CHF Mkombozi wa kweli kwa afya ya Jamii
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Ni jambo lisilopingika kokote duniani kuwa afya bora ndio chanzo cha maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla.
Afya ikiwa bora binadamu anakuwa na uwezo wa kuwaza na kufanya mambo mbalimbali yenye tija kwake na kwa taifa lake.
Kwa
kuonyesha kujali afya zetu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)
ilianzisha Mfuko wa Afya ya Jamii ujulikanao kama CHF ambao ulianza kwa
majaribio wilayani Igunga, Mkoa wa Tabora mwaka 1996 na kuanza rasmi
2001 baada ya bunge kupitisha muswada huo.
Chimbuko
hasa la kuanzisha Mfuko wa Afya ya Jamii ni kupungua kwa rasilimali na
vyanzo vya mapato vya kuhudumia sekta ya afya hivyo kusababisha kudorora
kwa huduma hiyo ambapo inasababisha wananchi kutopata matibabu
yanayotakiwa na wengine kuacha kabisa kwenda kupata huduma katika vituo
vya afya kwa kuwa gharama za matibabu ni kubwa.
Mfuko
wa Afya ya Jamii yaani CHF ni utaratibu wa hiari unaomuwezesha mtu
binafsi,vikundi au kaya kupata huduma za matibabu kwa mwaka mzima kwa
kuchangia kiasi cha shilingi 5000 hadi 20000 kwa kadri ya uwezo wa mtu
au jamii yenyewe kulingana na Halmashauri husika itakavyoamua.
Kiasi
hiki cha kuchangia kwa mwaka kinaweza kupatikana hata kwa mtu mwenye
kipato cha chini kwakua kiwango hiki ni sawa na bei ya kuku mmoja,
uchangiaji huu ndiyo uliyomfanya aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Iramba,
Mhe. Yahaya Nawanda kuja na kauli mbiu isemayo “Kuku mmoja, matibabu
mwaka mzima”. Uhamasishaji huu ulisaidia sana watu wengi kujiunga na CHF katika wilaya hiyo.
Na
kama iliwezekana katika Halmashauri ya Iramba kwa kuku mmoja kugharamia
matibabu ya kaya kwa mwaka mzima, tunaamini kuwa kauli mbiu hiyo
inaweza kufanya kazi pia katika Halmashauri nyingine iwapo kila kiongozi
aliyekabidhiwa dhamana ya kusimamia maisha ya watu atadhamiria kuwapa
wananchi huduma bora za matibabu kwa utaratibu wa kuchangia kabla ya
kuugua.

No comments:
Post a Comment