Serikali kuanza uchimbaji wa madini ya urani.
Naibu Kamishna wa Madini toka Wizara ya
Nishati na Madini Mhandisi Ally Samaje (KULIA) Akieleza kwa waandishi wa Habari
kuhusu uanzishwaji wa Mradi wa Uchimbaji Madini ya Urani eneo la mto Mkuju,
Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma, wakati wa Mkutano uliofanyika leo Jijini Dar
es Salaam katika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO).Kushoto ni Mkurugenzi wa
Idara ya Habari (MAELEZO) Bw. Assa Mwambene.Picha na Georgina
Misama-Maelezo.
======== ====== =======
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA
YA NISHATI NA MADINI
UANZISHAJI
WA MRADI WA UCHIMBAJI MADINI YA URANI ENEO LA MTO MKUJU, WILAYA YA NAMTUMBO
Utangulizi
Kulingana
na shughuli za utafutaji madini zilizofanywa miaka ya nyuma hadi sasa
zimebainisha madini ya urani kuwepo katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.
Maeneo hayo ni pamoja na Mto Mkuju (Namtumbo); Madaba (Liwale); Bahi (Dodoma);
Gallapo (Babati); Milima ya Uluguru (Morogoro); na Itigi (Manyoni). Madini hayo
yanaweza kugundulika katika maeneo zaidi kutokana na shughuli za utafutaji zinazofanywa
pamoja na taarifa zaidi za kijiolojia zinazoendelea kutayarishwa na Wakala wa
Jiolojia Tanzania.
Hata hivyo, hadi sasa eneo la Mto Mkuju ndilo limeonekana
kuwa na mashapo ya madini ya urani yanayoweza kuchimbwa kibiashara. Pamoja na
matokeo ya awali kuonesha kuwa yapo madini ya urani yanayoweza kuchimbwa
kibiashara bado utafutaji zaidi unahitajika ili kupata mashapo zaidi yatakayoweza
kuchimba kwa muda mrefu.
Mradi wa Urani wa Mto Mkuju
Kulingana
na
utafiti wa kina wa madini ya urani uliofanywa katika eneo la mradi huu
umegundua mashapo yanayoweza kuchimbwa kibishara. Hadi sasa kiasi cha
tani milioni 175.8 za mashapo (Measured, Indicated na Inferred) ya
urani kimegunduliwa. Kiasi hicho ni sawa na pound milioni 115.8 (kilo
milioni 52.5) za urani kwa grade ya 298.8 U3O8ppm. Kulingana na mashapo haya uhai
wa mgodi kwa sasa ni miaka 12.
Mradi
wa Mto Mkuju unamilikiwa na Kampuni ya Mantra Tanzania Limited, Kampuni tanzu
ya URMZ ya Urusi. Kampuni ya URMZ ni Kampuni ya Serikali ya urusi. Mradi wa Mto
Mkuju uko ndani ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Selous (Selous Game Reserve). Pia eneo
hilo ni Sehemu ya Urithi wa Dunia (World Heritage Site). Mwezi Julai, 2012, World Heritage Committee iliyoko chini ya
UNESCO ilitoa idhini ya kuondoa eneo la Mradi wa Mto Mkuju kwenye Eneo la
Urithi wa Dunia ili uchimbaji wa urani uweze kufanyika. Hata hivyo, eneo hilo litaendelea
kuwa ndani ya eneo la Hifadhi ya Wanyamapori la Selous.
Kutokana
na hatua hiyo, uchambuzi wa masuala ya mazingira ulikamilika mwezi Oktoba, 2012
ambapo Hati ya Mazingira (Environmental Impact Assessment Certificate) ilitolewa
na Baraza la mazingira la Taifa (NEMC). Baada ya hatua hizo kukamilika, Wizara
ya Nishati na Madini ilitoa leseni ya uchimbaji madini ya urani tarehe 05
Aprili, 2013. Leseni hiyo inaruhusu shughuli za uchimbaji kufanyika katika
mradi huo. Majadiliano kuhusu mkataba wa kuendeleza uchimbaji madini kuhusu
mradi huo yanaendelea.
Uchimbaji
wa madini ya urani katika mradi wa Mto Mkuju utafanyika hadi hatua ya yellow cake. Baada ya hapo urani hiyo
itasafirishwa kwenda nje ya nchi katika maeneo ambayo urutubishaji wa madini
hayo kwa matumizi mbalimbali kama vile kuzalisha umeme, kutengeneza vifaa
vinavyotumika kwenye sekta za Afya, Kilimo, Ujenzi na Mifugo utafanyika.
Manufaa
mbalimbali yanatarajiwa kutokana na uchimbaji wa urani katika mradi huo ikiwa
ni pamoja na mrabaha (Dola za marekani
zaidi ya milioni 190); Kodi (Dola za
Marekani zaidi ya milioni 363); PAYE (Dola
za marekani zaidi ya milioni 50). Mapato mengine ni pamoja na Kodi ya zuio
(Withholding taxes), gawio (dividend), Import duties, Service levy kwenye
Halmashauri ya Namtumbo, n.k. Hata
hivyo, mapato haya yatatokana na hali ya bei ya urani katika soko la dunia. Manufaa
mengine ni ajira kwa watanzania zaidi ya 690.
Udhibiti wa shughuli za urani
Tungependa
kuwahakikishia Watanzania na wananchi wanaoishi karibu na maeneo
yaliyogundulika kuwepo na madini ya urani kwa kiwango cha kuchimbwa kibiashara,
kwamba Serikali imechukua hatua kadhaa za kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya
shughuli za utafutaji, uchimbaji na usafirishaji nje ya nchi madini ya urani.
Hatua hizo ni pamoja na zifuatazo:-
- Kuwepo kwa Sheria za Madini, 2010 ambapo madini ya urani na madini mengine yanayotumika kuzalisha nishati, mfano makaa ya mawe yanatambuliwa kama kundi pekee la energy minerals. Tofauti na madini mengine, sheria imezuia utoaji wa leseni ya biashara ya madini (Dealer Licences) kwa madini ya urani kutokana na unyeti wa madini hayo.
- Kuwepo kwa Kanuni maalum za the Mining (Radioactive Minerals) Regulations, 2010 zimetungwa (GN. 407 dated 22/10/2010) kuhakikisha kuwa kampuni zinazowekeza katika utafutaji na uchimbaji wa madini ya urani zinafuata maelekezo maalum yanayohusu utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji, usafirishaji na uuzaji wa madini hayo. Vilevile, Kanuni hizo zinaelezea majukumu ya mamlaka mbalimbali ikiwa ni pamoja na taasisi za TAEC na NEMC, na Wizara zinazosimamia rasilimali za Maji na Madini. Madhumuni makuu ni kuhakikisha kuwa shughuli hizo haziathiri usalama, afya na mazingira yetu na uhusiano wetu na jumuia za kimataifa, ikiwa ni pamoja na IAEA.
- Kuwepo kwa Sheria na kanuni chini ya Tanzania Atomic Energy Commission (TAEC) ambazo zinahakikisha kuwa kunakuwepo na uthibiti wa viwango vya mionzi ambavyo vinaweza kuathiri binadamu. Aidha, watahakikisha kuwa ufungaji katika mapipa na usafirishaji wa urani unafanyika kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vinavyokubalika.
- Kanuni za Usalama, Afya na Mazingira Migodini zilizotungwa kwa GN Na. 408 ya tarehe 22/10/2010 zimehifadhi kanuni namba 187 – 190 zilizokuwa kwenye kanuni za mwaka 1999 zinazokusudia kusimamia usalama wa shughuli za utafutaji wa madini ya urani na mengineyo yenye mionzi ayonisha. Kanuni hizo zimeweka mfumo wa kushirikisha jamii inayozunguka maeneo yanayofanyiwa utafiti wa madini hayo.
No comments:
Post a Comment