Header Ads

16/6/2011 Leo ni siku ya Mtoto wa Afrika

                 Serikali haishabikii vituo vya watoto wa mitaani 


Leo ni siku ya Mtoto wa Afrika. Wakati tunaadhimisha siku hii, Serikali imetoa msimamo wake kuhusu vituo vya kulelea watoto wa mitaani na kusema haipendelei watoto kuwekwa katika vituo hivyo.Badala yake imesema, jamii inatakiwa kutafuta ufumbuzi wa tatizo la watoto wa mitaani ili kuepusha uwepo wa vituo hivyo.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Watoto katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Bi Tukae Njiku ametoa msimamo huo kwa niaba ya Waziri wa wizara hiyo jana jijini Dar Es Salaam wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu kilele cha siku ya mtoto wa Afrika.
 “Serikali haisisitizi kuweka watoto kwenye vituo. Kufanya hivyo iwe ni hatua ya mwisho wakati unatafutwa ufumbuzi wa tatizo la watoto wa mitaani,” amesema.
Katika mkutano huo ulioudhuriwa na watendaji wengine wa wizara hiyo, Bibi Tukae ameeleza kuwa vituo vya watoto yatima lazima viwesajili na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
 “Kama kituo kipo, serikali itataka kujua kama kimesajiliwa, baada ya kujiridhisha kuwa kinafaa kulelea watoto. Lakini kama kituo kinafanyakazi bila kusajiliwa, kituo hicho ni batili na kinatakiwa kufungwa,” amesema.
Takwimu zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO) zinaonyesha kuwa watoto wa mitaani duniani wanakadiriwa kufikia milioni 120, milioni 30 kati ya hao wako barani Afrika.Aidha utafiti uliofanywa Shirika lisilo la kiserikali Consortium for Street Children mwaka 2009 yanayoonyesha kuwepo sababu mbalimbali zinazochangia kuongezeka kwa watoto wa mitaani nchini.
Kwa mujibu wa utafiti huo, ukatili dhidi ya watoto unachangia kuwepo kwa asilimia 50 za watoto wanaoishi mitaani, njaa na umaskini  35%, ukosefu wa upendo 11% na kuvunjika kwa familia 4%.  
Siku ya Mtoto wa Afrika uadhimishwa na nchi zote wanachama wa Umoja wa Afrika kwa mujibu wa Azimio lililopitishwa na Umoja huo mwaka 1990. hapa nchini kila mkoa utaadhimisha siku hii kwa kushirikisha Halmashauri zake pamoja na tarafa, kata na vitongoji.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni
Tuungane kwa pamoja kuchukua hatua za haraka kushughulikia tatizo la watoto wanaoishi mitaani.”

No comments:

Powered by Blogger.