Header Ads

Wafanyakazi wa Airtel watoa mafunzo ya Kompyuta shule ya sekondari ya Kiromo

Mkuu wa mapato wa Airtel, Bw. Hoolass Lochee akiwafundisha kompyuta baadhi ya watoto wa shule ya msingi ya Kiromo iliyopo wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani ikiwa ni baada ya wafanyakazi wa Airtel kuitembelea shule hiyo kwa dhumuni la kutoa mafunzo ya kompyuta.
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule ya sekondari ya Kiromo, Bw. Joseph Ngunangwa akiwaelezea wafanyakazi wa kampuni ya simu za mkononi ya Airtel jinsi ambavyo kiwango cha ufaulu kimepanda shuleni hapo tangu Airtel ilivyoamua kuiendeleza shule hiyo kuanzia ujenzi hadi kwenye vifaa vya kufundishia ikiwa ni baada ya wafanyakazi wa Airtel kuitembelea shule hiyo iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani kwa dhumuni kubwa la kutoa mafunzo ya kompyuta kwa wanafunzi.
Mkurugenzi wa Idara ya Fedha wa Airtel Tanzania, Bw. Kalpesh Mehta akiwafundisha matumizi ya kompyuta baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari ya Kiromo iliyopo wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani. Wanafunzi wa shule hiyo walipata nafasi ya kujifunza kompyuta katika hatua za awali baada ya wafanyakazi wa Airtel kuitembelea shule hiyo leo.
Baadhi ya wafanyakazi wa Airtel mwishoni mwa wiki wameitembelea shule ya msingi ya Kiromo iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani na  kutoa mafunzo ya awali juu  ya matumizi ya kompyuta kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Wafanyakazi hao wamedai kuwa kujitolea kwenda kutoa mafunzo katika shule hiyo ambayo ilijengwa na kampuni yao kupitia mradi wa shule yetu sio jambo la msimu tu kwani wana mpango wa kuendelea kutoa huduma hiyo mara kwa mara katika shule mbalimbali nchini.
Mkurugenzi wa idara ya Fedha ya Airtel, Bw. Kalpesh Mehta alisema Airtel inaelewa wazi ni jinsi gani matumizi ya vifaa kama kompyuta hurahisisha kazi nyingi katika jamii na hivyo imeamua kwenda kutoa mafunzo ya ujumla kwa wanafunzi wa shule hiyo kwa dhumuni la kuleta mchango chanya kwenye jamii.
“Kompyuta ni kifaa muhimu sana ambacho hurahisisha kazi mbalimbali zinazofanywa kwa ajili ya maendeleo ya jamii hivyo inabidi wanafunzi waanze kujifunza juu ya umuhimu wa kifaa hiki mapema katika kusaidia maendeleo ya jamii huko mbeleni.” Alisema Mehta.
Kwa upande wake Mwalimu mkuu msaidizi wa shule ya Kiromo, Bw. Joseph Ngunangwa alisema masomo hayo yametoa hamasa kubwa sana kwa wanafunzi wa shule hiyo kwa sababu yamewafanya wahisi masomo hayo yana urahisi na sio magumu kama walivyokuwa wakifikiria.
“Wanafunzi walikuwa na mitazamo kwamba wanaojifunza kompyuta ni tabaka flani tu la watu na walikuwa wakihisi kwamba kompyuta ni somo gumu lakini leo  wametiwa moyo na wafanyakazi wa Airtel na wameanza kuona kuwa somo hilo ni rahisi na yeyote anaweza kulisoma na kufaulu vyema,” alisema Pangahela.
Mwalimu huyo aliongeza kuwa kupitia masomo hayo idadi ya wanafunzi watoro imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na sababu kuwa wengi huja shule kwa ajili ya kujifunza kompyuta.
Kwa upande wao wanafunzi wa shule ya Kiromo waliwashukuru wafanyakazi wa Airtel kwa kuonesha ukarimu mkubwa sana na kusema kuwa wanatamani masomo hayo yangekuwa yanafanyika kila siku.
Si mara ya kwanza kwa wafanyakazi wa Airtel kuzitembelea shule na kutoa mafunzo kama hayo vile vile Kampuni hiyo hutoa misaada ya vitabu mbalimbali vya kiada nchini na kuchangia katika ujenzi wa taifa hususani katika sekta ya elimu.

No comments:

Powered by Blogger.