- Asema analipwa zaidi ya Sh milioni 380 kwa mwaka

NAIBU Katibu
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe,
ametaja mshahara anaolipwa Rais Jakaya Kikwete. Amesema kwamba kwa
wadhifa alionao, Rais Kikwete analipwa zaidi ya Sh milioni 30 kwa
mwezi. Mbali
na mshahara huo, Zitto amesema kiongozi huyo wa nchi, analipwa wastani
wa zaidi ya Sh milioni 380 kwa mwaka ambazo ni marupurupu pamoja na
mshahara wake.
Zitto aliutaja mshahara huo mjini hapa jana, alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara.
Kwa mujibu wa Zitto, hakuna sababu kwa mshahara wa kiongozi kufanywa
siri kwa kuwa kufanya hivyo ni kutowatendea haki wananchi wanaolipa kodi
inayolipa mishahara ya viongozi.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Mwenyekiti wa Kamati
ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ametaja mshahara huo ikiwa ni wiki
moja baada ya kutaja mshahara wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye
alisema analipwa zaidi ya Sh milioni 20 kwa mwezi pasipo kukatwa kodi
Akihutubia mamia ya wananchi katika mkutano huo, Zitto alisema hoja ya
msingi siyo kiasi wanacholipwa viongozi hao walioajiriwa na wananchi,
bali ni usiri unaofanywa juu ya kiwango hicho kinachotokana na walipa
kodi.
“Ni jambo la kusikitisha kuona mwalimu anayelipwa mshahara wa shilingi
laki mbili kwa mwezi ukikatwa kodi, huku viongozi wa kuchaguliwa wakiwa
wanapokea mishahara mikubwa pasipo kukatwa kodi licha ya kuhudumiwa kila
kitu na Serikali.
“Katiba ya sasa, ibara ya 43 (1), inaeleza kuwa, rais atalipwa mshahara
pamoja na malipo mengine, huku ibara hiyo hiyo kifungu cha pili kikizuia
mshahara na marupu rupu kupunguzwa.
“Kwa hiyo, ni muhimu sasa Katiba mpya ikabadilisha eneo hilo kwa manufaa
ya nchi kwani hata kesho Dk. Slaa (Katibu Mkuu wa Chadema), akiwa Rais
na akataka kupunguza mshahara wake, kwa Katiba hii hawezi.
“Hili jambo siyo sahihi, kwani viongozi wa ngazi hizi wanapata kila kitu
bure kutoka serikalini, lakini wanalipwa fedha nyingi,” alisema Zitto.
Akiwa katika Kata ya Choma, Zitto alikagua kilichokuwa Kiwanda cha
Kuchambulia Pamba cha Ginery, ambacho kwa sasa hakifanyi kazi tangu
mwaka 1998.
Alisema viwanda vingi vimekufa kwa sababu Serikali ya Rais mstaafu,
Benjamin Mkapa ilishindwa kutofautisha kati ya uwekezaji na biashara
huru.
“Ni Serikali ya Mkapa iliyotufikisha hapa, kwani wao walidhani biashara
huru ni kuwapa wawekezaji viwanda vyetu na Serikali kujiweka pembeni,
sasa nchi imebaki kutegemea uchumi wa uchuuzi badala ya uzalishaji,”
alisema.
Alisema sera ya uwekezaji katika Serikali ya CCM, ilichukuliwa kama
fursa ya viongozi wa chama hicho kujinufaisha na mali za Serikali bila
kujua wataiendeleza vipi.
Zitto alisema pia kwamba, kutokana na umakini wa Chadema, kila wakati
kimekuwa kikisisitiza namna ya kupiga marufuku usafirishaji wa pamba
kwenda nje ya nchi na badala yake viwanda vilivyopo nchini, vifufuliwe
kwa ajili ya kukuza uchumi na kutoa ajira kwa Watanzania.
Akizungumzia uimara wa Chadema, alisema huu ni wakati ambao Watanzania
wanahitaji vyama vya upinzani kuliko wakati mwingine wowote na kwamba
Chadema imekuwa sehemu ya matumaini hayo.
“Kutokana na matumaini ya Watanzania kwa Chadema, watu wanaotumia sababu
binafsi kutaka kuwagombanisha viongozi wa chama chetu watakuwa na
dhamira ya kufifisha matumaini ya Watanzania na wanapoteza muda.
“Wapo wanaosema Zitto kanunuliwa kuharibu upinzani nchini na wapo wanaosema hatuelewani ndani ya chama chetu.
“Naomba niwatoe hofu wananchi, sisi tupo imara na nakuhakikishieni
hatutayumba kwa hilo kwani tupo tayari kushika dola mwaka 2015,” alisema
Zitto na kushangiliwa.
Chanzo - Mtanzania
No comments:
Post a Comment