Header Ads

KILICHOJIRI KATIKA OPERESHENI KIMBUNGA AWAMU YA PILI, MAJANGILI NA MAJAMBAZI YAKAMATWA

KINACHOJIRI KATIKA OPERESHENI KIMBUNGA AWAMU YA PILI, MAJANGILI NA MAJAMBAZI YAKAMATWA WAKIWEMO WACHUUZI WA SMG KUTOKA BURUNDI, NG’OMBE ZATAIFISHWA, WAHAMIAJI HARAMU 425 WAMEKAMATWA WAKIWEMO WANAOWAHIFADHI.

Mahakama ya Wilaya ya Biharamulo imetoa hukumu ya kutaifisha Ng’ombe 103 mali ya Bw. Kalemela George kwa kosa la kuingiza mifugo hiyo katika hifadhi ya taifa ya Biharamulo. Naibu Kamishna wa Polisi nchini Kamanda Simon Sirro amewaambia waandishi wa Habari mjini Bukoba leo Jumatano Oktoba 2,2013 kuwa adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa kifungu namba 111 cha sheria ya wanayama pori na uhifadhi ya mwaka 2009.

Ng’ombe hao walikamatwa wakati Operesheni Kimbunga awamu ya Pili inaendelea katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita ambapo jumla ya Ng’ombe 2,220 walikamatwa kwenye hifadhi ya Taifa kwa kipindi cha siku 10 tangu kuanza kwa awamu hii ya operesheni Septemba 21, 2013.

Kwa mujibu wa Kamanda Sirro, jumla ya watuhumiwa 88 wa unyang’anyi wa kutumia silaha pamoja na silaha 23 zikiwemo Bomu la kurushwa kwa mkono Moja, bunduki aina ya SMG 3, Pisto 2, Magobole18 na Risasi 484 miongoni mwake zipo risasi za SMG/SAR 471 na risasi za Pisto 13, magazine za SMG 2 na Sare za Jeshi la Burundi zimekamatwa katika kipindi cha siku 10 za operesheni Kimbunga Awamu ya Pili.

Akifafanua, Kamanda Sirro amesema watuhumiwa wawili wa ujambazi wa kutumia silaha wamekiri kufanya uchuuzi wa kununua silaha nchini Burundi hususan silaha za Kivita za SMG na kuziuza nchini kwa Majambazi wa kutumia Silaha.

Kamanda Sirro amesema mtu huyo bila kumtaja jina ameiambia polisi kuwa awali alikuwa mfanyabiashara ya Mbuzi kutokea Tanzania kwenda Burundi ndipo alipogundua biashara yake hiyo hailipi na kuamua kujiingiza kwenye biashara ya kununua Bunduki aina ya SMG kwa shilingi 500,000/= kutoka Burundi na kuja kuziuza Tanzania kwa zaidi ya shilingi milioni moja.

“Mtu huyu amekiri kuuza silaha nyingi nchini ambazo amekuwa akiziingiza kutoka nchini Burundi. Serikali itazungumza na Serikaliya Burundi kuona namna ya kudhibiti tatizo hilo nchini Burundi ambapo silaha za SMG zisizotakiwa kumilikiwa na Raia isipokuwa Jeshi pekee zinapatikana kirahisi,” alisema Kamanda Sirro.

Aidha, Majangili 11 wamekamatwa pamoja na meno ya Kiboko na Ngozi ya Mbwea.  Jumla ya Makokoro 12, Bangi kilo Tatu, Gongo Lita271 na Magunia ya Mkaa 100 yaliyotengenezwa kwa mazao ya misitu kinyume na Sheria vimekamatwa katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita.

Wakati huo huo, Kamanda Sirro amesema katika kipindi cha Operesheni Kimbunga Awamu ya Pili jumla ya Wahamiaji Haramu 425 walikamata wakiwemo watu 5 wanao tuhumiwa kwa kosa la kuwahifadhi na kuwatorosha wahamiaji haramu. Miongoni mwa wahamiaji haramu waliokamatwa ni Warundi 180, Wanyarwanda 149, Waganda 82 na Wakongo 14. Mkoa ambao unaongoza kwa kukamata wahamiaji haramu wengi ni Kagera (209), Kigoma (166) na Geita (50).

Kamanda Sirro amesema operesheni Kimbunga inaendeleza na kuwaomba wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali kuwabaini wahalifu. “Ulinzi na Usalama wa nchi hii ni wetu wote, tu shirikiane kubaini, kuzuia na kupambana na uhalifu na hasa ujambazi, ujangili, uhamiaji haramu pamoja na haribifu wa mazingira” amesisitiza kamanda Sirro. 

Amesema Operesheni Kimbunga inaendelea kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi pamoja na kufuata Haki za Binaadam. Wanaoshughulikiwa kwa kukamatwa na kuhojiwa ni watu wote wanaotiliwa shaka na wanaobainika wanachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kurudishwa nchini kwao.

  “ Katika utekelezaji wa operesheni hi mwananchi mwenye taarifa aonyeshe dhamira ya kijasiri, kizalendo na mshikamano wa kitaifa katika kusaidia vyombo vya dola kwa kutoa taarifa ili kukabili wahalifu na uhalifu nchini” alisisitiza Kamanda Sirro.


Taari fa hii imeandaliwa na kusambaza na Timu ya Habari na Mawasiliano ya Operesheni Kimbunga, Bukoba, Oktoba2, 2013.

No comments:

Powered by Blogger.