TANZANIA, KENYA, ZAMBIA WAANZA KUJADILI UTEKELEZAJI MRADI UMEME WA PAMOJA.
Katibu Mkuu Wizara ya
Nishati na Madini, Eliakim Maswi, akiongea wakati wa kikao cha Wataalamu kutoka
nchi za Zambia, Kenya na Tanzania Kujadili Utekelezaji wa Mradi wa Kuunganisha
Mtandao wa Umeme katika Gridi za nchi hizo. Wengine kutoka kushoto ni Balozi wa
Zambia nchini Judith Kapijimpanga, Katibu Mkuu Wizara ya Migodi, Nishati na Maendeleo ya Maji Zambia, Charity
Mwansa, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya
Nishati Petroli Kenya, Mhandisi Richard Mwiru na Katibu Mkuu
Msaidizi wa Jumuiya ya Soko la pamoja la nchi za Mashariki na Kusini mwa
Afrika anayeshughulikia miradi (COMESA), Dkt. Kipyego Cheluges.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu
Wizara ya Nishati Petroli Kenya,
Mhandisi Richard Mwiru (wa pili kulia) akiongea jambo wakati wa kikao hicho,
ambapo ameeleza utayari wa nchi ya Kenya katika utekelezaji wa mradi huo.
Sehemu ya Wataalamu kutoka
nchi za Zambia, Kenya na Tanzania wakifuatilia kikao cha Kujadili Utekelezaji wa Mradi wa Kuunganisha Mtandao wa Umeme
katika Gridi za nchi hizo.

Mtaalamu Mwelekezi kutoka
nchi ya Zambia Siyanga Zomba, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji na hatua
mbalimbali zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi wa kuunganisha Mtandao wa
Umeme katika Gridi kwa nchi za Zambia, Kenya na Tanzania.
Na
Asteria Muhozya, Dar es Salaam.
Wataalamu kutoka nchi za Zambia,
Kenya na Tanzania kutoka Wizara zinazoshughulika na masuala ya nishati wameanza
majadiliano ya Utekelezaji wa Mradi wa Kuunganisha Mtandao wa Umeme katika
Gridi za nchi hizo. Kikao cha Majadiliano hayo kiliongozwa na
Makatibu Wakuu kutoka katika nchi husika na kitafuatiwa na mkutano wa Mawaziri
utakaofanyika tarehe 30 Septemba, 2014 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao hicho Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi amezitaka nchi hizo kuunga
mkono jitihada za utekelezaji wa mradi huo kutokana na umuhimu wake kiuchumi
ikiwemo kuhakikisha nchi hizo zinakuwa na nishati ya umeme ya kutosha.
Aidha, ameongeza kuwa,
tayari Tanzania imeanza kufanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha inaanza
utekelezaji wa mradi huo ambao umechukua kipindi kirefu kuanza kutekelezwa na
kuongeza kuwa, Tanzania iko tayari kushiriki katika utekelezaji wa mradi huo
ikiwemo kuhakikisha kwamba mradi huo unafanikiwa.
Kwa upande wake mwakilishi
wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na
Petroli Kenya Mhandisi Richard Mwiru,
ameeleza kuwa, kuna matokeo bora yatakayotokana na utekelezaji wa mradi huo,
matokeo ambayo yatasaidia biashara ya umeme na upatikanaji wa umeme rahisi kwa nchi
hizo. Aidha, ameongeza kuwa, nchi ya Kenya iko tayari kushiriki katika
utekelezaji wa mradi huo.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya
Migodi,Nishati na Maendeleo ya Maji wa Zambia,
Charity Mwansa, ameeleza kuwa, anatarajia mkutano huo utatoa fursa
zitakazosaidia utekelezaji wa mradi huo kuendelea kutoka mahali ulipofikia ili
kuweza kutoa matokeo chanya yatakayokuwa na manufaa kwa nchi hizo ukizingatiwa kuwa, nchi hizo zimebahatika
kuwa na rasilimali asilia za kutosha.
Aidha, Katibu Mkuu
Msaidizi wa Jumuiya ya Soko la pamoja la nchi za Mashariki na Kusini mwa
Afrika anayeshughulikia miradi (COMESA), Dkt. Kipyego Cheluges amezitaka nchi
hizo kuhakikisha kwamba mradi huo unatekelezwa
kutokana na manufaa ambayo nchi hizo zitayapata ikiwemo bara la Afrika
na kuongeza kuwa, COMESA itashirikiana kwa karibu na nchi hizo kuhakikisha
kwamba, mradi unatekelezwa kama ulivyopangwa.
No comments:
Post a Comment