Header Ads

KUB Freeman Mbowe Vs NS Job Ndugai: Kushindwa kwa Uongo baada ya kweli kufahamika!

Imeandikwa na Dkt. Hamisi Kigwangalla, MB

Leo nimeamka na mzuka wa kuandika. Kwanza nasukumwa na kuandika kuhusu ukweli, zaidi kwa kuwa nafurahia kuandika maneno yanayofanana na yale yaliyosemwa na mwandishi nguli wa Kiswahili, babu yangu Shaaban Robert, ambaye kazi zake hazitokuja kufubaa vizazi na vizazi, nikizifananisha na zile za William Shakespeare, mwandishi mashuhuri wa mashairi na fasihi simulizi wa Uingereza ya karne ya 16. 

Lakini pia nafurahi kuandika kuhusu dhana ya ukweli ambayo mimi daima naisimamia na nitaifia itapobidi. Hayati Shaaban Robert anaandika hivi katika kitabu chake cha Kusadikika: ‘Msema kweli huchukiwa na marafiki zake. Nikipatwa na ajali kama hiyo, sitaona wivu juu ya wale wawezao kudumu na marafiki zao siku zote. Siwezi kuikana kweli kwa kuchelea upweke wa kitambo, nikajitenga na furaha ya milele itakayotokea pale uongo utakaposhindwa.’

Nimeazima hekima hizi kutoka kwa Shaaban Robert kwa lengo la kutaka kuzungumza ukweli, maana ukweli una tabia nyingi sana na kubwa niipendayo mimi ni ile ya kutobadilika badilika. Ukweli hubaki ukweli hata kama utaishi miaka dahari, utabaki kuwa kweli tu. 

Nimependa leo kujadili jambo hili kwa sababu kwanza lilileta aibu kubwa kwa bunge letu, pili mijadala iliyofuatia baada ya jambo hili ilileta taswira ya kuonewa na kukandamizwa kwa upinzani kwa kuzibwa mdomo, na tatu kwa kuwa iliongeza nguvu kwa wapinzani bungeni kudumu katika kususia kushiriki mjadala wa hoja ya muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba iliyokuwa ikijadiliwa. Yote haya naona yanapelekea kutuondoa kwenye mtindo wa ‘muafaka’ wa pamoja kwenye mchakato wa kuandika upya katiba yetu tuliokuwa tukiendelea nao.  

Nitaomba nitumie kanuni za bunge kujenga hoja yangu. Nianze na ile kanuni ya 60 (1.) ambayo inatoa maelekezo ni wakati gani mbunge atapata muda wa kusema bungeni, inasema: ‘ Mbunge akitaka kusema bungeni anaweza:- (a) kumpelekea spika ombi la maandishi; (b) kusimama kimya mahali pake; na (c) kutumbukiza kadi ya elektroniki.’ Mhe. Mbowe aliposimama bungeni alitumia kanuni hii kwenye ile fasili ndogo ya (b). 

Lakini ukisoma kanuni hiyo hiyo ya 60 ile fasili ya pili inasema ‘isipokuwa kwamba, Mbunge yeyote hataanza kuzungumza hadi aitwe na spika ama kwa jina ama kwa wadhifa wake na kumruhusu kusema…’ Hivyo Mhe. Ndugai (NS) alimuona Mhe. Mbowe lakini hakumruhusu kusema, na kwa mujibu wa kanuni hii alikuwa kwenye mamlaka ya kuamua aidha kumruhusu ama kutomruhusu.

No comments:

Powered by Blogger.