Header Ads

Benki ya Exim yazindua kampeni kuhamasisha huduma bora kwa wateja

 Meneja Masoko Msaidizi wa Benki ya Exim Tanzania Mariam Mwapinga akisisitiza jambo mbele ya waandishi (hawapo pichani)  kuhusu kampeni maalumu kuhamasisha matumizi ya kituo  cha  huduma  kwa wateja kwa njia ya mawasiliano ya simu cha benki hiyo jijini Dar es Salaam hivi karibuni.. Wengine ni pamoja na Mkuu wa kitengo cha hazina wa benki hiyo , Bw. George Shumbusho (katikati) na Meneja Mwandamizi Huduma kwa wateja  wa Benki hiyo Bw. Frank Matoro (kushoto).
Mkuu wa kitengo cha hazina benki ya Exim Tanzania , Bw. George Shumbusho (kulia), akikata utepe kuzindua kampeni maalumu kuhamasisha matumizi ya kituo cha  huduma  kwa wateja kwa njia ya mawasiliano ya simu cha benki hiyo jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Wanaoshuhudia ni pamoja Meneja Mwandamizi Huduma kwa wateja  wa Benki hiyo Bw. Frank Matoro (kushoto).

BENKI ya Exim Tanzania imezindua kampeni maalumu kuhamasisha matumizi ya kituo chake cha  huduma  kwa wateja kwa njia ya mawasiliano ya simu ikiwa ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo kuhakikisha inawarahisishia wateja wake upatikanaji wa huduma  zake kupitia  teknolojia ya mawasiliano.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki wakati wa hafla fupi ya kuzindua kituo hicho,  Meneja Mwandamizi Huduma kwa wateja  wa Benki hiyo Bw. Frank Matoro alisema matumizi ya kituo hicho  yatawawezesha wateja wa benki hiyo kupata taarifa za kina kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo.
“Ni matarajio yetu kwamba wateja wetu watafurahia zaidi huduma bora kutoka kwa wahudumu wenye vigezo na uelewa wa kutosha kuhusiana na masuala ya kibenki kila siku za Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 1:00 jioni na siku za Jumamosi kuanzia saa 3 kamili asubuhi hadi saa 7:00 mchana kupitia namba yetu ya 0784 107 600,’’ alisema.
Kwa mujibu wa Bw Matoro kituo hicho tayari kimekwisha anza kutoa huduma huku akibainisha kuwa malengo ya kampeni hiyo ni kuhakikisha wateja wa benki hiyo wanatambua uwepo wa kituo hicho na kutumia ipasavyo huduma zitolewazo na kituo hicho.
“Katika kuhakikisha kwamba kampeni hii inaleta mafanikio, itaambatana na  droo ndogo ndogo zitakazowezesha utoaji wa zawadi mbalimbali kwa wateja  zikiwemo fulana zenye nembo ya benki, muda wa maongezi pamoja na simu mpya aina ya iPhone 5s,’’ alitaja.
Aliongeza kuwa huduma zinazotolewa na kituo hicho zinatolewa kupitia mazungumzo kwa njia simu, mitandao ya kijamii ikiwemo ukurasa wa Facebook na njia nyingine za kimtandao kama vile website na barua pepe.
Bw. George Shumbusho, mkuu wa kitengo cha hazina aliongeza kwamba: “Pia tunatarajia kwamba mafanikio ya huduma hii yatatuongezea ukubwa wa soko kwa kuwa itapanua wigo wa kuwafikia wateja, kujiongezea ukuaji wa fursa  sambamba na kutoa fursa kwa wateja wetu waweze kutupa mrejesho wa huduma mbalimbali tunazowapatia,’’

No comments:

Powered by Blogger.