JK AKUTANA NA PRINCE CHARLES JIJINI COLOMBO, SRI LANKA, AHUDHURIA UFUNGUZI WA CHOGM 2013
Mrithi wa Kiti cha
 Ufalme wa Uingereza, Prince Charles ambaye pia ni Mtoto wa Malkia wa 
nchi hiyo, Malkia Elizabeth II ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa 
hatua zake za dhati za kulinda wanyamapori na kupambana na ujagili dhidi
 ya tembo na faru. 
 Aidha,
 Prince Charles amesema kuwa yuko tayari kuunga mkono juhudi hizo za 
Tanzania kwa kushirikiana na mtoto wake, Prince William ambaye amechagua
 shughuli za kulinda wanyamapori na kupambana na ujangili duniani kama 
moja ya shughuli zake kuu. 
 Moja
 ya hatua ambazo Prince Charles ameamua kuchukua ni kukabiliana na soko 
la bidhaa kuu za ujangili duniani, na hasa meno ya tembo na faru, na 
kufanya kampeni kubwa duniani dhidi ya biashara hiyo haramu. 
 Prince
 Charles ametoa pongezi hizo na msimamo wake wa kuunga mkono jitihada za
 Tanzania wakati alipokutana kwa mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya 
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Viongozi hao wamekutana kwenye Jumba la Tintagel mjini Colombo, Sri 
Lanka, ambako amefikia wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa 
Jumuiya ya Madola (CHOGM) ambao Prince Charles ameufungua rasmi asubuhi 
ya leo, Ijumaa, Novemba 15, 2013, kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mahinda 
Rajapaksa. 
Rais
 Kikwete naye yuko Sri Lanka kuhudhuria Mkutano huo.
 
Wakati wa mazungumzo hayo, Rais Kikwete ametumia muda mrefu kumwelezea 
Prince Charles kuhusu hatua ambazo zimekuwa zinachukuliwa na Serikali 
yake kupambana na ujagili dhidi ya tembo na faru ikiwamo Operesheni 
Maalum – Operesheni Tokomeza -ambayo ilifanyika hivi karibuni kuwasaka 
na kukabiliana na wafanya biashara haramu ya meno ya tembo.
 Rais
 Kikwete amemwambia Prince Charles kuwa pamoja na kuchunguza malalamiko 
yaliyotolewa na makundi mbali mbali ya watu kuhusu operesheni hiyo ya 
kwanza, bado operesheni hiyo itaendelea kwa sababu ni muhimu kulinda 
wanyamapori dhidi ya majangili.
“Imefika mahali ambako tunahitaji kuchukua hatua kali. 
Wakati
 wa Uhuru wetu kulikuwepo na tembo kiasi cha 350,000 lakini ilipofika 
mwaka 1989 idadi hiyo ilikuwa imepungua na kubakia 55,000. Hata hivyo, 
baada ya operesheni maalum na kubwa, idadi hiyo ilikuwa imeongezeka hadi
 kufikia 110,000 kabla ya kuanza wimbi jipya la ujangili mwaka 2010. 
Operesheni lazima iendelee,” Rais Kikwete amemwambia Prince Charles. 
 “Tusaidie
 kufunga na kuvuruga hili soko la bidhaa za wanyampori. Operesheni ya 
sasa imethibitisha kuwa mtandao wa uwindaji haramu na biashara haramu ya
 meno ya tembo na faru ni mkubwa na watu wengi wanahusika, lakini 
kinachovuruga zaidi ni kwamba lipo soko la uhakika la meno ya tembo.” 
 Prince
 Charles amemweleza Rais Kikwete kuhusu hatua ambazo anakusudia 
kuzichukua kukabiliana na hali hiyo, ikiwa ni pamoja na kuandaa mkutano 
mkubwa wa wakuu wa nchi na Serikali Februari 13, mwakani na kufanya 
mkutano mwingine mkubwa na vyombo vya habari kutoka pote duniani 
mwakani. 
 “Nakusudia
 pia kutumia wasanii nyota mbali mbali duniani kuendesha kampeni ya 
kuielimisha dunia kuhusu athari za biashara hiyo haramu kwa sababu 
asilimia kubwa ya mapato ya ujangili inasaidia kugharimia vikundi vya 
kigaidi duniani.” 
Rais
 Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Mwana wa Malkia  Elizabeth II wa 
Uingereza, Prince Charles,  jijini Colombo, Sri Lanka, leo Novemba 15, 
2013 pembeni ya mkutano wa Wakuu wa nchi za Junuiya ya Madola (CHOGM 
2013) ambako Prince Charles, maarufu zaidi kama His Royal Highness the 
Prince of Wales, anamwakilisha mama yake mwenye umri wa miaka 87 ambaye 
hakuhudhuria kwa mara ya kwanza katika miaka 40 ya historia ya mkutano 
huo unaofanyika kila baada ya miaka miwili katika nchi itayoteuliwa 
mwishoni mwa mkutano. Kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe 
Peter Kallaghe.
Malkia
 Elizabeth wa II alihudhuria CHOGM kwa mara ya kwanza mwaka 1973 jijini 
Ottawa, akiwa kakosa kikao cha mwaka 1971, na tokea hapo hajakosekana 
tena hadi safari hii. Alikuwepo pia katika mkutano wa mwisho uliofanyika
 mwaka 2011 jijini  Perth,
 Australia. Na hii ni mara ya kwanza kwa Prince Charles kumwakilisha mama yake ambaye imesemekana hakwenda Sri Lanka kutokana na ushauri wa kutosafiri umbali mrefu. Ila katika CHOGM 2007 iliyofanyika Kampala, Uganda, yeye na mama yake walihudhuria pamoja.
Sherehe
hizo zilizofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Nelum Pokuna Mahinda Rajapaksa
mjini Colombo, Sri Lanka, ziliendelea kwa karibu saa mbili kuanzia saa nne
kamili asubuhi.
Miongoni
mwa viongozi ambao walizungumza kwenye sherehe hiyo ya ufunguzi ni Rais wa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kisoshalisti ya Sri Lanka, Mheshimiwa Mahinda
Rajapaksa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Mheshimiwa Kamalesh Sharma.
Mrithi
wa Kiti cha Ufalme wa Uingereza Prince Charles ndiye amefungua rasmi Mkutano
huo kwa niaba ya Mama yake, Malkia Elizabeth ambaye ni Mkuu wa Jumuiya ya
Madola. Malkia Elizabeth hakuweza kuhudhuria Mkutano huo.
Mara
baada ya ufunguzi huo uliopambwa na ngoma za kuvutia sana ukiwamo muziki wa
vijana na maonyesho ya watoto wa shule ambao walizunguka Ukumbi wa Mikutano,
wakuu hao walihamia kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kumbukumbu wa Bandaranaike kwa
ajili ya kuanza vikao rasmi.
Wakati
wa chakula cha mchana, viongozi hao walihudhuria hafla rasmi iliyoandaliwa na
Mheshimiwa Sharma na baadaye jioni wamehudhuria Chakula cha Usiku
kilichoandaliwa na Prince Charles na mkewe, The Duchess of Cornall kwenye
Hoteli ya Cinnamon Lakeside.
Imetolewa na; 
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, 
Ikulu, DAR ES SALAAM. 
 15 Novemba, 2013


No comments:
Post a Comment