JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA
YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
Habari iliyotolewa Oktoba 26, mwaka huu na baadhi ya magazeti na mitandao
ya kijamii yenye kichwa cha habari ‘Msafara wa Waziri Nchimbi wapigwa mawe Songea’
si za kweli bali zimetengenezwa na walizituma kwa nia ya kupotosha jamii.
Oktoba 25, mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi na Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi alitembelea
Miradi ya Maendeleo pamoja na kufanya Mkutano aliianza katika Kata ya
Mletele na kumalizia Kata ya Matarawe, katika jimbo lake la Songea Mjini.
Wakati alipomaliza mkutano wake wa Mletele alitaarifiwa makundi ya watu
yamefunga njia katika daraja la Matarawe na wamesema hawatalifungua
mpaka Mhe Nchimbi akaliangalie na kuzungumza nao.
Mhe. Nchimbi alishauriwa kubadili njia ili kuwahi
mkutano wa hadhara wa Matarawe ambapo wananchi walikuwa wanamsubiri
kwa zaidi ya saa mbili. Pamoja na kushauriwa kupita njia nyingine, Mhe.
Nchimbi aliamua kwenda kuwasikiliza, alifika katika eneo la daraja akiwa
amefuatana na viongozi mbalimbali wa Manispaa na Serikali, mhe Nchimbi
aliwapa fursa wananchi hao kueleza kero zao, nao walimwambia kuwa eneo
hilo limekuwa na ajali mara kwa mara tokea barabara ya lami ilipokamilika
na kusababisha vifio vya watu karibu wanne hivyo walimuomba mbunge wao
awasaidie kumaliza kero hiyo.
Akijibu kero hiyo, Mhe. Nchimbi aliwaambia wananchi
wake kuwa ni yeye aliyefanikisha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango
cha lami atalishughukia tatizo hilo pia na kuwa amelichukua kwa uzito
mkubwa. Baada ya majibu ya mhe Nchimbi wananchi hao waliridhika na ndipo
wenyewe wakafungua barabara na kutoa vizuizi ili waziri na msafara wake
waweze kupita. Mhe Nchimbi na ujumbe wake waliendelea na safari na kwenda
kwenye mkutano wa hadahara takribani mita 200 toka daraja hilo. Saa
moja baada ya mhe Nchimbi kuwa ameshapita baadhi ya vijana walifunga
tena barabara na ndipo Jeshi la Polisi lilipolazimika kuwatawanya na
kuwakama vijana saba.
Waandishi wa habari wa Televisheni za Star TV, Channel
Ten na TBC wanamikanda ya tukio zima na hivyo mikanda hiyo inaweza kuthibitisha
habari kuwa mhe Nchimbi alipigwa mawe ni uzushi mtupu.
Waziri Nchimbi alikuwa katika ziara ya kawaida jimboni
kwake na aliweza kufanya mikutano minane ya hadhara iliyohudhuriwa na
mamia ya watu na iliendeshwa kwa utulivu mkubwa ambapo wenyeviti wa
mikutano hiyo walikuwa madiwani wa kata husika, ambapo katika kata sita
mikutano hiyo iliongozwa na madiwani wa CCM na kata mbili iliongozwa
na madiwani wa Chadema.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inavisihi vyombo
vya habari na mitandao ya kijamii kujiridhisha na ukweli wa taarifa
wanazozipata kabla ya kuzitoa kwa wananchi ili wananchi waweze kupata
haki yao ya kupata habari zilizokuwa sahihi.
Mwisho.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Ndani ya Nchi
28 Oktoba,
2013
No comments:
Post a Comment