ATCL yaongeza safari zake visiwa vya Comoro.
Abiria wakishuka kwenye Ndege ya Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL) aina ya CRJ 100. Picha ya Maktaba
SHIRIKA
la ndege la taifa (ATCL) limetangaza uamuzi wake wa kuongeza idadi ya
safari zake kuelekea visiwa vya Comoro hatua inayolenga kuendana na
ongezeko la mahitaji ya huduma za shirika hilo hususani katika kuelekea
kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Kwa
sasa shirika hilo linatoa huduma zake kwenye mikoa ya Dar es Salaam,
Kigoma na Mtwara kila siku. Sambamba na kutoa huduma hizo hapa nchini,
shirika hilo lina mpango mpya utakaoanza rasmi tarehe mosi ya mwezi Juni
mwaka huu kwa kuongeza safari zake kuelekea visiwa vya Comoro hadi
kufikia mara nane kwa wiki ikiwemo mara mbili siku za Alhamisi.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
wa ATCL Bw. Johnson Mfinanga alisema shirika hilo ndilo pekee linalotoa
huduma ya safari za anga kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro huku
akibainisha fursa za kibiashara zilizopo kati ya nchi hizi mbili jambo
linalosababisha uwepo wa ongezeko la mahitaji ya huduma za ATCL.
Pia
amewaasa watanzania hususan wakazi wa mtwara kuchangamkia fursa hizo
kwa kuwa shirika hilo kwa sasa linatoa huduma zake kati ya Mtwara na
visiwa vya Comoro kwa siku za Jumatano na Ijumaa kila wiki.
“Siku zote tumekuwa tukihakikisha kwamba tunabadilika kuendana na mahitaji ya wateja wetu.
Ni
dhahiri kwamba katika kipindi hiki kuna hitaji kubwa la usafiri wa anga
kuelekea visiwa vya Comoro kwa sababu za kibiashara, mapumziko na
sherehe mbalimbali, hivyo ATCL imejipanga kuchangamkia fursa hiyo,’’
alibainisha.
Akizungumzia
ufanisi wa shirika hilo katika safari nyingine ikiwemo zile za Kigoma
na Mtwara, Bw. Mfinanga alisema wamekuwa wakihudumia idadi kubwa ya
abiria kutokana na ndege za shirika hilo kusafiri kwa mwendo kasi wa
kuridhisha sambamba na huduma nzuri zinazotolewa kwa wateja wakati wa
safari.
“Zaidi
tunaamini kwamba huduma tunazozitoa kati ya Tanzania na Comoro zimekuwa
zikichangia kuongeza ushirikiano baina ya nchi hizi mbili na tunaamini
kuwa hata hili ongezeko la safari zetu kwenye mataifa haya mawili
zitatoa fursa kwa wateja wetu kufaidi fursa zinazopatikana ndani ya nchi
hizi,’’ aliongeza Bw. Mfinanga.
Kuhusu
mpango wa shirika hilo kujipanua zaidi kihuduma, Bw. Mfinanga alisema:
“Ndege yetu aina ya De-Havilland Dash 8 Q300 kwa sasa inafanyiwa
marekebisho makubwa kwenye karakana yetu iliyopo kwenye uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na itakapokamilika tutaendelea na
huduma zetu katika mikoa ya Mwanza, Tabora, Kilimanjaro na Mbeya,’’
Bw.
Mfinanga aliongeza kuwa kwa kufanya safari zake kuelekea visiwa hivyo
shirika hilo limekuwa likiwezesha wateja wake kunufaika na fursa
zilizopo kwenye visiwa hivyo huku pia akitoa wito kwa watanzania wengine
kujitokeza kushiriki katika kuchangamkia fursa hizo.
No comments:
Post a Comment