Bondia chipukizi Mtanzania, Amos Mwamakula, 23, ameendelea kutesa katika ndondi za kulipwa nchini Brazil
Bondia chipukizi Mtanzania, Amos Mwamakula, 23, ameendelea kutesa katika ndondi za kulipwa nchini Brazil baada ya kumtwanga kwa pointi bondia Edgar Canto wa Brazil na kunyakuwa ubingwa wa mkanda wa UFC kwenye Ukumbi wa Luis Antonio jijini Sao Paulo.
Mwamakula anaishi nchini Brazil katika jiji la Sao Paulo tangu Novemba mwaka jana na amekuwa kivutio kwa mashabiki wa mchezo wa ngumi nchini Brazil licha ya kutelekezwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Brazil.
Alimtwanga Canto kwa pointi na kufanikiwa kumuangusha mara mbili katika pambano ambalo lilionyeshwa moja kwa moja na kituo kikubwa cha televisheni cha Brazil, TV Knockout, huku akishuhudiwa na mashabiki wa mchezo huo Amerika Kusini.
Hilo lilikuwa pambano la tatu kwa Mwamakula ambaye awali alipoteza pambano lake la kwanza dhidi ya Bondia Rodrofh wa Brazil na kisha kushinda pambano lililofuata dhidi ya Sam Silva naye wa Brazil.
Hata hivyo, licha ya kufanya vyema katika mapambano yake, Mwamakula ambaye kabla ya kutua Brazil alikuwa akipigana nyumbani Tanzania, ameulalamikia ubalozi wa Tanzania nchini Brazil kwa kumtelekeza.
“Nimewaalika watu wa ubalozini kwetu mara tatu waje kunishuhudia lakini hawajafika hata mara moja. Nimewatumia namba zangu za simu lakini hawajanipigia walau kunipongeza.
Inasikitisha sana kwamba wanashindwa kutoa sapoti kwa mtu wao ambaye nakubalika miongoni mwa jamii ya Wabrazili na sijabadili uraia wangu.” alisema Mwamakula
No comments:
Post a Comment