GLOBAL EDUCATION LINK WAISAIDIA SERIKALI KUZALISHA RASILIMALI WATU WENYE UJUZI.
Taasisi
ya Global Education Link imeisaidia Serikali kuzalisha rasilimali watu wenye
ujuzi na elimu ya kutosha ili watumike katika kuinua viwanda na uchumi wa nchi.
Hayo
yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo,
Abdulmaliki Mollel alipokuwa akiongea na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi
wa maonesho ya kwanza ya viwanda Tanzania yaliyofanyika katika viwanja vya Sabasaba
vilivyopo jijini humo.
Mollel
amesema kuwa Tanzania imeamua kuwa nchi ya viwanda lakini bila kuwa na
rasilimali watu wenye ujuzi na elimu ya kutosha kuhusu uzalishaji na
uendelezaji wa viwanda hakutakuwa na maendeleo kwani maendeleo yoyote mzizi wake
ni elimu na ujuzi.
“Kuna baadhi ya masomo ambayo ni muhimu hayapatikani
katika vyuo vya Tanzania na kama zinapatikana basi nafasi ni chache
hivyo,taasisi hii ni kama daraja la kutengeneza rasilimali watu wenye ubora
watakaoleta maendeleo ya nchi kupitia kusoma nchi za nje,”alisema Mollel.
Ameongeza
kuwa ili nchi ipate maendeleo kwa haraka ni lazima isaidiwe na taasisi na
mashirika binafsi na ndio maana taasisi hiyo imeamua kuisaidia Serikali kwa
kuwarahisishia Watanzania kupata elimu nje ya nchi ambayo itasaidia Serikali
kupunguza matumizi pamoja na kuzuia wataalamu wa nchi za nje kufanya kazi
nchini.
Mkurugenzi
huyo amefafanua kuwa mpaka sasa chuo hicho kimeshatoa wanafunzi takribani 5400
ambao wengi wao wameshika nyazfa mbalimbali kwenye taasisi za Umma na Binafsi.
Aidha,
taasisi hiyo ina mpango wa kuandaa programu za miezi 4 hadi 6 ambazo zitakuwa
maalum kwa ajili ya kuongeza ujuzi kwa wafanyakazi kwa kupitia elimu ya vitendo kwenye viwanda
mbalimbali vilivyoko nchini India.
Taasisi
hiyo imeanzishwa mnamo mwaka 2006 ikiwa na lengo la kurahisisha mchakato na
kuwaondolea usumbufu wanafunzi wanaohitaji kwenda kusoma nje ya nchi pamoja na
kuwasaidia wanafunzi kutimiza ndoto zao.
No comments:
Post a Comment