WAZIRI MKUU AAGIZA TAMISEMI ISIMAMIE VIZURI MIKOA, HALMASHAURI
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ndiyo kitovu cha nchi na kwamba kila
Mtanzania ameelekeza jicho lake pale kwa sababu anasubiri kupata huduma
ya msingi.
“Hapa ndiyo kitovu cha nchi na Watanzania wote macho yao yako
huku. Kwa nini? Kwa sababu huduma zinasowagusa za barabara, maji, elimu,
zinatokea huku kwa maana ya bajeti na usimamizi,” alisema.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Januari 21, 2016) wakati
akizungumza na wakurugenzi, wakuu wa taasisi na watumishi wa Ofisi ya
Rais – TAMISEMI kwenye mkutano uliofanyika ofisi ya TAMISEMI mjini
Dodoma.
“Wananchi wakilalamikia ukosefu wa hizi huduma chanzo ni hapa.
Katika wizara kuna mawaziri lakini wao kule ni wasimamizi wakuu. Ninyi
chini yenu kuna mikoa, wilaya, halmashauri, rasimali watu na raslimali
fedha za kuwasaidia kufikisha huduma tarajiwa kwa Watanzania walio
wengi,” alisisitiza.
Waziri Mkuu ameitaka ofisi hiyo ihakikishe inaisimamia vizuri
mikoa na halmashauri ili Serikali iweze kupata matokeo mazuri na
tarajiwa.
Waziri Mkuu alisema jukumu kubwa lililopo hivi sasa katika Mamlaka
za Serikali za Mitaa ni kuhakikisha kuwa zinabuni vyanzo vipya vya
mapato na kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya serikali.
“Hatukubaliani na uzembe kwenye idara na halmashauri za wilaya kwa
kuwa hivi sasa Serikali ya Awamu ya Tano inasimamia utumishi uliotukuka
na wenye uadilifu hivyo kila mmoja ahakikishe anasimamia vizuri eneo
lake,” alisema.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imekusudia kuwahudumia ipasavyo
Watanzania wenye uelewa tofauti na matakwa tofauti na kwa kuanzia
Serikali imeanza kuwajenga watumishi wa Serikali kutambua kuwa wao ni
wahudumu wa wananchi hivyo inawapasa kuwahudumia vema.
“Lazima tujenge moyo wa huruma wa kuwahudumia wenzetu, anapokuja
mwananchi msikilize, mhudumie na mwelekeze eneo sahihi ili aweze kupata
huduma. Lazima tusimamie na kuona maeneo yote yanafanya kazi kama
ilivyokusudiwa, ili kupata matokeo tarajiwa iwe ni wajibu ya kila mmoja
kuhakikisha kuwa anatoa usimamizi thabiti katika eneo lake,”
alisisitiza.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na watumishi hao,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Bw. George Simbachawene
alisema TAMISEMI wapo tayari kubadilika na kufanya kazi kama kauli ya
Rais John Pombe Magufuli inavyotaka, yaani HAPA KAZI TU.
Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Bernard Makali
alimpongeza Waziri Mkuu Majaliwa kwa kusimamia vizuri masuala ya elimu
nchini wakati akiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya
elimu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
L. P. 980,
DODOMA.
ALHAMISI, JANUARI 21, 2016.
No comments:
Post a Comment