Header Ads

Ulinzi mkali kwa Mwenyekiti UVCCM

Sadifa Juma Khamis, Mwenyekiti wa UVCCM Taifa
Hali  siyo shwari ndani ya mkutano wa Baraza kuu la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) baada ya  mwenyekiti wa umoja huo, Sadifa Juma Khamis kuonekana akishuka ndani ya gari katika makao makuu ya chama hicho akiwa na walinzi jambo ambalo si la kawaida.

 NIPASHE ilishuhudia mwenyekiti huyo akishuka ndani ya gari akiwa na walinzi hao wawili ambao wamevaa kiraia jambo ambalo si la kawaida kwa kiongozi huyo wa UVCCM.

Kabla ya kuanza kwa kikao hicho jana mjini hapa, kilitanguliwa na kamati ya utekelezaji ya UVCCM kilichoanza juzi na kumalizika leo (jana) na baadaye kufuatiwa na baraza hilo.

Hata hivyo, baraza hilo ambalo lilitakiwa kuanza jana saa 5 asubuhi lilichelewa kuanza huku baadhi ya wajumbe wakionekana wakirandaranda huku wengine wakiwa wamekaa kwenye makundi mbalimbali.

Aidha, NIPASHE ilishuhudia baadhi ya wajumbe hao wakiwa wamesimama kwenye makundi huku wakimjadili mwenyekiti huyo wakidai kuwa hana ushirikiano na viongozi wenzake na wengine wakitaka aachie ngazi.

Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Donge, analalamikiwa na baadhi ya wajumbe hao kutokana na matatizo mbalimbali ya kiutawala, matumizi mabaya ya fedha na usimamizi mbovu wa mali za umoja huo.

Mmoja wa wajumbe hao ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema uongozi wa mwenyekiti huyo umefikia ukingoni kwani mara kwa mara amekuwa akifanya ‘madudu’.
 “Huyu amekuwa ni tatizo ndani ya umoja huu…kwani sasa hivi hali imekuwa si shwari…amekuwa mharibifu, anatukana wenzake yaani amekuwa ni tatizo kwa hiyo ni lazima ang’oke,” alisema.

Akizungumza kabla ya kufungua mkutano huo, Katibu Mkuu wa umoja huo, Sixtus Mapunda, alisema kikao hicho kilitarajiwa kujadili masuala ya ndani ya umoja huo na kuwataka waandishi wa habari kutoka nje ya ukumbi.

“Kwa maana hiyo wale waliosomwa kwenye ibara ya 88 ndiyo wanaotakiwa kubaki kwenye ukumbi wetu ila kwa wale waandishi wa habari na wageni waalikwa tunaomba watupishe kwenye kikao hiki kwa sababu kina uzito mkubwa,” alisema Mapunda.

Hata hivyo, habari ambazo NIPASHE ilizipata baadaye zinaeleza kuwa Sadifa aliwaomba msamaha wajumbe pamoja na wanachama wa UVCCM kutokana na yote yaliyojitokeza na kuwataka wayasahau ili umoja huo usonge mbele.

Katika kudhihirisha nia yake ya kutaka mwafaka, Sadifa alimteua hasimu wake, Paul Makonda, kuwa katibu wa Oganaizesheni na Uhamasishaji wa UVCCM, nafasi ambayo ni nyeti kwa jumuiya hiyo.

Katika uchaguzi mkuu wa UVCCM mwaka jana, Makonda aligombea nafasi ya umakamu mwenyekiti, lakini alishindwa na Mboni Mhita.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Powered by Blogger.