Header Ads

WAZIRI NCHIMBI ATEMBELEWA NA BALOZI WA IRANI NCHINI

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Emmanueli Nchimbi (kulia) akizungumza na Rais wa Kituo cha Utamaduni na Uhusiano wa Kiislam kutoka nchini Iran Dkt. Mohammed Basheir Khurrqmshad (kushoto)  mara baada ya kuwasili katika Ofisi za Wizara hiyo leo jijini Dar es salaam. Pamoja na mambo mengine Rais huyo ameahidi kuendeleza ushirikiano kati ya Tanzania na Iran katika sekta ya utamaduni na michezo ikiwemo kusaidia kuleta makocha wa mchezo wa riadha.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt Emmanueli Nchimbi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa serikali ya Iran waliomtembelea ofisini kwake leo jijini Dar es salaam.
Balozi wa Irani nchini Tanzania (katikati) Movahhedi Ghomi akimweleza jambo waziri wa Habari, Vijana,Utamaduni na Michezo Dkt. Emmanueli Nchimbi (kushoto) mara baada ya kumtembelea ofisini kwake leo jijini Dar es salaam. Kulia ni Rais wa Kituo cha Utamaduni na Uhusiano wa Kiislam cha  Iran Dkt. Mohammed Basheir Khurrqmshad.
 Picha na Aron Msigwa –MAELEZO.

Benjamin Sawe na Ismail Ngayonga

Kitengo cha Habari

WHVUM.

Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Dk. Emmanuel John Nchimbi ameishukuru  Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuanza utekelezaji wa kupatiwa kocha wa mchezo wa riadha ikiwa ni mkataba wa ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Dk. Nchimbi aliyasema hayo jana (leo) alipokutana na Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu wa Iran Dk.Mohammad Bagher Khurramshad jijini Dar es Salaam ambapo alisema hatua hiyo ni moja ya utekelezaji wa mkataba wa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Iran.

Alisema nchi ya Iran imekuwa ni moja kati ya nchi yenye makocha bora na wenye uzoefu katika mchezo wa riadha kwa miaka mingi na kusema ni wakati muafaka kuichangamkia ofa hiyo.

“Nchi ya Iran ina makocha bora wa mchezo wa mbio za riadha sasa ni wakati muafaka kwa Chama cha Mchezo wa Riadha kuichangamkia ofa hii ili mchezo huu uweze kuiweka nchi katika ramani ya michezo duniani’’.Alisema Dr. Nchimbi.

Kwa Upande wake Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu wa Iran Dk. Khurramshad alisema Iran itaendelea kuisaidia Tanzania katika sekta ya Michezo,Utamaduni na Sanaa ikiwa ni kuboresha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.

“Huu ni mwanzo tu wa makubaliano ya mkataba lakini tutaendelea kuisaidia Tanzania katika sekta za utamaduni na sanaa kama tulivyokubaliana katika mkataba baina yetu”.Alisema Dr.Khurramshad 

Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Kiislam ya Iran mwezi uliopita zilitiliana saini mkataba wa ushirikiano katika sekta za Utamaduni na Sanaa ambapo kwa upande wa Serikali ya Tanzania iliwakilishwa na Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Dr. Emmanuel Nchimbi na upande wa Jamhuri ya Kiislam ya Iran iliwakilishwa na  Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu Dk.Khurramshad.

Katika mkataba huo uliosainiwa Jijini Tehran moja kati ya makubaliano ni pamoja na ushirikiano katika sekta ya Utamaduni na Sanaa ambapo Serikali ya Tanzania iliombwa na ilikubali kuandaa Wiki ya Utamaduni wa Tanzania nchini Iran.

No comments:

Powered by Blogger.