|
Wednesday, 20 April 2011 14:22 | |
Hawra Shamte KATIBA ya nchi kwa kiasi kikubwa inaainisha itikadi inayohalalishwa utawala na matumizi ya madaraka kwa upande wa tabaka-tawala dhidi ya matabaka-tawaliwa. Kwa mujibu wa nadharia, falsafa na itikadi ya kiliberali, katiba ndio medani pekee ya kujenga, kukuza na kuhakikisha mwafaka kati ya watawala na watawaliwa. Profesa wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Issa Shivji anasema kuwa katiba ndio chimbuko la uhalali wa kisheria (legal authority) na uhalali wa kisiasa (political legitimacy). Profesa Shivji anasema kuna aina ya mshikamano kati ya uhalali wa kisheria na uhalali wa kisiasa, hivyo ndiyo kusema kuwa utungaji wa katiba siyo kazi ya kitaaluma tu, bali ni medani ya mapambano ya kisiasa. “Uzuri au ubaya wa katiba hauwezi ukapimwa na upeo wa kitaaluma pekee, bali hubainika pale katiba inapopata mwafaka katika jamii husika. Hivyo katiba yapaswa kujenga mwafaka katika jamii. Profesa Shivji anasema tatizo linaloonekana katika mifumo ya siasa barani Afrika ni kuwa katiba imekuwa chombo cha kugawa madaraka/nguvu za dola bila kuzingatia chimbuko la kujenga na kukuza mwafaka. Hata hivyo Profesa Shivji anasema yawezekana katiba ikawa na uhalali wa kisheria na isiwe na uhalali wa kisiasa, au ikawa na uhalali wa kisiasa isiwe na uhalali wa kisheria. Anasema uhalali wa kisiasa katika katiba unapatikana kutokana na ushiriki wa wananchi au makundi maslahi katika katiba yenyewe kwa sababu katiba ni mkataba kati ya wananchi na serikali yao kuhusu vipi wanataka waongozwe. Profesa Shivji anasema mara nyingine watawala hupata uhalali si kutokana na matakwa ya wananchi bali uhalali wao wa kutawala hutokana na mtutu wa bunduki au itikadi zisizo za kikatiba au za kisheria, hususan kupitia itikadi za kiuchumi. Kwa mfano; nchini Tanzania uhalali wa utawala ulitokana na itikadi ya Azimio la Arusha na siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na siyo katiba. “Kwa hivyo, utungaji/urekebishaji wa katiba ya nchi haukuwa na umuhimu wa kujenga mwafaka bali ulikuwa kurekodi hali halisi ya mgawanyo na matumizi ya madaraka katika sura yake ya nguvu za dola,” anaeleza Profesa Shivji. Historia ya mabadiliko ya Katiba Tanzania Tangu Tanzania ipate uhuru wake kumetungwa tano mpya na kufanyika marekebisho mengi ya mara kwa mara. Profesa Shivji anasema Katiba ya mwaka 1977 ambayo ndiyo inayotumika hadi leo nchini Tanzania ni Katiba iliyosimikwa kutokana na nguzo kuu tatu ambazo ni mfumo wa urais wa kifalme (imperial presidency), muungano wa serikali mbili na mfumo wa chama kimoja. Katiba ya Uhuru 1961 Profesa Shivji anasema umuhimu wa katika ya mwaka 1961 ni kwa kuwa ilikuwa kama njia ya kutoa uhuru kwa Tanganyika. “Kwa wananchi na viongozi wao, katiba hii haikuwa mwafaka wa siasa kati ya watawala wa ndani na watawaliwa bali ilikuwa hitimisho la mapambano ya kitaifa dhidi ya ukoloni. Katiba hii ilitungwa na wataalam wa ofisi ya koloni huko Uingereza na katiba iliwekwa kama nyongez (schedule) ya Sheria ya Uhuru wa Tanganyika iliyopitishwa na Bunge la Uingereza. “Katiba ya mwaka 1961 ilifuata muundo wa demokrasia ya Westminster. Mkuu wan chi aliendelea kuwa Malkia akiwakilishwa na Gavana; mtekelezaji mkuu wa nchi alikuwa Waziri Mkuu ambaye aliteuliwa kutokana na chama chenye viti vingi bungeni. Katiba hii iliweka mfumo wa demokrasia ya kiliberali ikiiga mfumo wa kisiasa wa Uingereza. Katiba ya Jamhuri 1962 Mwaka 1962 serikali Serikali ya Tanganyika ilitangaza Jamhuri na ikatunga katiba ya mwaka 1962, yaani Katiba ya Jamhuri.” Profesa Shivji anasema ingawa hakukuwa na mjadala wa kitaifa juu ya mabadiliko hayo, serikali ilitoa mapendekezo yake katika ‘white paper’Kwa muendelezo wa habari hii bonyeza hapa..... |
No comments:
Post a Comment