KURA ZA MAONI MGOMBEA WA CCM ARUMERU MASHARIKI KURUDIWA
![]() |
| Nape akizungumza na waandishi leo, Dar es Salaam |
Katibu
wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye
amesema leo jijini Dar es Salaam, kwamba kikao hicho chini ya Mwenyekiti
wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kimeamua upigaji kura huo urudiwe kwa kuwa
katika matokeo ya upigaji kura uliopita, hakuna mgombea aliyepata
kura zinazovuka asilimia 50 ya kura zote.
Nape
alisema, watachuana kwenye marudio hayo ni wagombea wawili, Wiliam
Sarakikya na Sioi Solomon ambao waliwashinda wenzao wote katika kura za
maoni za awali.
Kulingana
na kumbukumbu ambazo mtandao huu unazo ni kwamba katika kura za maoni
zilizopita, Sioi aliongoza kwa kura 361 wakati Sarakikya aliyeshika
nafasi ya pili akipata kura 259 huku watatu Elishilia Kaaya akipata kura
176.
Nape
alisema uchaguzi huo wa kura za maoni utarudiwa Machi 1, 2012 yaani
Alhamisi wiki hii, na wapigakura ni wale wale wa Mkutano Mkuu wa jimbo
walioshiriki uchaguzi wa kura za maoni uliopita.
Alisema,
uchaguzi huo utasimamiwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Mzee Pius
Msekwa , Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara) Kapteni Mstaafu, John
Chiligati na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kagera, Costancia Buhiye.
Nape
alisema siku itakayofuata yaani Machi 2, 2012, (Ijumaa), Kamati ya
siasa ya wilaya itapitisha majina ya wagombea hao na baadaye siku hiyo
hiyo jioni kamati ya siasa ya mkoa itapitia mapendekezo ya wilaya
kabla Kamati Kuu kupitisha rasmi jina la mgombea Machi 3, 2012.
Akijibu
maswali ya waaandishi wa habari, Nape alisema, hatua hiyo ya Kamati
kuu ni ya utaratibu wa kawaida na haikuchukuliwa kwa dharura yoyote
lakini ni katika kutekeleza moja ya kanuni za uchaguzi ndani ya CCM na
umewahi kutumika.
Kwa
mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, uchaguzi mdogo jimbo la Arumeru
Mashariki utafanyika Aprili Mosi mwaka huu, baada ya vyama
vitakavyoshiriki kwenye uchaguzi huo kuchuana katika kampeni ambazo
kipyenga chake kitapulizwa rasmi Machi 9, mwaka huu.
Uchaguzi
huo unafanyika kufuatia jimbo hilo kubaki wazi baada ya aliyekuwa
mbunge wa jimbo hilo, Jeremiah Sumari kufariki dunia hivi karibuni.

No comments:
Post a Comment