Trilioni nane zatumika kuboresha umeme ndani ya miaka 10
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la ugavi la umeme nchini (TANESCO) Mhandisi Felchesmi Mramba akifafanua jambo wakati akizungumza na
waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
Na Beatrice Lyimo-Maelezo.
Zaidi ya Dola billioni
nne za Kimarekani ikiwa sawa na Trilioni nane kwa shilingi ya Kitanzania zimewekezwa
katika sekta ya umeme kwenye Miradi yote ya uzalishaji, usambazaji na
usafirishaji wa umeme nchini.
Hayo yamesemwa na
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la ugavi la umeme nchini (TANESCO) Mhandisi Felchesmi Mramba wakati akizungumza na
waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa katika
kipindi cha miaka 10 (2005-2015), Serikali imeongeza uwezo wa mitambo ya
kuzalisha umeme katika Gridi ya Taifa kutoka MW 891 hadi kufika MW 1,501.24
sawa na ongezeko la asilimia 68.5.
“Baadhi ya miradi
iliyokamilika ni pamojaj na mtambo wa
kuzalisha umeme MW 100 uliopo Ubungo, na Ujenzi wa mtambo wa kufua umeme MW
45 uliopo Tegeta jijini Dar es salaam.
Miradi mingine ni mtambo wa kuanzisha umeme MW 60 Mwanza, na mradi wa umeme wa
Somanga Fungu MW 7.5 Mkoani Lindi” amesema Mkurugenzi huyo.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mramba,
kukamilika kwa Miradi hiyo kumewezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini
na kufanikisha kuondoa mgawo wa umeme hususani kuanzia mwaka 2012 na hivyo
kuboresha ufanisi wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Mtendaji huyo Mkuu wa TANESCO
ameeleza kuwa kumekuwa na mikakati mbalimbali ya kuongeza uzalishaji wa umeme
kwenye Gridi ya Taifa na nje ya Gridi ya Taifa ikiwemo utekelezaji wa Mradi wa
Kinyerezi 1 (MW 150) kwa kutumia Gesi asilia, mradi wa kupeleka umeme katika miji
ya Mpanda, Ngara, na Biharamulo.
Aidha Mkurugenzi huyo ametoa
ufafanuzi kuhusu kubadilisha mfumo umeme wa LUKU utakaofanyika tarehe 1/8/2015.
“Zoezi la kubadilisha
mfumo wa LUKU litachukua muda wa saa 24 kuanzia usiku wa manane wa Agosti Mosi,
2015 hadi usiku wa manane wa tarehe 2/8/2015 sio siku saba kama ilivyoenezwa
katika mitandao ya kijamii,” amesema.
Lengo la zoezi hili ni
kuongeza kasi na kuwawezesha watu wengi kuunganishwa na mfumo mpya wa LUKU utakaohudumia
idadi kubwa zaidi ya watu tofauti na hali ilivyo sasa.

No comments:
Post a Comment