PROF. MBARAWA AZUNGUMZA NA WADAU WA MAENDELEO.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akimsikiliza
mjumbe wa wadau wa maendeleo katika kikao kazi kujadili namna ya
kushirikiana katika ujenzi wa miundombinu ya kisasa nchini, kikao hicho
kimefanyika Jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi
Msaidizi Ufuatiliaji na Tathmini (Sekta ya Uchukuzi), Bw. Aunyisa Meena
akifafanua jambo katika kikao kazi kujadili namna ya kushirikiana
katika ujenzi wa miundombinu ya kisasa baina ya viongozi wa Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na wadau wa maendeleo, Jijini Dar es
salaam.
Wadau
wa Maendeleo kutoka Benki ya Dunia (WB), Umoja wa Ulaya (EU), Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Shirika la Maendeleo la Japani (JICA)
wakisikiliza maelezo ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Profesa Makame Mbarawa (hayupo pichani) kuhusu mikakati ya Serikali
kuimarisha miundombinu na kukuza uchumi katika kikao cha pamoja
kilichofanyika jijini Dar es salaam.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akifafanua
jambo kwa wadau wa maendeleo katika kikao kazi kujadili namna ya
kushirikiana katika ujenzi wa miundombinu ya kisasa nchini, kikao hicho
kimefanyika Jijini Dar es salaam.
Picha na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (W-UUM).
WAZIRI
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa
amewahakikishia wadau wa Maendeleo kuwa Serikali ya Awamu ya Tano iko
tayari kupokea changamoto na ushauri utakaoiwezesha kutimiza adhma yake
ya kuwa na miundombinu bora na yakisasa itakayoiwezesha nchi kufikia
uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Akizungumza
katika kikao cha pamoja kati ya wataalam wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano na wadau wa Maendeleo kutoka Benki ya Dunia (WB), Umoja
wa Ulaya (EU), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Shirika la
Maendeleo la Japani (JICA), Prof. Mbarawa amewahakikishia wadau hao wa
maendeleo kuwa wizara yake inatarajia ushirikiano mkubwa hususani katika
sekta ya ujenzi wa reli, barabara, bandari na viwanja vya ndege.
“Sekta
ya Ujenzi, uchukuzi na mawasiliano inachukua asilimia kubwa ya bajeti
ya nchi yetu hivyo licha ya jitihada na misaada mnayotupa bado tupo
tayari kupokea misaada, changamoto na ushauri ili ituwezeshe kukamilisha
kwa wakati na ubora miradi ya ujenzi inayoendelea na tunayotarajia
kuianzisha”, amesema Prof. Mbarawa.
Profesa
Mbarawa amesisitiza kwamba Serikali imejipanga kudhibiti rushwa ili
fedha nyingi zinazotumika katika miundombinu ilete matokeo chanya na
kuwahakikishia kwamba ujenzi wa reli ya kisasa ya kati (Standard Gauge),
itaanza baadaye mwaka huu na ikikamilika itapunguza gharama kubwa za
usafirishaji zinazotumika kupitia malori.
Profesa
Mbarawa amewashukuru wadau wa maendeleo kwa misaada mbalimbali
wanayotoa katika sekta ya ujenzi wa barabara na ukarabati wa reli mara
kwa mara na kusisitiza kwamba Serikali inatambua na kuthamini michango
hiyo na kuomba washirikiane katika ujenzi wa reli ya kisasa ya kati
(Standard gauge).
Zaidi
ya kilomita 2600 za Reli ya Kisasa (Standard gauge) zinatarajiwa
kujengwa kutoka Dar es Salaam-Morogoro-Dodoma-Tabora-Isaka hadi Mwanza
ambayo ni uti wa mgongo wa reli hiyo.
Na
Sehemu nyingine ni kutoka Tabora-Mpanda hadi Kalemela na Tabora-Uvinza
hadi Kigoma ambayo itaunganisha na nchi za Rwanda na Burundi na hivyo
kufungua huduma za kiuchumi na uchukuzi kati ya Tanzania na nchi za
maziwa makuu.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment