Header Ads

VITA YA TATU YA DUNIA INAWEZA KUTOKEA–MKAPA

Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, amezipa angalizo nchi za Kiafrika kukuza uongozi bora na kuachana na mikataba mibovu isiyojali ustawi wa wananchi kwa kuwa inaweza kuzipeleka katika vita.
Miongoni mwa mikataba ambayo amesema kuwa ni mibovu na isiyofaa, hivyo iepukwe ni wa Kiuchumi
baina ya Mataifa ya Afrika, Caribbean na Pacific (EPA), ili kuepusha vita, ambayo kwa sasa itakuwa ni ya kiuchumi.
Aidha, ametaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) lifumuliwe ili kuongeza nchi nyingine ambazo zinastahili kuingia kwa sasa.
Rais huyo wa awamu ya tatu aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati wa mahojiano aliyoyafanya na vyombo vya habari kwenye Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), baada ya kutoa mhadhara kwa wanafunzi wa chuo hicho.
Mkapa alitoa mhadhara kuhusiana na tathmini ya kiuchumi kuelekea vita ya tatu ya dunia.
Mkapa alisema kwa hali ilivyo sasa ni sababu za kiuchumi ndizo zinazoleta vita, kutokana na uongozi mbaya, njaa na kiu ya baadhi ya nchi kutaka maliasili za mataifa mengine.
“Hatutarajii kuwa na vita kama ile ya pili ya dunia, kwa sababu Dunia sasa inamiliki silaha kali kama za nyuklia, zinazoweza kuangamiza maisha kwa wingi, na ndiyo maana unaona mazungumzo kupunguza silaha za nyuklia kama yale ya Iran,” alisema.
Alisema ili kuzuia vita kutokea ndani ya nchi, ama kati ya nchi mbili, ukanda, bara na hata dunia, kuna umuhimu wa serikali zilizoko madarakani na hasa barani Afrika kuwekeza kwenye uongozi bora na kuwashirikisha wananchi katika maamuzi ya kidemokrasia, yanayohusu maisha na rasilimali za nchi zao.
“Ni vizuri kuwa na sera zinazojenga, zisizogawa wananchi katika misingi ya udini na ukabila, kuhakikisha mikataba inayoingiwa juu ya rasilimali za nchi inawanufaisha wananchi na si wageni peke yao, na kama kuna unahitaji wa kuirekebisha, ni bora hilo likafanyika,” alisema.
Alisema mikataba kama ule wa EPA, si ya kuiruhusu kwani mwisho wa siku itaua juhudi za nchi maskini kuendelea, kwa sababu zinalenga kuifanya Afrika kuwa soko la bidhaa za Ulaya.
“Mazungumzo juu ya EPA kwa nchi nyingi zilizo kwenye eneo la Sahara ni kama yamemalizika, kinachosubiriwa sana sana na kuridhiwa na mabunge, lakini mkataba huu kimsingi haufai kwa nchi zetu za Afrika,” alitahadharisha Mkapa.
Mkapa alisema: “Iwapo EPA itaridhiwa na mataifa yetu, itakuwa ni chanzo cha kudhoofisha kilimo chetu, viwanda vyetu, malighafi  hazitasindikwa na maduka yetu yatajaa bidhaa za Ulaya na mwisho wa siku ajira itakosekana.”
Akizungumzia suala la muundo wa sasa wa UNSC, Mkapa alisema: “Kuna umuhimu wa kuifumua taasisi hiyo kwa sababu dunia sasa imebadilika, tofauti na ilivyokuwa wakati inaundwa,” alisema.
Alisema tasisi hiyo inastahili kufumuliwa na kuundwa upya kwa sababu hivi sasa kuna mataifa ambayo yameendelea sana kiuchumi na kiuwezo katika dhana za kivita na hivyo kustahili kuwamo ndani yake.
Alisema mataifa hayo yanastahili kuwamo ndani ya taasisi hiyo kwa sababu ya ushawishi na nafasi yaliyonayo sasa, inayoyafanya yawe na mchango kwenye maamuzi ya taasisi hiyo.
Taasisi hiyo ina nchi wanachama 15, nchi tano zikiwa ni wanachama wa kudumu, zenye kura ya turufu na nchi 10 zikiwa si wanachama wa kudumu.
Nchi wanachama wa kudumu na zenye kura ya turufu ni Marekani, Urusi, Uingereza, Ufaransa na China.
Kumekuwapo na kilio cha siku nyingi cha kutaka chombo hicho kufanyiwa marekebisho kwa kukipanua na kuzipa nchi nyingine zaidi nafasi za uwakilishi. Baadhi ya nchi ambazo zinapendekezwa ni Brazil na India huku ikipendekezwa Afrika kuwakilishwa na Nigeria na Afrika Kusini.
Kwa upande wake, Mkuu wa chuo hicho, Meja Jenerali Gaudens Milanzi, alisema ujio wa mkuu huyo wa nchi mstaafu, ni faraja kwao kama chuo cha Taifa cha ulinzi.
“Hii inaonyesha kuwa bado viongozi wetu waliopita wanaendelea kukienzi chuo, na bado wanaendelea kuchangia mawazo yao kama kawaida kwenye masuala ya usalama na stratejia nchini na katika dunia kwa ujumla wake,” alisema Jenerali Milanzi.
NIPASHE

No comments:

Powered by Blogger.