DK MVUNGI AZIKWA KIJIJINI CHANJALE KISANGARA JUU
Aliyekuwa
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi alizikwa
jana kijijini kwake, Chanjale, Kisangara Juu katika mazishi ambayo
yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiongozwa na Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda, wajumbe wa tume hiyo, vyama vya siasa na wananchi.
Akizungumza
katika mazishi hayo, Askofu Rogath Kimario wa Kanisa Katoliki Dayosisi
ya Same alisema tukio la kushambuliwa lililosababisha kifo chake
halikuwa la ujambazi.
Akizungumza
wakati wa ibada ya mazishi iliyofanyika Kanisa la Moyo Mtakatifu Yesu
la Parokia ya Kisangara Juu iliyopo Chanjale, ambayo pia ilihudhuriwa na
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha, Josephat Lebulu; Askofu wa Jimbo la
Mbulu, Beatus Kinyaiya na Askofu Damiani Ngalu wa Geita wote wa Kanisa
Katoliki, Askofu Kimario alisema waliofanya mauaji hayo ni wauaji wa
kimtandao na kuitaka Serikali kutoa majibu sahihi kuhusiana na tukio
hilo badala ya majibu mepesi yasiyofanyiwa utafiti.
Kauli
hiyo ilionekana kujibu ile ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, Suleiman Kova kuwa mauaji ya Dk Mvungi ni tukio la ujambazi.
“Eti
waliotenda hilo ni majambazi, nani kasema ni majambazi?... Ni research
(utafiti) ipi ama upelelezi gani umefanyika?… Hawa ni wauaji wa
kimtandao, kuna maswali mengi yasiyo na majibu,” alisema Askofu Kimario
na kuongeza:
“Ni
kifo cha fedheha hata kuku hauawi hivyo. Watu wana uchungu, kila mtu
ana maswali ambayo hayana majibu… kwa nini auawe? Kwani alikuwa tajiri
hata majambazi watake pesa?”
Askofu
Kimario alisema Watanzania wanamlilia Dk Mvungi na familia yake
inamlilia kama ambavyo wasomi na wanazuoni wanavyomlilia hivyo Serikali
inawajibika kutoa majibu sahihi juu ya kifo chake.
“Damu
yake inadai Watanzania tujiulize Dk Mvungi yuko wapi… wanausalama ndugu
yetu yupo wapi? Wasomi mlikuja hapa kwenye harusi yake mkafurahi naye
leo mnatuletea marehemu,” alisema.
Askofu
huyo alisema kinachofanya taifa kubwa kama Marekani liheshimike ni
wepesi wake wa kuwaeleza wananchi wake ukweli na kutaka Watanzania
wasiridhike na majibu mepesi ya kifo hicho.
“Tusiridhike
na majibu rahisi. Marekani wanafanya uchunguzi mpaka ukweli unajulikana
kama ilivyokuwa kwa Osama Bin Laden… ilichukua muda mrefu lakini ukweli
ulijulikana,” alisema.
Akitoa
salamu za Serikali katika mazishi hayo, Waziri Mkuu Pinda alisema
Serikali inafanya jitihada kuwakamata waliohusika na mauaji hayo.
“Ni
kweli Serikali inafanya jitihada za kuwakamata waliofanya tukio hili la
ovyo lakini hata tukiwapeleka mahakamani wakahukumiwa kunyongwa hiyo si
mbadala wa Dk Mvungi,” alisema.
Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alisema watamuenzi
Dk Mvungi kwa kukamilisha kazi ya kutunga Katiba Mpya yenye masilahi ya
nchi.
“Tunawaomba
wananchi wote tumuenzi Dk Mvungi kwa kuangalia mapendekezo ya Katiba
kwa masilahi ya Taifa ili tupate Katiba ya maridhiano,” alisema.
Mwenyekiti
wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba
alisema kifo cha Dk Mvungi kimewaumiza lakini akasisitiza kuwa tukio
hilo halitarudisha nyuma harakati za kupigania haki ya Watanzania.
Baadhi
ya viongozi waliohudhuria mazishi hayo ni Waziri wa Maji ambaye pia ni
Mbunge wa Mwanga, Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira, Waziri wa Uchukuzi Dk
Harrison Mwakyembe na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki.
Wengine
waliohudhuria ibada hiyo ni Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia
na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment