JK AFUNGUA MKUTANO MKUU WA MWAKA WA MAAFISA WAANDAMIZI WA JESHI LA POLISI LEO MJINI MOSHI
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwasili Chuo cha Polisi mjini Moshi leo
Machi 6, 2012 tayari kwa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa
Waandamizi wa Jeshi la Polisi. Kulia kwake ni Waziri wa Mambo ya Ndani
Mh Shamsi Vuai Nahodha na kushoto kwake ni Inspekta Jenerali wa Polisi
Saidi Mwema. (PICHA NA IKULU)
Rais
Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu
wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi Chuo cha Polisi
mjini Moshi leo Machi 6, 2012
Rais Jakaya Kikwete akizindua mojawapo ya vitabu vya muongozi wa
Jeshi la Polisi wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa
Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi Chuo cha Polisi mjini Moshi leo
Machi 6, 2012 Kulia ni Waziri wa Mambo ya Ndani Mh Shamsi Vuai
Nahodha wa kulia Rais ni Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema
akifuatiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mh Leonidas Gama
Sehemu ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa
Jeshi la Polisi Chuo cha Polisi uliofunguliwa na Rais Jakaya Mrisho
Kikwete mjini Moshi leo Machi 6, 2012
HOTUBA
YA MHESHIMIWA DKT JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO
WA TANZANIA, WAKATI WA KUFUNGUA MKUTANO MKUU WA MWAKA WA MAAFISA
WAANDAMIZI WA JESHI LA POLISI, CHUO CHA POLISI MOSHI, TAREHE 06 MACHI
2012
-
Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi;
Inspekta Generali wa Polisi, Said Ally Mwema;
Mheshimiwa Leonidas Gama, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro;
Makamishna na Manaibu Makamishna wa Jeshi la Polisi;
Maofisa Wakuu wa Jeshi la Polisi;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Nakushukuru
sana wewe Mheshimiwa Waziri pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini
kwa kunialika kuja kufungua Mkutano wenu. Nakupongeza kwa dhati Mkuu wa
Jeshi la Polisi na viongozi wenzako kwa kuwa na utaratibu wa kukutana
kila mwaka kufanya tathmini ya shughuli zenu. Huu ni utaratibu mzuri
kwa vile kila Kamanda kwa ngazi yake anatoa taarifa ya utekelezaji wa
majukumu yake kwa mujibu wa sera, mikakati na mipango mbalimbali ihusuyo
usalama wa raia na mali zao katika eneo lake la uongozi.
Nathubutu
kusema kuwa msingeweza kuwa na utaratibu mwingine mzuri kushinda huu.
Matumaini yangu ni kuwa taarifa hizo zinafanya uchambuzi wa kina wa
mafanikio yaliyopatikana, kasoro zilizojitokeza na changamoto
mlizokabiliana nazo na mnazoendelea kukabiliana nazo. Aidha, ni
matumaini yangu kuwa mjadala unakuwa wa uwazi na ukweli na kwamba
hamtaoneana muhali kuambiana ukweli kuhusu kasoro za mwenzenu pale
inapostahili. Ni jambo jema na la kijasiri kujiwekea utaratibu wa
kujipima wenyewe.
Mheshimiwa Waziri,
Ndugu Mkuu wa Jeshi la Polisi;
Nimefurahishwa sana na Kauli Mbiu ya mkutano wenu “Usingoje, tumia rasilimali ulizonazo kuongeza ufanisi”. Ni Kauli Mbiu muafaka inayohimiza
uwajibikaji na ufanisi wa kazi kwa kuzingatia rasilimali zilizopo.
Inatambua hali halisi kwamba utegemee ulichonacho kutimiza majukumu
yako. Usisubiri usichokuwa nacho. Usisubiri ulichoomba au ulichoahidiwa
kupata. Nawaomba mkitoka hapa mwende kwenye vituo vyenu vya kazi mkiwa
mmebeba ujumbe huu mzito wa Kauli Mbiu. Mwende mkatekeleze maudhui yake
kwa vitendo, kwa kushirikiana na maofisa, wakaguzi na askari wa vyeo
mbalimbali.
Mkifanya
hivi, bila shaka mtaweza kukidhi matarajio ya wananchi na hivyo
kulinda heshima ya Jeshi letu la Polisi.Ni ukweli ulio wazi kuwa sote
tungetamani muwe na zana na vitendea kazi vilivyo bora, vingi vya
kutosheleza mahitaji yetu. Lakini uwezo wa kifedha uliopo ni mdogo,
vitu hivyo unavyovitaka hutavipata vyote kwa wakati mmoj. Hivyo basi
hamna budi kuwa na subira, kupanga vipaumbele vyenu vizuri na hasa kuwa
wabunifu ili kwa kutumia vifaa vilivyopo vizuri muweze kutekeleza
majukumu yenu kwa kiwango cha kuridhisha.
Mheshimiwa Waziri;
Ndugu IGP,
Maafisa na Askari,
Nataka
kuwahakikishia kuwa mimi na viongozi wenzangu Serikalini tunatambua
umuhimu wa kuendelea kuliongezea Jeshi la Polisi uwezo wa kibajeti ili
liweze kutimiza kwa ufanisi zaidi majukumu yake. IGP ni shahidi kwa
kiasi gani tumeendelea kuongeza bajeti ya Jeshi la Polisi mwaka hadi
mwaka.
Kwa mfano, mwaka 2005 Bajeti ilikuwa Shilingi 69 bilioni na mwaka huu wa fedha zimetengwa Shilingi 134 bilioni.
Nawaahidi kuwa tutaendelea kuongeza fedha kila mwaka katika miaka
ijayo. Pia tumetumia uhusiano wetu na nchi rafiki kuomba misaada
inayoendelea kuimarisha Jeshi letu kwa zana, mafunzo na weledi.
Napenda
kutumia nafasi hii kuwapongeza Maofisa, Wakaguzi na askari wote kwa
kazi kubwa na nzuri muifanyayo katika kulinda maisha na mali za raia.
Nawapongeza kwa uchapakazi wenu na moyo wenu wa kujitolea na kujituma.
Hakika maudhui ya Kauli Mbiu yenu ya mwaka huu mmekuwa mnayatekeleza
kwa vitendo. Matokeo ya jitihada zenu yanaonekana. Mafanikio ya kutia
moyo yanazidi kupatikana na sote tunayashuhudia.
Mwenye
macho haambiwi tazama. Uhalifu (hususan wa kutumia nguvu) unaendelea
kupungua nchini kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma. Kulingana na takwimu
za mwaka wa jana makosa makubwa ya jinai yalipungua kutoka 94,390 mwaka
2010 hadi 76,052 mwaka 2011.
Haya
ni mafanikio ya kutia moyo, lakini hamna budi mtambue kuwa bado idadi
ya makosa 76,052 ni kubwa mno. Hivyo bado mnayo na tunayo kazi kubwa
ya kufanya mbele yenu na yetu. Inatupasa tuongeze juhudi maradufu au
hata zaidi ili tupunguze kabisa uhalifu nchini.
Ndugu Makamanda,
Maofisa Waandamizi wa Polisi;
Mheshimiwa
Waziri na Inspekta Generali wamezieleza vizuri changamoto
zinazolikabili Jeshi la Polisi na mimi sina haja ya kuzirudia. Napenda
kutumia nafasi hii kurudia kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea
kusaidiana nanyi kwa kuwawezesha ili muweze kuzikabili changamoto hizo
kwa mafanikio. Tumefanya hivyo miaka iliyopita, tunafanya hivyo hivi
sasa na tutafanya hivyo miaka ijayo.
Tutaendelea
kuliwezesha Jeshi la Polisi kifedha ili muweze kutekeleza ipasavyo
majukumu yenu. Tutaendelea kuwawezesha muongeze idadi ya askari.
Tutawawezesha
mpate vyombo vya usafiri, zana na vitendea kazi vya kisasa vya
kufanyia kazi za kukabiliana na uhalifu. Kazi ya kulipatia Jeshi la
Polisi zana na vifaa vipya vya kazi inaendelea ikiwa ni sehemu ya
Programu ya Maboresho ya Jeshi la Polisi. Nawahakikishia kuwa
tutaendelea kutoa fedha za kutekeleza Programu hiyo na shughuli
nyingine za Jeshi la Polisi. Tutaendelea kuwawezesha katika kuboresha
mafunzo ya askari na maafisa wa Jeshi la Polisi. Natambua mahitaji ya
kuviboresha vyuo vilivyopo sasa.
Panapohitaji
kukarabati pakarabatiwe na panapotakiwa ujenzi wa majengo mapya
yajengwe. Na panapotakiwa kuanzishwa chuo kipya kianzishwe. Hatuna budi
kuwekeza katika mafunzo kwani mafunzo ni msingi mzuri wa weledi na
kuwa na askari wenye tabia na mwenendo mwema. Kupata zana za kisasa za
upelelezi na kudhibiti uhalifu pekee hazitoshi kama zitakuwa mikononi
mwa askari asiyejua kitu, asiyekuwa na nidhamu na utiifu.
Kufanya
hivyo kunalihakikishia Jeshi uwezo wa kutimiza majukumu yake kwa
ufanisi mkubwa na kuleta sifa kwa Jeshi la Polisi Tanzania. Dunia
imebadilika, Tanzania imebadilika na mbinu za uhalifu na aina za uhalifu
yamebadilika. Pia, mbinu, mikakati na maarifa ya kukabiliana na
uhalifu, nayo yamebadilika duniani. Lazima tusisitize mafunzo, kwani
ndiyo msingi wa weledi na ufanisi. Mafunzo ndiyo njia ya kuwawezesha
askari na maofisa wa Jeshi la Polisi kupata elimu na maarifa mapya
kuhusu uhalifu na namna ya kukabiliana nao. Mafunzo ndiyo
yatakayowezesha kuelewa zana na vifaa vipya vya kupambana na uhalifu na
kujua namna ya kuvitumia. Hakuna badala ya mafunzo.
Mheshimiwa Waziri,
Ndugu Inspekta Jenerali,
Maofisa,
Wakaguzi na Askari;
Mimi
na wenzangu katika Serikali tunatambua umuhimu wa kuboresha maslahi ya
maofisa na askari wa Jeshi la Polisi pamoja na kuboresha mazingira ya
kufanyia kazi na kuishi. Mara baada ya kuchaguliwa mwaka 2005,
nilipotembelea Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na baadhi ya kambi
nilijifunza mengi kuhusu hali ya maslahi na mazingira ya kazi na malazi
ya wanajeshi wetu. Baada ya hapo tulianza kuyachukulia hatua mambo
hayo na tumekuwa tunaendelea kufanya hivyo hadi sasa. Tumeboresha
maslahi kwa kiasi chake na bado tunaendelea. Tumeanza ujenzi wa nyumba
bora za kuishi na bado tunaendelea na mpango huo.
Napenda
kurudia kuwahakikishia kuwa kwangu na wenzangu Serikalini, hakuna
upungufu wa dhamira ya kuboresha na kuimarisha Jeshi la Polisi nchini
kwa maana ya idadi, mafunzo, vitendea kazi, maslahi na mazingira ya
kuishi. Kinachotutatiza ni uwezo wa kifedha wa Serikali ambao si mkubwa
sana kuweza kumudu sawia mahitaji yote ya kugharamia shughuli zote za
Serikali na Taifa. Pamoja na changamoto hizo, bado tumeendela
kuthubutu kuchukua hatua na kwa haya tuliyoweza kufanya kwa upande wa
Jeshi la Polisi si haba. Tunaendelea.
Mheshimiwa Waziri,
Ndugu IGP;
Sina
budi kuelezea furaha yangu na pongezi za dhati kwako IGP, Makamishna
walioko Makao Makuu ya Polisi pamoja na Makamanda wa ngazi mbalimbali
kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana kutokana na rasilimali iliyopo. Huu
ni uthibitisho wa uongozi wako makini ukishirikiana na viongozi wa
ngazi mbalimbali wa Jeshi letu. Hakika Kauli Mbiu ya mwaka huu kwenu si
jambo geni hivyo tunategemea kuona mafanikio makubwa zaidi miaka ijayo.
Aidha, mnanipa moyo kuwa hapo rasilimali zitakapoongezeka Jeshi la
Polisi litastawi sana.
Usalama Barabarani
Mheshimiwa Waziri,
Inspekta Generali wa Polisi,
Ndugu Makamanda;
Napenda
kutumia nafasi hii kurudia maombi yangu kwenu kuimarisha usimamizi wa
usalama barabarani. Ajali za barabarani zimezidi mno, hatuna budi
kuzizuia zisizidi kuongezeka. Tufanye kila tuwezalo zipungue. Nawaomba
mtumie fursa ya mkutano wenu huu kujadili tatizo hili kwa marefu na
mapana yake na mkubaliane juu ya nini cha kufanya. Naamini mtaweza.
Nawaomba
jambo hili mlipe uzito unaostahili kabla halijageuka kuwa janga la
kitaifa. Ukweli kwamba katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka
juzi (2010) jumla ya watu 3,687 walipoteza maisha kutokana na ajali za
barabarani. Mwaka na jana (2011) katika kipindi hicho hicho idadi hiyo
iliongezeka na kufikia watu 4,013. Hili si ongezeko dogo inatulazimu
kushtuka na kuchukua hatua. Nafahamu dhana ya kuwianisha kuongezeka kwa
ajali na kuongezeka kwa pikipiki na magari na hali ya barabara zetu.
Hata hivyo hivi visiwe visingizio vya kuona kuongezeka kwa ajali za
barabarani ni jambo la kawaida.
Tuseme
ukweli kuwa ajali nyingi zinasababishwa na uzembe wa madereva
kutokuheshimu Sheria ya Usalama Barabarani na ubovu wa vyombo vya
usafiri. Kwa sababu zote hizi mbili Jeshi la Polisi lina wajibu maalum
kukabiliana nazo. Tafadhali timizeni ipasavyo wajibu wenu. Mkajipange
vizuri, kwa kushirikiana na Idara nyingine husika za Serikali, ili
ajali na vifo viweze kupungua.
Madereva
wazembe, walevi na wasiotaka kufuata Sheria na Kanuni za usalama
barabarani wachukuliwe hatua kali. Wakati umefika madereva wakaidi
wanyang’anywe leseni zao ili wasihatarishe tena maisha ya Watanzania.
Najua haiwezekani kukomesha kabisa ajali za barabarani, lakini naamini
kuzipunguza inawezekana. Endapo kuna msaada mnahitaji au jambo mnataka
kutoka kwetu, tuambieni. Kama mnadhani Sheria ya Usalama Barabarani na
Kanuni zake zinahitaji marekebisho, tuleteeni mapendekezo yenu
tuyafanyie kazi. Au kama mnaona kuna mapungufu katika mfumo wa
kitaasisi uliopo, msisite kutushauri na sisi tutaangalia namna ya
kurekebisha.
Mheshimiwa Waziri,
Ndugu IGP,
Makamanda, Maafisa na Askari,
Jambo lingine ninalopenda mlizungumze kwa kina na mkubaliane katika
Jeshi letu ni juu ya hatua za kuchukua dhidi ya tuhuma za kuenea kwa
vitendo vya rushwa katika Jeshi la Polisi. Najua mnajitahidi lakini bado
ni hisia ya muda mrefu ya wananchi na haionekani kubadilika. Utafiti
unaofanywa na taasisi zinazojihusisha na masuala ya utawala bora kuhusu
rushwa bado zinalinyooshea kidole chombo chetu hiki muhimu sana cha
dola. Natamani sana hisia na taarifa hizo ingekuwa hazina chembe ya
ukweli lakini, bahati mbaya huo ndio mtazamo wa jamii na inaelezea
wakati mwingine kwa nini baadhi ya wananchi huchukua sheria mikononi
mwao.
Pamoja
na kuwepo kwa hisia hizo mimi naamini wapo Polisi wengi wazuri na
kwamba hali haijafikia kusema imeshindikana kupambana na kukomesha
vitendo vya rushwa katika Jeshi la Polisi. Penye nia pana njia.
Tafadhali sana tieni nia ya dhati kupambana na tatizo hili na
kushinda. Watambueni wale wenzenu miongoni mwenu wenye tabia ya kuomba
kitu kidogo muwawajibishe ipasavyo kwa adhabu zinazostahili. Hawa ni
watu wanaosaidia wahalifu wasibanwe na mkono wa sheria hivyo ni kikwazo
kwa Jeshi la Polisi kutimiza ipasavyo wajibu wake wa msingi wa
kupambana na uhalifu. Waondoeni katika Jeshi kwani wanaharibu sifa yenu
nzuri na kudhoofisha Chombo chetu.
Mheshimiwa Waziri,
Ndugu IGP,
Ndugu Makamishna,
Maofisa Waandamizi wa Polisi;
Mabibi na Mabwana;
Yamekuwapo
malalamiko mengi ya ukiukwaji wa haki za binadamu yanayoelekezwa kwa
Jeshi letu la Polisi katika utendaji kazi. Taarifa za kila mwaka
zinazotolewa na Tume ya Haki za Binadamu na taasisi nyingine mbalimbali
za Kitaifa na Kimataifa zimekuwa zikionesha hivyo. Yapo pia madai ya
watu kunyanyaswa na Polisi kwa kukamatwa bila makosa, kubambikiwa
makosa, kuteswa wakiwa mahabusu na hata kuuliwa. Kuna madai ya Polisi
kutumia nguvu kupita kiasi na hata kusababisha vifo ya raia.
Nawaomba
mtumie fursa ya mkutano huu myazungumze madai hayo na kuamua hatua
zipasazo za kuchukua. Natambua kuwa katika Programu ya Maboresho ya
Jeshi kuwaelimisha wanajeshi wetu kuhusu masuala ya haki za binadamu ni
moja ya mambo yaliyopewa kipaumbele. Nawaomba mtekeleze dhamira yenu
hii njema kwa kasi zaidi ili katika kipindi kifupi muwafikie Polisi
wetu wote. Aidha, mafunzo kuhusu haki za binadamu yawemo katika mitaala
ya vyuo vyetu hapa CCP, Police College - Kurasini na Chuo cha Maafisa
Wakuu Kidatu.
Aidha,
Jeshi liweke utaratibu mzuri na unaoeleweka wa kupokea na kufanyia
kazi malalamiko au maoni yanayopelekwa kwao na wananchi.
Ni
muhimu kwa Jeshi la Polisi kusisitiza na kusimamia kwa dhati nidhamu
ya maofisa na askari wake. Nidhamu ni sifa ya msingi ya askari. Askari
asiye na nidhamu amepoteza sifa ya kuendelea kuwa mwanajeshi. Ni hatari
sana kwa usalama wa raia na anaharibu sifa ya Jeshi. Vitendo vya utovu
wa nidhamu vinavyofanywa na baadhi ya maofisa na askari kamwe
visivumiliwe. Hivi majuzi nimesikia kuwa hapa Moshi askari ametoroka
lindo na kwenda disco, tena akiwa na silaha! Vitendo vya namna hii
vinaleta fedheha kwa Jeshi la Polisi na kuwaacha watu wakishangaa na
kuwa na maswali mengi juu ya Jeshi lao. Inawezekanaje ifikie hapo kwa
askari aliyefunzwa vizuri.
Nawaomba
mzingatie upya taratibu zenu za ajira. Wakati umefika wa kuwepo na
utaratibu mzuri wa upekuzi wa vijana kabla ya kuteuliwa kusomea kazi ya
Polisi. Pawepo na utaratibu thabiti na kufuatilia mienendo ya askari
wakati wote wa utumishi wao. Majeshi mengine yanafanya hivyo. Kufanya
hivyo kutasaidia kupata vijana walio safi kwa tabia na mwenendo
kuajiriwa na kuendelea na utumishi katika Jeshi la Polisi. Kwa ajili
hiyo tutakuwa na askari walio watiifu, waaminifu, wachapa kazi hodari na
kuliletea sifa Jeshi letu.
Mwisho
Mheshimiwa Waziri,
Inspekta Generali,
Makamanda wa Polisi;
Kabla
ya kumaliza hotuba yangu napenda kurudia kutoa pongezi za dhati kwa
kazi kubwa na nzuri muifanyayo pamoja na changamoto mbalimbali
mnazokabiliana nazo. Nawapongeza sana kwa kubuni utaratibu wa Polisi
Jamii ambao ni mfano mzuri wa ubunifu wa kutumia rasilimali zilizopo.
Tafadhali uimarisheni na kuuboresha utaratibu huu mzuri. Sisi katika
Serikali tutafanya kila linalowezekana kuongeza rasilimali kwa Jeshi la
Polisi ili kuliwezesha kukabiliana na uhalifu nchini. Nawaomba mkumbuke
na kuzingatia ukweli kwamba katika kila hatua mnayopiga, sisi
Serikalini na taifa zima kwa ujumla tutakuwa pamoja nanyi kuwapa moyo
na kuwaunga mkono kwa rasilimali muhimu.
Ndugu Inspekta Jenerali,
Makamanda wa Mikoa na Vikosi,
Mabibi na Mabwana,
Baada
ya kusema hayo, ninayo furaha sasa kutamka kwamba, Mkutano Mkuu wa
Mwaka 2012 wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi umefunguliwa rasmi.
Nawatakia mkutano mwema, mazungumzo yenye ufanisi na matokeo mazuri.
“Ahsanteni kwa kunisikiliza”
No comments:
Post a Comment