapambano dhidi ya rushwa na uwajibikaji.
Mwenyekiti huyo amemtaka Spika kuonyesha kwa vitendo jinsi ofisi
yake inavyochukizwa na vitendo vya rushwa nchini kwa kuitisha uchunguzi
utaovishirikisha vyombo vya dola ili ukweli ujulikane.
No comments:
Post a Comment