UZINDUZI WA STIKA MAALUM YENYE UJUMBE WA KUTOKOMEZA MAUAJI YA ALBINO
Na Nyakongo Manyama-MAELEZO
TAASISI ya watu wenye ulemavu wa
ngozi mkoa wa Dar es salaam inatarajia kufanya uzinduzi wa ‘stika’
maalum yenye ujumbe wa kutokomeza mauaji ya watu wenye albinism
utakaofanyika januari 26 mwaka huu.Akizungumza na waandishi wa
habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa taasisi hiyo Bw. Michael
Lugendo amesema kuwa uzinduzi huo utafanyika katika kituo cha polisi
kati jijini Dar es Salaam kuanzia saa tano asubuhi.
Bw. Michael Lugendo amesema kuwa
stika hiyo ina lengo la kuhamasisha jamii kuungana na Rais Mhe.Dkt. John
Pombe Magufuli na Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es salaam ili
kuyafanya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yatokomezwe na yabaki
kuwa historia.
Kwa upande mwingine Bw. Lugendo
ameongeza kuwa kulingana na kasi ya mabadiliko tabia nchi, jamii
isipochukua hatua za makusudi kuna uwezekano wa watu wenye ulemavu wa
ngozi kuangamizwa na saratani ya ngozi.
Alisema watu wenye ulemavu wa
ngozi wanaishi katika mazingira ya umaskini kiasi kwamba waliowengi
hawana uwezo wa kupata fedha ya kununua mafuta ya kuzuia mionzi ya jua
ambayo husababisha saratani ya ngozi.“Sisi watu wenye ulemavu wa ngozi
ni wahanga wakubwa sana na jamii isipochukua hatua za makusudi upo
uwezekano wa kuangamizwa na saratani ya ngozi ukizingatia kwamba
tunaishi katika mazingira ya umaskini na walio wengi hatuna uwezo wa
kupata fedha ya kununua mafuta” alisema Bw. Lugendo.
Aidha Bw. Lugendo amesema kuwa
taasisi hiyo imemteua Bw. Mbwana Ally Samata kuwa balozi wa kudumu wa
kusemea watu wenye ulemavu wa ngozi.
Alibainisha kuwa majukumu ya
Nahodha huyo wa Timu ya Taifa ya Tanzania kwa ujumla ni kuhamasisha
dunia kwa njia ya soka kuhakikisha kwamba hakuna mlemavu wa ngozi
anayefariki kwa kifo cha saratani ya ngozi au mauaji ya kukatwa viungo
yanayotokana na Imani za kishirikina.
Bw. Lugendo aliwataka wadau
mbalimbali, kampuni, balozi mbalimbali, Mashirika yasiyokuwa ya Serikali
kujitokeza ili kuwezesha kutimiza lengo hilo kwa kutoa taarifa za
uhalifu dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi kupitia vyombo vya habari
pamoja na jeshi la polisi.
No comments:
Post a Comment