MAPATO YA NDANI YAIMARISHWE KUFANIKISHA MALENGO YA MILLENIA
Mkurugenzi
wa kupunguza umaskini kutoka Wizara ya Fedha, Ana Mwasha (kulia)
akifungua kongamano, linalojadili yaliyojiri katika Malengo ya Millenia
na nini kinastahili kufanywa katika SDG's ili kuhakikisha mafanikio
katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Uchumi na Utafiti wa Kijamii
nchini (ESRF). Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Uchumi na
Utafiti wa Kijamii nchini (ESRF) Dk.Oswald Mashindano na Katikati ni
Naibu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa
(UNDP)- Programme, Amon Manyama.(Picha na Zainul Mzige wa modewjiblog).
MKURUGENZI wa Kupunguza Umasikini kutoka Wizara ya Fedha, Anna Mwasha
amesema changamoto za uwezo wa kifedha kutekeleza miradi mbalimbali
iliyokuwa katika Malengo ya Milennia, zinatoa ishara tosha ya kubadili
mikakati ili kuwa na mafanikio katika Mipango ijayo ya Maendeleo
Endelevu (SDGs).Alitoa kauli hiyo jana wakati
akizungumza na washiriki wa kongamano, linalojadili yaliyojiri katika
Malengo ya Millenia na nini kinastahili kufanywa katika SDGs ili
kuhakikisha mafanikio.
Alisema ipo haja ya kuimarisha makusanyo ya fedha za ndani na kuacha
kutegemea wahisani, kwa kuwa moja ya sababu za kushindwa kutekelezwa kwa
Malengo ya Millenia ni ahadi za wahisani kutotekelezwa. Alisema
kipengele cha nane katika Malengo ya Millennia, kiligusia ushirikiano
wa kimataifa, ahadi ambazo amesema ukiachia nchi za Luxemburg, Denmark,
Sweden na Norway, mataifa mengi hayakutoa asilimia 0.7 ya pato lao la
ndani, ambalo lilikubalika kimataifa kusaidia Malengo ya Millennia kwa
nchi masikini.
Alisema
ili kuwepo na mafanikio katika miradi mipya na ile inayoendelezwa
kutoka MDGs, iko haja ya kuangalia jamii iliyopo vijijini, ambako
ndiko kwenye umasikini wa kutisha, ingawa Tanzania imefanya vyema
kuondokana na umasikini wa chakula. Umasikini wa chakula umepungua hadi asilimia 9 wakati Malengo ya Millenia yalikuwa ni asilimia 11. Alisema ipo haja ya kufungua mawasiliano ya vijijini, kuinua kilimo, kuwapatia nafasi ya masoko na kuinua huduma za jamii.
Pamoja
na kuzungumzia uwezo wa kifedha, alisisitiza haja ya wadau kuangalia
namna ya kushirikisha sekta binafsi katika kutafuta vyanzo vya fedha kwa
ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ili kukabili umasikini.
Naibu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa
(UNDP)- Programme, Amon Manyama akizungumza kwenye kongamano la siku
moja linalojadili yaliyojiri katika Malengo ya Millenia na nini
kinastahili kufanywa katika SDG's ili kuhakikisha mafanikio
lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Uchumi na Utafiti
wa Kijamii nchini (ESRF).
Sehemu ya washiriki wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa kwenye kongamano hilo.
No comments:
Post a Comment