Header Ads

TAASISI 145 HAZIJAWASILISHA TAARIFA IWAPO WANA WATUMISHI HEWA AU HAWANA WATUMISHI HEWA,MWISHO KUWASILISHA TAARIFA ZAO NI AGOSTI 26,2016


 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.  Angellah J.  Kairuki (Mb) akitoa taarifa kwa Vyombo vya Habari  kuhusu zoezi la kuondoa watumishi hewa katika orodha ya malipo ya mishahara serikalini ofisini kwake mapema leo.
 Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.  Angellah J. Kairuki (Mb)  alipozungumza leo ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.  Angellah J.  Kairuki (Mb) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawako pichani) kuhusu utekelezaji wa agizo la kuondoa watumishi hewa katika orodha ya malipo ya mishahara Serikalini ofisini kwake mapema leo.





Kama mnavyokumbuka, mnamo tarehe 15 Machi, 2016 Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwaagiza Wakuu wa Mikoa na Waajiri wote kwa ujumla kuchukua hatua ya kuhakikisha katika Mikoa au Taasisi zao hakuna watumishi hewa ifikapo tarehe 30 Machi, 2016.
Katika kutekeleza agizo hilo la Mheshimiwa Rais, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imekuwa ikifuatilia utekelezaji wa agizo hili na mnamo tarehe 26 Mei, 2016 waajiri wote waliagizwa kuwasilisha taarifa za mwisho za zoezi la kuwabaini na kuwaondoa watumishi hewa katika orodha za malipo ya mshahara (payroll) ifikapo mwisho wa Mwezi Juni, 2016. Waajiri wote walielekezwa kutuma taarifa tajwa kwa kuzingatia muundo wa uandaaji na uwasilishaji wa taarifa hizo kwa kuainisha mambo yafuatayo:-
·        Jina la Taasisi;
·        Fungu (Vote);
·        Cheki Namba ya Mtumishi;
·        Jina Kamili la Mtumishi;
·        Cheo cha Mtumishi;
·        Jina la Tawi la Benki ambalo mshahara wa mtumishi umekuwa ukipitishwa/ukilipwa;
·        Akaunti Namba ya Benki ya Mtumishi;
·        Tarehe ambayo Mtumishi aliondolewa kwenye Mfumo wa Taarifa ya Kiutumishi na Mshahara;
·        Kiasi cha fedha zilizolipwa kwa mtumishi husika tangu alipotakiwa kuondolewa hadi tarehe aliyoondolewa kwenye Mfumo;
·        Sababu ya kuondolewa kama utoro, kufariki dunia, kuacha kazi, kustaafu n.k.
·        Hatua zilizochukuliwa na mwajiri dhidi ya watumishi hwa waliobainika kama kurejesha fedha, na Maafisa wengine wa Taasisi husika waliosababisha uwepo wa Watumishi Hewa kuwachukulia wahusika hatua za kinidhamu/kisheria.
Aidha, waajiri 264 kati ya waajiri wote 409 wamewasilisha taarifa zao kuhusu uwepo wa watumishi hewa. Kati ya waajiri 264 waliowasilisha taarifa zao, waajiri 63 wamethibitisha kwamba hawana watumishi hewa katika Taasisi zao na waajiri 201 wana watumishi hewa mmoja (1) na kuendelea.
Katika kufanikisha zoezi hili Ofisi yangu imechukua hatua kadhaa ikiwemo kuendelea kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa Maafisa Utumishi wenye dhamana ya kutumia Mfumo wa Malipo ya Mshahara, kukuza uwajibikaji kwa Maafisa wanaosimamia malipo ya mishahara kwa kuwachukulia hatua za kinidhamu/kisheria wanaobainika kusababisha watumishi hewa, kufanya uhakiki wa kushtukiza na kuanza safari ya kuunganisha Mfumo wa Malipo ya Mishahara na mifumo mingine mikubwa kama ya NIDA, RITA na Baraza la Mitihani la Taifa, na kuwezesha mfumo kuwaondoa moja kwa moja (automatically) watumishi waliofikisha umri wa kustaafu kwa lazima.
Pamoja na taarifa hiyo, zipo Taasisi 145 ambazo hazijawasilisha taarifa iwapo wana watumishi hewa au hawana watumishi hewa. Waajiri ambao hawajawasilisha taarifa zao wamegawanyika katika makundi yafuatayo:-
·        Mabaraza mbalimbali                                        11
·        Bodi mbalimbali                                                  10
·        Vyuo Vikuu                                                          25
·        Hospitali                                                                3
·        Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa                 12
·        Mamlaka mbalimbali                                            6
·        Tume mbalimbali                                               10
·        Mamlaka za Serikali za Mitaa                           38
·        Taasisi za Umma na Wakala                            30
Aidha, kuanzia tarehe 15 Agosti, 2016 Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inaendesha zoezi la uhakiki wa kushtukiza katika Taasisi sabini (70) za Serikali zikiwepo Wizara, Idara za Serikali Zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi za Umma kwa madhumuni ya kujiridhisha kwamba taarifa za watumishi hewa zilizowasilishwa na waajiri ni sahihi.
Vilevile, napenda kuwataarifu pia kwamba taarifa kamili ya watumishi hewa itatolewa baada ya kupata taarifa hizo kutoka kwa waajiri ambao hawajawasilisha taarifa hizo na kukamilika kwa zoezi la uhakiki wa Taasisi sabini (70) linaloendelea sasa. Naagiza Taasisi zote hazijawasilisha Taarifa za Watumishi Hewa kufanya hivyo kabla au ifikapo tarehe 26 Agosti, 2016.
Ofisi hii itawasilisha taarifa rasmi ya watumishi hewa kwa Mheshimiwa Rais ikiwa na orodha na majina ya Taasisi ambazo zimewasilisha taarifa ya watumishi hewa na na zile ambazo hazijawasilisha taarifa hizo.
Taarifa hizo ziwasilishwe kwa kuzingatia mfumo uliotolewa katika barua ya tarehe 26 Mei, 2016 kwa nakala ngumu na nakala laini (Soft Copy/Hard Copy) kupitia anuani ya barua pepe ps@utumishi.go.tz. Na kwa nakala ngumu iwasilishwe Ofisi ya Katibu Mkuu (Utumishi).
Imetolewa na Mhe. Angellah J. Kairuki (MB.) WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA
 NA UTAWALA BORA,
20 AGOSTI, 2016

No comments:

Powered by Blogger.